1 Timotheo
1
Salamu
Paulo, mtume wa Al-Masihi Isa, kwa amri ya Mungu Mwokozi wetu, na ya Al-Masihi Isa aliye tumaini letu.
Kwa Timotheo, mwanangu halisi katika imani.
Neema, rehema na amani zinazotoka kwa Mungu Baba*Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. Mwenyezi na kwa Al-Masihi Isa, Bwana wetu.
Maonyo dhidi ya walimu wa uongo
Kama nilivyokusihi wakati nilipoenda Makedonia, endelea kubaki Efeso, ili upate kuwaagiza watu wasiendelee kufundisha mafundisho ya uongo wala wasitoe muda wao kwa hadithi za kubuniwa na orodha za majina ya vizazi visivyo na mwisho, ambazo huchochea mabishano badala ya mpango wa Mungu utokanao na imani. Kusudi la maagizo haya ni upendo unaotoka katika moyo safi, dhamiri safi na imani ya kweli. Watu wengine wamepotoka kutoka haya na kugeukia majadiliano yasiyo na maana kwa kuwa, wanataka kuwa walimu wa Torati, lakini hawajui mambo yale wanayosema wala hayo wanayoyatumainia kwa uthabiti.
Tunajua kwamba sheria ni njema ikiwa inatumika kwa halali kama ilivyokusudiwa. Lakini tunajua ya kuwa sheria si kwa ajili ya wenye haki, bali kwa ajili ya wavunja sheria na waasi, kwa ajili ya wasiomcha Mungu na wenye dhambi, wasio watakatifu na wanaokufuru; kwa wale wawauao baba zao au mama zao, kwa wauaji, 10 kwa wazinzi na wahanithi, kwa wale wauzao watu, na kwa waongo na waapao kwa uongo, na kwa chochote kingine kilicho kinyume na mafundisho ya kweli, 11 ambayo yanakubaliana na Injili ya utukufu wa Mungu anayehimidiwa, ambayo mimi nimewekewa amana.
Neema ya Mwenyezi Mungu kwa Paulo
12 Namshukuru Al-Masihi Isa Bwana wetu, aliyenitia nguvu, kwa sababu aliniona mwaminifu, akaniteua kwa kazi yake. 13 Ingawa wakati fulani nilikuwa mwenye kukufuru, mtesaji na mwenye jeuri, lakini nilipata rehema kwa sababu nilitenda hivyo kwa kutojua na kutoamini kwangu. 14 Neema ya Bwana wetu ilimiminwa juu yangu kwa wingi, ikiambatana na imani na upendo ulio katika Al-Masihi Isa.
15 Msemo huu ni wa kweli na unaostahili kukubalika, usemao kwamba: Al-Masihi Isa alikuja ulimwenguni kuokoa wenye dhambi, ambao mimi ndiye niliye mbaya kuliko wote. 16 Lakini kwa sababu hiyo nilipata rehema, ili katika mimi, niliyekuwa mwenye dhambi kuliko wote, Al-Masihi Isa apate kuonesha uvumilivu wake usio na kikomo, ili niwe kielelezo kwa wale watakaomwamini na wapate uzima wa milele. 17 Basi Mfalme wa milele, asiye na mwisho, asiyeonekana, aliye Mungu pekee, apewe heshima na utukufu milele na milele. Amen.
Timotheo anaagizwa upya
18 Mwanangu Timotheo, ninakupa agizo hili, kwa kadiri ya maneno ya unabii yaliyosemwa kukuhusu, ili kwa kuyafuata upate kupigana vita vizuri, 19 ukiishikilia imani na dhamiri safi, ambazo wengine wamevikataa, na hivyo wakaangamia kwa habari ya imani yao. 20 Miongoni mwao wako Himenayo na Iskanda, ambao nimemkabidhi Shetani ili wafundishwe wasije wakakufuru.

*1:2 Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.