5
Makao yetu ya mbinguni
Kwa maana twajua kama hema letu la dunia tunayoishi likiharibiwa, tunalo jengo kutoka kwa Mungu, nyumba iliyo ya milele kule mbinguni, isiyojengwa kwa mikono ya wanadamu. Katika hema hili twalia kwa uchungu, tukitamani kuvikwa makao yetu ya mbinguni, kwa kuwa tukishavikwa hatutaonekana tena kuwa uchi. Kwa kuwa tukiwa bado katika hema hili twalia kwa uchungu na kulemewa, kwa sababu hatutaki kuvuliwa bali kuvikwa makao yetu ya mbinguni ili kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima. Basi Mungu ndiye alitufanya kwa ajili ya jambo lilo hilo, naye ametupatia Roho wa Mungu kuwa amana, akituhakikishia ahadi ya kile kijacho.
Kwa hiyo siku zote tuna ujasiri, hata ingawa tunajua kwamba tukiwa katika mwili huu, tuko mbali na Bwana Isa. Kwa maana twaenenda kwa imani wala si kwa kuona. Naam, tuna ujasiri, na tunaona ingekuwa bora zaidi kuuacha mwili huu na kwenda kukaa na Bwana Isa. Kwa hiyo, tukiwa katika mwili huu au tukiwa mbali nao, lengo letu ni kumpendeza Bwana Isa. 10 Kwa kuwa sisi sote tutasimama mbele ya kiti cha hukumu cha Al-Masihi, ili kila mmoja apate kulipwa kwa ajili ya yale ambayo yametendwa katika mwili wake, yakiwa mema au mabaya.
Huduma ya upatanisho
11 Basi, kwa kuwa tunajua kumcha Mwenyezi Mungu, tunajitahidi kuwavuta wengine. Lakini Mungu anatufahamu dhahiri, nami natumaini kwamba tu dhahiri katika dhamiri zenu pia. 12 Sio kwamba tunajaribu kujistahilisha kwenu tena, lakini tunataka kuwapa nafasi ili mwone fahari juu yetu, mweze kuwajibu hao wanaoona fahari kuhusu mambo yanayoonekana badala ya mambo yaliyo moyoni. 13 Kama tumerukwa na akili, ni kwa ajili ya Mungu; kama tuna akili timamu, ni kwa ajili yenu. 14 Kwa kuwa upendo wa Al-Masihi unatutia nguvu, kwa sababu tunasadiki kuwa mmoja alikufa kwa ajili ya wote, kwa hiyo wote walikufa. 15 Naye alikufa kwa ajili ya watu wote, ili wote wanaoishi wasiishi tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa na kufufuliwa tena kwa ajili yao.
16 Hivyo tangu sasa hatumwangalii mtu yeyote kwa mtazamo wa kibinadamu. Ingawa wakati fulani tulimwangalia Al-Masihi kwa namna ya kibinadamu, hatumwangalii tena hivyo. 17 Kwa hiyo mtu akiwa ndani ya Al-Masihi, amekuwa kiumbe kipya: ya kale yamepita; tazama, yamekuwa mapya. 18 Haya yote yanatokana na Mungu, ambaye ametupatanisha sisi na nafsi yake kupitia kwa Isa Al-Masihi, na kutupatia sisi huduma ya upatanisho: 19 kwamba Mungu alikuwa ndani ya Al-Masihi akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake mwenyewe, akiwa hawahesabii watu dhambi zao. Naye ametukabidhi sisi ujumbe huu wa upatanisho. 20 Kwa hiyo sisi ni mabalozi wa Al-Masihi, kana kwamba Mungu anawasihi kupitia kwa vinywa vyetu. Nasi twawaomba sana ninyi kwa niaba ya Al-Masihi: mpatanishwe na Mungu. 21 Kwa maana Mungu alimfanya yeye asiyekuwa na dhambi kuwa dhambi*au kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kufanywa haki ya Mungu kupitia kwake Al-Masihi.

*5:21 au kuwa sadaka ya dhambi