3
Mwenyezi Mungu amwita Samweli
Kijana Samweli alihudumu mbele za Mwenyezi Mungu chini ya Eli. Katika siku zile neno la Mungu lilikuwa adimu, hapakuwa na maono mengi.
Usiku mmoja Eli, ambaye macho yake yalikuwa yamefifia sana kiasi kwamba aliona kwa shida sana, alikuwa amelala mahali pake pa kawaida. Taa ya Mungu bado ilikuwa haijazimika, na Samweli alikuwa amelala hekaluni*Hekaluni maana yake ndani ya Maskani ya Mwenyezi Mungu. mwa Mwenyezi Mungu, ambapo Sanduku la Mungu lilikuwa. Kisha Mwenyezi Mungu akamwita Samweli.
Samweli akajibu, “Mimi hapa.” Naye akakimbia kwa Eli na kumwambia, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”
Lakini Eli akasema, “Sikukuita; rudi ukalale.” Hivyo akaenda kulala.
Mwenyezi Mungu akaita tena, “Samweli!” Naye Samweli akaamka, kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”
Eli akasema, “Mwanangu, sikukuita, rudi ukalale.”
Wakati huu Samweli alikuwa bado hajamjua Mwenyezi Mungu. Neno la Mwenyezi Mungu lilikuwa bado halijafunuliwa kwake.
Mwenyezi Mungu akamwita Samweli mara ya tatu, naye Samweli akaamka kwenda kwa Eli na kusema, “Mimi hapa, kwa kuwa umeniita.”
Ndipo Eli akatambua kuwa Mwenyezi Mungu alikuwa akimwita kijana. Hivyo Eli akamwambia Samweli, “Nenda ukalale; akikuita, sema, ‘Nena Mwenyezi Mungu, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.’ ” Hivyo Samweli akaenda na kulala mahali pake.
10 Mwenyezi Mungu akaja, akasimama pale, akiita kama hapo awali, “Samweli! Samweli!”
Kisha Samweli akasema, “Nena Mwenyezi Mungu, kwa kuwa mtumishi wako anasikiliza.”
11 Naye Mwenyezi Mungu akamwambia Samweli: “Tazama, nipo karibu kufanya kitu katika Israeli ambacho kitafanya masikio ya kila mmoja atakayesikia yawashe. 12 Wakati huo nitatimiza dhidi ya Eli kila kitu nilichonena dhidi ya jamaa yake, kuanzia mwanzo hadi mwisho. 13 Kwa kuwa nilimwambia kwamba ningehukumu jamaa yake milele kwa sababu ya dhambi aliyoijua, wanawe kumkufuru Mungu, naye akashindwa kuwazuia. 14 Kwa hiyo, nikaapa kuhusu nyumba ya Eli, ‘Hatia ya nyumba ya Eli kamwe haitaweza kufidiwa kwa dhabihu au sadaka.’ ”
15 Samweli akalala hadi asubuhi, kisha akafungua milango ya nyumba ya Mwenyezi Mungu. Aliogopa kumwambia Eli yale maono, 16 lakini Eli akamwita na kumwambia, “Samweli mwanangu.”
Samweli akamjibu, “Mimi hapa.”
17 Eli akamuuliza, “Ni nini alichokuambia? Usinifiche. Mwenyezi Mungu na akuadhibu vikali zaidi kama utanificha chochote alichokuambia.” 18 Kwa hiyo Samweli akamwambia kila kitu bila kumficha chochote. Ndipo Eli akasema, “Yeye ni Mwenyezi Mungu; na afanye lile lililo jema machoni pake!”
19 Mwenyezi Mungu alikuwa pamoja na Samweli alipokuwa akikua, na hakuacha neno lolote la Samweli lianguke chini. 20 Nao Israeli wote kuanzia Dani hadi Beer-Sheba wakatambua kuwa Samweli amethibitishwa kuwa nabii wa Mwenyezi Mungu. 21 Mwenyezi Mungu akaendelea kutokea huko Shilo, na huko alijidhihirisha kwa Samweli kupitia neno lake.

*3:3 Hekaluni maana yake ndani ya Maskani ya Mwenyezi Mungu.