5
Sanduku la Agano huko Ashdodi na Ekroni
1 Baada ya Wafilisti kuteka Sanduku la Mungu, walilichukua kutoka Ebenezeri hadi Ashdodi. 2 Kisha wakaliingiza lile Sanduku ndani ya hekalu la Dagoni na kuliweka kando ya huyo Dagoni. 3 Watu wa Ashdodi walipoamka asubuhi na mapema kesho yake, kumbe, wakamkuta Dagoni ameanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu! Wakamwinua Dagoni na kumrudisha mahali pake. 4 Lakini asubuhi iliyofuata, walipoamka kumbe, walimkuta Dagoni ameanguka kifudifudi mbele ya Sanduku la Mwenyezi Mungu! Kichwa chake na mikono vilikuwa vimevunjwa, navyo vimelala kizingitini; ni kiwiliwili chake tu kilichokuwa kimebaki. 5 Ndiyo sababu hadi leo makuhani wa Dagoni na wengine wanaoingia katika hekalu la Dagoni huko Ashdodi hawakanyagi kizingiti.
6 Mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa mzito juu ya watu wa Ashdodi na vijiji jirani, akaleta uharibifu juu yao na kuwatesa kwa majipu. 7 Watu wa Ashdodi walipoona kile kilichokuwa kikitokea, wakasema, “Sanduku la Mungu wa Israeli kamwe lisikae hapa pamoja na sisi, kwa sababu mkono wake ni mzito juu yetu na juu ya Dagoni mungu wetu.” 8 Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kuwauliza, “Tutafanya nini na hili Sanduku la Mungu wa Israeli?”
Wakajibu, “Sanduku la Mungu wa Israeli na liende Gathi.” Basi wakalihamisha Sanduku la Mungu wa Israeli.
9 Lakini baada ya kulihamisha, mkono wa Mwenyezi Mungu ulikuwa dhidi ya huo mji wa Gathi, akiuweka katika fadhaa kuu. Mungu akawatesa watu wa huo mji, vijana kwa wazee, kwa kuwaletea majipu. 10 Basi wakapeleka Sanduku la Mungu Ekroni.
Sanduku la Mungu lilipokuwa linaingia Ekroni, watu wa Ekroni walilia wakisema, “Wamelileta Sanduku la Mungu wa Israeli kwetu ili kutuua sisi na watu wetu.” 11 Basi wakawaita watawala wote wa Wafilisti pamoja na kusema, “Liondoeni Sanduku la Mungu wa Israeli na lirudishwe mahali pake, la sivyo litatuua sisi na watu wetu.” Kwa kuwa kifo kilikuwa kimeujaza mji hofu; kwani mkono wa Mungu ulikuwa mzito sana juu yake. 12 Wale ambao hawakufa walipatwa na majipu, na kilio cha mji kilifika hadi mbinguni.