6
Sulemani ajenga Hekalu
(2 Nyakati 3)
Katika mwaka wa mia nne na themanini baada ya Waisraeli kutoka nchi ya Misri, katika mwaka wa nne wa utawala wa Sulemani katika Israeli, katika mwezi wa Zivu*mwezi wa tano katika kalenda ya Kiyahudi, uliokuwa mwezi wa pili, alianza kujenga Hekalu la Mwenyezi Mungu.
Hekalu ambalo Mfalme Sulemani alilijenga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu lilikuwa na urefu wa dhiraa sitiniDhiraa 60 ni sawa na mita 27., upana wa dhiraa ishiriniDhiraa 20 ni sawa na mita 9., na kimo cha dhiraa thelathini§Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5. kwenda juu. Baraza iliyokuwa mbele ya ukumbi mkuu wa Hekalu iliongeza upana wa Hekalu kwa dhiraa ishirini, na kuchomoza dhiraa kumi mbele ya Hekalu. Akatengeneza madirisha membamba katika Hekalu. Akajenga vyumba vya pembeni kulizunguka Hekalu lote, vikishikamana na kuta za ukumbi wa Hekalu na za Patakatifu pa Patakatifu. Ghorofa ya chini kabisa ilikuwa na upana wa dhiraa tano*Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25., ya kati ilikuwa dhiraa sitaDhiraa 6 ni sawa na mita 2.7., na ya tatu ilikuwa dhiraa sabaDhiraa 7 ni sawa na mita 3.15.. Kuzunguka ukuta wa nje wa Hekalu akapunguza ukuta pande zote ili boriti zisishikane kwenye kuta za Hekalu.
Katika kujenga Hekalu, yalitumika tu mawe yaliyochongwa huko machimboni, wala hakuna nyundo, patasi au chombo kingine chochote cha chuma kilichosikika katika eneo la ujenzi wa Hekalu wakati lilipokuwa likijengwa.
Ingilio la ghorofa ya chini kabisa lilikuwa upande wa kusini wa Hekalu; ngazi ilielekea ghorofa ya kati na kutoka hapo ilielekea hadi ghorofa ya tatu. Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha, akiliweka paa za boriti na mbao za mwerezi. 10 Mfalme Sulemani akajenga vyumba vya pembeni kuzunguka Hekalu lote. Kimo cha kila kimoja kilikuwa dhiraa tano. Navyo vilikuwa vimeunganishwa na Hekalu kwa boriti za mwerezi.
11 Neno la Mwenyezi Mungu likamjia Sulemani kusema: 12 “Kuhusu Hekalu hili unalojenga, kama ukifuata amri zangu, ukatunza masharti yangu na kushika maagizo yangu yote na kuyatii, nitatimiza kupitia kwako ahadi niliyomwahidi Daudi baba yako. 13 Nami nitakaa miongoni mwa Waisraeli, nami sitawaacha watu wangu Israeli.”
14 Basi Sulemani akajenga Hekalu na kulikamilisha. 15 Akazifunika kuta zake za ndani kwa mbao za mwerezi, akizipigilia ukutani kuanzia sakafuni mwa Hekalu hadi kwenye dari, na kufunika sakafu ya Hekalu kwa mbao za misunobari. 16 Akagawa dhiraa ishirini sehemu ya nyuma ya Hekalu kwa mbao za mwerezi kuanzia kwenye sakafu hadi darini ili kufanya sehemu takatifu ya ndani, yaani Patakatifu pa Patakatifu. 17 Ukumbi mkuu uliokuwa mbele ya chumba hiki ulikuwa na urefu wa dhiraa arobaini§Dhiraa 40 ni sawa na mita 18.. 18 Ndani, Hekalu lilipambwa na mbao za mwerezi zilizonakshiwa mifano ya maboga na maua yaliyochanua. Kila kitu kilikuwa cha mwerezi; hakuna jiwe ambalo lilionekana.
19 Ndani ya Hekalu akatengeneza mahali patakatifu pa kuliweka Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu. 20 Mahali patakatifu palikuwa na urefu wa dhiraa ishirini, upana wa dhiraa ishirini, na kimo cha dhiraa ishirini. Akapafunika upande wa ndani, na madhabahu ya mwerezi pia, kwa dhahabu safi. 21 Sulemani akalifunika Hekalu upande wa ndani kwa dhahabu safi, na akaitandaza mikufu ya dhahabu kutoka upande mmoja hadi ule mwingine mbele ya mahali patakatifu, palipofunikwa kwa dhahabu. 22 Basi akafunika upande wote wa ndani kwa dhahabu. Pia akafunika kwa dhahabu yale madhabahu yaliyokuwa ndani ya mahali patakatifu.
23 Katika mahali patakatifu, akatengeneza makerubi wawili kwa mzeituni, kila moja likiwa na dhiraa kumi*Dhiraa 10 ni sawa na mita 4.5. kwenda juu. 24 Bawa moja la kerubi wa kwanza lilikuwa na urefu wa dhiraa tano na bawa jingine dhiraa tano, hivyo urefu kutoka ncha ya bawa moja hadi ncha ya bawa jingine ulikuwa dhiraa kumi. 25 Kerubi wa pili alikuwa na urefu wa dhiraa kumi pia, kwa kuwa makerubi hao wawili walifanana kwa vipimo na kwa umbo. 26 Kimo cha kila kerubi kilikuwa dhiraa kumi. 27 Aliwaweka makerubi hao katika chumba cha ndani kabisa cha Hekalu, mabawa yao yakiwa yamekunjuliwa. Bawa la kerubi mmoja liligusa ukuta mmoja, wakati bawa la yule mwingine liligusa ukuta wa upande mwingine, nayo mabawa yao mengine yaligusana katikati ya chumba. 28 Akafunika wale makerubi kwa dhahabu.
29 Kuta zote za Hekalu, za vyumba vya ndani na vya nje, zilipambwa kwa nakshi za makerubi, mitende na maua yaliyochanua. 30 Pia alifunika sakafu zote za vyumba vya ndani na vya nje vya Hekalu kwa dhahabu.
31 Katika ingilio la mahali patakatifu sana, alitengeneza milango ya mbao za mzeituni, yenye miimo ya sehemu moja ya tano ya upana wa madhabahu. 32 Kwenye milango hiyo miwili ya mbao za mzeituni, alinakshi makerubi, mitende, pamoja na maua yaliyochanua, na kufunika makerubi na mitende kwa dhahabu iliyofuliwa. 33 Kwa namna hiyo hiyo, alitengeneza miimo kwa mbao za mzeituni yenye upana wa robo ya upana wa ukumbi mkuu kwa ajili ya ingilio la ukumbi huo. 34 Pia akatengeneza milango miwili kwa mbao za msunobari, kila mmoja ukiwa na vipande viwili ambavyo vilikunjwa kwa bawaba. 35 Akanakshi makerubi, mitende na maua yaliyochanua juu yake, na kufunika kwa dhahabu iliyonyoshwa vizuri juu ya michoro.
36 Tena akajenga ua wa ndani safu tatu za mawe yaliyochongwa, na safu moja ya boriti za mwerezi zilizosawazishwa.
37 Msingi wa Hekalu la Mwenyezi Mungu uliwekwa katika mwaka wa nne, katika mwezi wa Zivu. 38 Katika mwaka wa kumi na moja, mwezi wa Buli, ndio mwezi wa nane, Hekalu lilikamilika katika hatua zake zote kwa kufuatana na maelekezo yake Sulemani. Alilijenga kwa miaka saba.

*6:1 mwezi wa tano katika kalenda ya Kiyahudi

6:2 Dhiraa 60 ni sawa na mita 27.

6:2 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9.

§6:2 Dhiraa 30 ni sawa na mita 13.5.

*6:6 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25.

6:6 Dhiraa 6 ni sawa na mita 2.7.

6:6 Dhiraa 7 ni sawa na mita 3.15.

§6:17 Dhiraa 40 ni sawa na mita 18.

*6:23 Dhiraa 10 ni sawa na mita 4.5.