9
Yehu atiwa mafuta kuwa Mfalme
Nabii Al-Yasa akamwita mtu mmoja kutoka kwa wana wa manabii na kumwambia, “Jikaze viuno, uichukue hii chupa ya mafuta, na uende Ramoth-Gileadi. Ukifika huko, mtafute Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi. Nenda kwake, umtenge na wenzake, na umpeleke katika chumba cha ndani. Kisha chukua hii chupa na umimine mafuta juu ya kichwa chake, nawe utangaze, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Ninakupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ Kisha ufungue mlango na ukimbie; usikawie!”
Basi yule kijana nabii akaenda Ramoth-Gileadi. Alipofika, akawakuta maafisa wa jeshi wameketi pamoja, akasema, “Nina ujumbe wako, ee jemadari.”
Yehu akauliza, “Kwa yupi miongoni mwetu?”
Akamjibu, “Kwako wewe, jemadari.”
Yehu akainuka na kuingia ndani ya nyumba. Ndipo yule nabii akamimina mafuta juu ya kichwa cha Yehu, na kutangaza, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Ninakupaka mafuta uwe mfalme juu ya watu wa Mwenyezi Mungu, yaani Israeli. Inakupasa uiangamize nyumba ya bwana wako Ahabu, nami nitalipiza kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii na damu ya watumishi wote wa Mwenyezi Mungu iliyomwagwa na Yezebeli. Nyumba yote ya Ahabu itaangamia. Nitamkatilia mbali kila mzaliwa wa kiume wa Ahabu katika Israeli, aliye mtumwa ama aliye huru. Nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama ile nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ile nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya. 10 Kuhusu Yezebeli, mbwa watamla kwenye kiwanja huko Yezreeli, wala hakuna mtu atakayemzika.’ ” Kisha akafungua mlango na kukimbia.
11 Yehu alipotoka nje na kurudi kwenda kwa maafisa wenzake, mmoja wao akamuuliza, “Je, kila kitu ni salama? Kwa nini huyu mwenye wazimu alikuja kwako?”
Yehu akajibu, “Wewe unamfahamu huyo mtu, na aina ya mambo ambayo yeye husema.”
12 Wakasema, “Hiyo siyo kweli! Tuambie.”
Yehu akasema, “Haya ndio aliyoniambia: ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Ninakupaka mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ ”
13 Wakaharakisha kuvua mavazi yao, na kuyatandaza chini ya Yehu ili akanyage juu kwenye ngazi ya nje. Kisha wakapiga tarumbeta na kupaza sauti wakisema, “Yehu ni mfalme!”
Yehu awaua Yoramu na Ahazia
14 Basi Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akapanga njama dhidi ya Yoramu. (Wakati huu, Yoramu na Waisraeli wote walikuwa wakiilinda Ramoth-Gileadi dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu, 15 lakini Mfalme Yoramu alikuwa amerudishwa Yezreeli ili kujiuguza kutokana na majeraha ambayo Waaramu walimtia katika vita na Hazaeli mfalme wa Aramu.) Yehu akasema, “Kama hii ndiyo nia yenu, msimruhusu hata mmoja kutoroka nje ya mji kwenda kupeleka habari huko Yezreeli.” 16 Ndipo Yehu akaingia katika gari lake la vita na kuendesha kwenda Yezreeli, kwa sababu Yoramu alikuwa amepumzika huko, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameenda kumwona.
17 Mlinzi aliyesimama juu ya kinara cha Yezreeli alipoona askari wa Yehu wanakuja, akaita akisema, “Naona askari wanakuja.”
Yoramu akaamuru, “Mtwae mpanda farasi umtume akakutane nao na kuuliza, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”
18 Mpanda farasi akaondoka kwenda kukutana na Yehu na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme: ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”
Yehu akamjibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”
Mlinzi akatoa habari, “Mjumbe amewafikia lakini harudi.”
19 Basi mfalme akamtuma mpanda farasi wa pili. Alipowafikia akasema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”
Yehu akajibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”
20 Yule mlinzi akatoa taarifa akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini hata yeye harudi. Uendeshaji ule ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi, anaendesha kama mwenye wazimu!”
21 Yoramu akaagiza, akasema, “Weka tayari gari langu la vita.” Na baada ya gari kuwa tayari, Yoramu mfalme wa Israeli, na Ahazia mfalme wa Yuda, wakaondoka kila mmoja kwenye gari lake ili kukutana na Yehu. Walikutana naye katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. 22 Yoramu alipomwona Yehu, akauliza, “Je, Yehu, umekuja kwa amani?”
Yehu akajibu, “Kunawezaje kuwa na amani wakati ibada za sanamu na uchawi wa mama yako Yezebeli bado ziko?”
23 Yoramu akageuka nyuma na kukimbia, akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini, Ahazia!”
24 Kisha Yehu akatwaa upinde wake na kumchoma Yoramu katikati ya mabega. Mshale ukapenya kwenye moyo wake, naye akaanguka ghafula ndani ya gari lake la vita. 25 Yehu akamwambia Bidkari, mwendeshaji wa gari lake la vita, “Mwinue na umtupe katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. Kumbuka jinsi mimi na wewe tulivyokuwa tukiendesha pamoja magari yetu ya vita nyuma ya Ahabu baba yake, wakati Mwenyezi Mungu alitoa unabii huu kumhusu: 26 ‘Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya wanawe, nami kwa hakika nitakufanya uilipe juu ya shamba hili, asema Mwenyezi Mungu.’ Sasa basi, mwinue na umtupe juu ya kiwanja, kulingana na neno la Mwenyezi Mungu.”
27 Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipaza sauti na kusema, “Muue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake la vita kwenye njia inayoelekea Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido, akafia huko. 28 Watumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi. 29 (Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala katika Yuda.)
Yezebeli auawa
30 Kisha Yehu akaenda Yezreeli. Yezebeli aliposikia habari hii, akayapaka macho yake wanja, akatengeneza nywele zake na kutazama nje dirishani. 31 Yehu alipokuwa akiingia langoni, Yezebeli akasema, “Je, umekuja kwa amani, Zimri, wewe muuaji wa bwana wako?”
32 Yehu akaangalia juu dirishani na kuita, “Je, ni nani aliye upande wangu? Ni nani?” Matowashi wawili au watatu wakamtazama. 33 Yehu akasema, “Mtupeni huyo mwanamke chini!” Kwa hiyo wakamtupa chini, nayo sehemu ya damu yake ikatapanyika ukutani, na nyingine juu ya farasi walipokuwa wakimkanyaga kwa miguu yao.
34 Yehu akaingia ndani, akala na akanywa. Akasema, “Mshughulikieni huyo mwanamke aliyelaaniwa. Mzikeni, kwa sababu alikuwa binti ya mfalme.” 35 Lakini walipotoka kwenda kumzika, hawakukuta kitu chochote isipokuwa fuvu la kichwa, miguu yake na mikono. 36 Wakarudi na kumwambia Yehu, ambaye alisema, “Hili ndilo neno la Mwenyezi Mungu alilosema kwa kinywa cha mtumishi wake Ilya Mtishbi, kwamba: Katika kiwanja cha Yezreeli, mbwa wataila nyama ya Yezebeli. 37 Maiti ya Yezebeli itakuwa kama kinyesi juu ya ardhi katika uwanja wa Yezreeli, kwamba hakutakuwa mtu atakayeweza kusema, ‘Huyu ni Yezebeli.’ ”