8
Sanduku la Agano laletwa Hekaluni
(2 Nyakati 5)
1 Kisha Mfalme Sulemani akawaita mbele zake huko Yerusalemu wazee wa Israeli, viongozi wote wa makabila na wakuu wa jamaa za Waisraeli, ili walilete Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu kutoka Sayuni, Mji wa Daudi. 2 Wanaume wote wa Israeli wakakusanyika kwa Mfalme Sulemani wakati wa sikukuu ya mwezi wa Ethanimu, ndio mwezi wa saba.
3 Wazee wote wa Israeli walipofika, makuhani wakajitwika lile Sanduku, 4 nao wakalipandisha Sanduku la Mwenyezi Mungu, na Hema la Kukutania, pamoja na vyombo vyote vitakatifu vilivyokuwa ndani yake. Makuhani na Walawi wakavibeba, 5 naye Mfalme Sulemani na kusanyiko lote la Israeli waliokuwa wamemzunguka wakasimama mbele ya hilo Sanduku, nao wakatoa dhabihu za kondoo na ng’ombe nyingi kiasi kwamba idadi yao haikuweza kuandikwa au kuhesabika.
6 Makuhani wakalileta Sanduku la Agano la Mwenyezi Mungu hadi mahali pake ndani ya mahali patakatifu sana humo Hekaluni, ndipo Patakatifu pa Patakatifu, na kuliweka chini ya mabawa ya makerubi. 7 Makerubi yalitandaza mabawa yao juu ya mahali pa Sanduku la Agano na kutia kivuli Sanduku pamoja na mipiko yake ya kubebea. 8 Mipiko hiyo ilikuwa mirefu sana kiasi kwamba ncha zake zilionekana kutoka Mahali Patakatifu mbele ya Patakatifu pa Patakatifu, lakini sio nje ya Mahali Patakatifu. Hiyo mipiko ipo hata leo. 9 Ndani ya Sanduku hapakuwa na kitu kingine isipokuwa vile vibao viwili vya mawe ambavyo Musa aliviweka ndani yake huko Horebu, mahali Mwenyezi Mungu alipofanya agano na Waisraeli baada ya kutoka Misri.
10 Makuhani walipoondoka katika Mahali Patakatifu, wingu likajaza Hekalu la Mwenyezi Mungu. 11 Nao makuhani hawakuweza kufanya huduma yao kwa sababu ya lile wingu, kwa kuwa utukufu wa Mwenyezi Mungu ulijaza Hekalu lake.
12 Ndipo Sulemani akasema, “Mwenyezi Mungu alisema kwamba ataishi katika giza nene; 13 naam, hakika nimekujengea Hekalu zuri sana, mahali pako pa kuishi milele.”
Hotuba ya Sulemani
(2 Nyakati 6:3-11)
14 Kusanyiko lote la Israeli walipokuwa wamesimama hapo, mfalme akageuka na kuwabariki. 15 Kisha akasema:
“Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, ambaye kwa mkono wake mwenyewe ametimiza alilomwahidi Daudi baba yangu kwa kinywa chake mwenyewe. Kwa kuwa alisema, 16 ‘Tangu siku niliyowatoa watu wangu Israeli kutoka Misri, sikuchagua mji katika kabila lolote la Israeli ili Hekalu lijengwe humo na Jina langu liwe humo, bali nimemchagua Daudi kuwatawala watu wangu Israeli.’
17 “Ilikuwa moyoni mwa Daudi baba yangu kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 18 Lakini Mwenyezi Mungu akamwambia Daudi baba yangu, ‘Kwa sababu ilikuwa moyoni mwako kujenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu, ulifanya vyema kuwa na jambo hili moyoni mwako. 19 Hata hivyo, sio wewe utakayenijengea Hekalu, bali mwanao, ambaye ni mwili wako na damu yako mwenyewe, yeye ndiye atakayejenga Hekalu kwa ajili ya Jina langu.’
20 “Mwenyezi Mungu ametimiza ahadi aliyoiweka: Nimeingia mahali pa Daudi baba yangu, na sasa ninakikalia kiti cha ufalme cha Israeli, kama vile Mwenyezi Mungu alivyoahidi, nami nimejenga Hekalu kwa ajili ya Jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli. 21 Nimetenga nafasi humo kwa ajili ya Sanduku la Agano, ambalo ndani yake kuna lile Agano la Mwenyezi Mungu alilofanya na baba zetu alipowatoa Misri.”
Maombi ya Sulemani ya kuweka Hekalu wakfu
(2 Nyakati 6:12-42)
22 Kisha Sulemani akasimama mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu machoni pa kusanyiko lote la Israeli, akanyoosha mikono yake kuelekea mbinguni, 23 na kusema:
“Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, hakuna Mungu kama wewe juu mbinguni wala chini duniani, wewe unayetunza agano lako la upendo na watumishi wanaodumu katika njia yako kwa moyo wote. 24 Umetimiza ahadi yako kwa mtumishi wako Daudi baba yangu, kwa kinywa chako uliahidi na kwa mkono wako umetimiza, kama ilivyo leo.
25 “Sasa Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, mtimizie mtumishi wako Daudi baba yangu ahadi zako ulizomwahidi uliposema, ‘Kamwe hutakosa kuwa na mtu atakayeketi mbele zangu kwenye kiti cha ufalme cha Israeli, ikiwa wanao watakuwa waangalifu kwa yote wayafanyayo ili kuenenda mbele zangu kama ulivyofanya.’ 26 Sasa, Ee Mungu wa Israeli, ruhusu neno lako ulilomwahidi mtumishi wako Daudi baba yangu litimie.
27 “Je, hakika Mungu atafanya makao duniani? Mbingu, hata mbingu zilizo juu sana, haziwezi kukutosha wewe. Sembuse Hekalu hili nililojenga! 28 Hata hivyo, sikiliza dua la mtumishi wako na maombi yake ya kuhurumiwa, Ee Mwenyezi Mungu, Mungu wangu. Sikia kilio na dua ambalo mtumishi wako anaomba mbele zako siku hii ya leo. 29 Macho yako na yafumbuke kuelekea Hekalu hili usiku na mchana, mahali hapa ambapo ulisema, ‘Jina langu litakuwa humo,’ ili upate kusikia maombi ambayo mtumishi wako ataomba kuelekea mahali hapa. 30 Usikie maombi ya mtumishi wako na ya watu wako Israeli wakati wanapoomba kuelekea mahali hapa. Sikia ukiwa mbinguni, makao yako, na unaposikia, samehe.
31 “Mtu akimkosea jirani yake na akatakiwa kuapa, akija na kuapa mbele ya madhabahu yako ndani ya Hekalu hili, 32 basi, sikia ukiwa mbinguni, ukatende. Hukumu kati ya watumishi wako, ukimhukumu yule mwenye hatia na kuleta juu ya kichwa chake yale aliyoyatenda. Umtangazie mwenye haki kwamba hana hatia, hivyo ukathibitishe kuwa haki kwake.
33 “Watu wako Israeli watakapokuwa wameshindwa na adui kwa sababu ya dhambi walizofanya dhidi yako, nao wakakugeukia na kulikiri jina lako, wakiomba na kufanya dua kwako katika Hekalu hili, 34 basi usikie ukiwa mbinguni, ukasamehe dhambi ya watu wako Israeli na kuwarudisha katika nchi uliyowapa baba zao.
35 “Mbingu zitakapokuwa zimefungwa kusiwe na mvua kwa sababu watu wako wametenda dhambi dhidi yako, watakapoomba kuelekea mahali hapa na kulikiri jina lako nao wakageuka kutoka dhambi zao kwa sababu umewaadhibu, 36 basi usikie ukiwa mbinguni, usamehe dhambi ya watumishi wako, watu wako Israeli. Wafundishe njia sahihi ya kuishi, na ukanyeshe mvua juu ya nchi uliyowapa watu wako kuwa urithi.
37 “Njaa au tauni itakapotokea katika nchi, koga au ukungu, nzige au panzi, au wakati adui atakapowazingira katika mji wao wowote, maafa ya namna yoyote au ugonjwa wowote unaoweza kuwajia, 38 kila dua au ombi litakalotolewa na yeyote kati ya watu wako Israeli, akitambua taabu za moyo wake mwenyewe, naye akainyoosha mikono yake kuelekea Hekalu hili, 39 basi usikie ukiwa mbinguni, makao yako. Usamehe na utende; umpe kila mtu kulingana na matendo yake, kwa kuwa unaujua moyo wake (kwa kuwa ni wewe peke yako ujuaye mioyo ya watu wote), 40 ili wakuogope kwa wakati wote watakaoishi katika nchi uliyowapa baba zetu.
41 “Kuhusu mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako, 42 kwa maana watu watasikia kuhusu Jina lako kuu na kuhusu mkono wako wenye nguvu na mkono wako ulionyooshwa, atakapokuja na kuomba kuelekea Hekalu hili, 43 basi na usikie ukiwa mbinguni, makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli, na pia wapate kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako.
44 “Watu wako watakapoenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa Mwenyezi Mungu kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, 45 basi usikie dua na maombi yao ukiwa mbinguni, ukawape haki yao.
46 “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu asiyetenda dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi yake mwenyewe, mbali au karibu; 47 na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya wale waliowashinda na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa, tumetenda uovu’; 48 wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako; 49 basi usikie dua na maombi yao ukiwa mbinguni, makao yako, ukawape haki yao. 50 Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako; uwasamehe makosa yote waliyoyatenda dhidi yako, na ukawafanye wale waliowashinda kuwaonea huruma; 51 kwa maana ni watu wako na urithi wako, uliowatoa Misri, kutoka lile tanuru la kuyeyushia chuma.
52 “Macho yako na yafumbuke kwa ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako Israeli, nawe uwasikilize wakati wowote wanapokulilia. 53 Kwa maana uliwachagua kati ya mataifa yote ya ulimwengu wawe urithi wako mwenyewe, kama ulivyotangaza kupitia mtumishi wako Musa wakati wewe, Ee Bwana Mungu Mwenyezi, ulipowatoa baba zetu kutoka Misri.”
54 Sulemani alipomaliza dua na maombi haya yote kwa Mwenyezi Mungu, akainuka kutoka mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, mahali alipokuwa amepiga magoti akiwa amenyoosha mikono yake kuelekea mbinguni. 55 Akasimama na kubariki kusanyiko lote la Israeli kwa sauti kubwa, akisema:
56 “Ahimidiwe Mwenyezi Mungu, aliyewapa pumziko watu wake Israeli kama alivyokuwa ameahidi. Hakuna hata neno moja lililopunguka kati ya ahadi zote nzuri alizozitoa kupitia mtumishi wake Musa. 57 Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, na awe pamoja nasi kama alivyokuwa na baba zetu, kamwe asituache wala kutukataa. 58 Yeye na aielekeze mioyo yetu kwake, ili tutembee katika njia zake zote na kushika amri, maagizo, na masharti aliyowapa baba zetu. 59 Nami maneno yangu haya, ambayo nimeyaomba mbele za Mwenyezi Mungu, yawe karibu na Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, usiku na mchana, ili awape haki mtumishi wake na watu wake Israeli, kulingana na mahitaji yao ya kila siku, 60 ili mataifa yote ya dunia wajue kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mungu na kwamba hakuna mwingine. 61 Lazima mwiweke mioyo yenu kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, mwishi kwa maagizo yake na kutii amri zake, kama ilivyo wakati huu.”
Hekalu lawekwa wakfu
(2 Nyakati 7:4-10)
62 Kisha mfalme na Waisraeli wote pamoja naye wakatoa dhabihu mbele za Mwenyezi Mungu. 63 Sulemani akatoa dhabihu sadaka za amani kwa Mwenyezi Mungu: ng’ombe elfu ishirini na mbili, pamoja na kondoo na mbuzi elfu mia moja na ishirini. Ndivyo mfalme na Waisraeli wote walivyoweka wakfu Hekalu la Mwenyezi Mungu.
64 Siku hiyo hiyo mfalme akaweka wakfu sehemu ya katikati ya ua uliokuwa mbele ya Hekalu la Mwenyezi Mungu, na hapo akatoa sadaka za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani, kwa sababu madhabahu ya shaba iliyokuwa mbele za Mwenyezi Mungu ilikuwa ndogo sana kuweza kubeba sadaka hizo za kuteketezwa, sadaka za nafaka, na mafuta ya wanyama wa sadaka za amani.
65 Hivyo Sulemani akaiadhimisha sikukuu kwa wakati ule, na Waisraeli wote pamoja naye: walikuwa kusanyiko kubwa sana, watu kutoka Lebo-Hamathi hadi Kijito cha Misri. Wakaiadhimisha mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, kwa siku saba na siku saba zaidi, yaani jumla siku kumi na nne. 66 Siku iliyofuata, aliwaruhusu watu waondoke. Wakambariki mfalme, kisha wakaenda nyumbani wakiwa na mashangilio na furaha moyoni kwa ajili ya mambo yote mema ambayo Mwenyezi Mungu alimtendea kwa ajili ya Daudi mtumishi wake na watu wake Israeli.