19
Vita dhidi ya Waamoni
(2 Samweli 10:1-19)
1 Baada ya muda, Nahashi mfalme wa Waamoni akafa, na mwanawe akawa mfalme baada yake. 2 Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kwa sababu baba yake alinitendea wema.”
Hivyo Daudi akatuma wajumbe ili kumfariji Hanuni kwa ajili ya kifo cha baba yake. Watu wa Daudi walipofika kwa Hanuni katika nchi ya Waamoni ili kumfariji, 3 wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni, “Hivi unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kuwatuma wajumbe kukufariji? Je, hawa watu hawakuja kuipeleleza na kuidadisi nchi ili waishinde?” 4 Kwa hiyo Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa ndevu, akakata nguo zao katikati kwenye matako, akawaachia waende zao.
5 Mtu mmoja alipofika na kumpasha Daudi habari za watu hawa, akawatuma wajumbe wengine kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko hadi ndevu zenu ziote, ndipo mje.”
6 Waamoni walipotambua kwamba wamekuwa machukizo kwa Daudi, basi Hanuni na Waamoni wakatuma talanta elfu moja*Talanta 1,000 ni sawa na tani 34. za fedha ili kukodisha magari ya vita, pamoja na waendeshaji wa hayo magari ya kukokotwa na farasi, kutoka Mesopotamia, Aram-Maaka na Soba. 7 Wakakodisha magari ya vita elfu thelathini na mbili na waendeshaji wake, pamoja na mfalme wa Maaka na vikosi vyake. Wakapiga kambi karibu na Medeba. Waamoni nao wakakusanyika toka miji yao, wakatoka ili kupigana vita.
8 Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji. 9 Waamoni wakatoka, wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati wale wafalme wengine waliokuja nao walijipanga kwa vita uwanjani.
10 Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli, akavipanga dhidi ya Waaramu. 11 Akawaweka wale wanajeshi wengine waliobaki chini ya amri ya Abishai ndugu yake, nao wakapangwa ili wakabiliane na Waamoni. 12 Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itakupasa wewe uniokoe; lakini kama Waamoni watakuzidi nguvu, basi mimi nitakuokoa. 13 Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Mwenyezi Mungu atafanya lile lililo jema machoni pake.”
14 Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake. 15 Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao pia wakakimbia mbele ya nduguye Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi Yerusalemu.
16 Baada ya Waaramu kuona kwamba wameshindwa na Israeli, wakapeleka wajumbe na kuwataka Waaramu wengine kutoka ng’ambo ya Mto†yaani Mto Frati, wakiongozwa na Shofaki, jemadari wa jeshi la Hadadezeri.
17 Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote na kuvuka Yordani. Akasonga mbele dhidi yao na akajipanga kuwakabili. Daudi akapanga vita ili kupigana na Waaramu, nao wakapigana dhidi yake. 18 Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari ya vita elfu saba, na askari wa miguu elfu arobaini. Pia akamuua Shofaki, jemadari wa jeshi lao.
19 Raia wa Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya mapatano ya amani na Daudi, wakawa watumishi wake.
Hivyo Waaramu hawakukubali kuwasaidia Waamoni tena.