11
Athalia na Yoashi
(2 Nyakati 22:10–23:21)
1 Athalia mamaye Ahazia alipoona kuwa mwanawe amekufa, akainuka na kuangamiza jamaa yote ya mfalme. 2 Lakini Yehosheba, binti ya Mfalme Yehoramu, aliyekuwa pia dada yake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia kwa siri kutoka miongoni mwa wana wa mfalme waliokuwa karibu kuuawa. Akamweka Yoashi pamoja na yaya wake ndani ya chumba cha kulala na kumficha humo ili Athalia asimwone; kwa hiyo hakuuawa. 3 Alibaki amefichwa pamoja na yaya wake katika Hekalu la Mwenyezi Mungu kwa muda wa miaka sita wakati Athalia alikuwa akitawala nchi.
4 Katika mwaka wa saba, Yehoyada akatumania wakuu wa vikundi vya mamia, na Wakari*yaani Wakerethi (taz. 1 Samweli 30:14; Ezekieli 25:16; Sefania 2:5, 6). na walinzi, nao wakaletwa kwake katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Alifanya agano nao na kuwaapisha katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Ndipo akawaonesha mwana wa mfalme. 5 Akawaamuru akisema, “Hivi ndivyo iwapasavyo kufanya: Ninyi ambao mko makundi matatu mnaoingia zamu siku ya Sabato, theluthi moja italinda jumba la kifalme, 6 theluthi nyingine Lango la Suri, na theluthi nyingine lango lililo nyuma ya walinzi, ambao hupeana zamu kulinda Hekalu. 7 Nanyi ambao mko katika makundi mengine mawili ambao kwa kawaida hupumzika siku ya Sabato, wote mtalinda Hekalu kwa ajili ya mfalme. 8 Jipangeni kumzunguka mfalme, kila mtu akiwa na silaha yake mkononi. Yeyote anayesogelea safu zenu lazima auawe. Kaeni karibu na mfalme popote aendapo.”
9 Wakuu wa vikosi vya mamia wakafanya vile kuhani Yehoyada aliagiza. Kila mmoja akawachukua watu wake, wale waliokuwa wakiingia zamu siku ya Sabato na wale waliokuwa wakienda mapumziko, nao wakaja kwa kuhani Yehoyada. 10 Ndipo akawapa wale wakuu mikuki na ngao zilizokuwa za Mfalme Daudi, zilizokuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu. 11 Wale walinzi, kila mmoja akiwa na silaha yake mkononi mwake, wakajipanga kumzunguka mfalme, karibu na madhabahu na Hekalu, kuanzia upande wa kusini hadi upande wa kaskazini mwa Hekalu.
12 Yehoyada akamtoa mwana wa mfalme na kumvika taji, akampa nakala ya agano, na kumtangaza kuwa mfalme. Wakampaka mafuta, nao watu wakapiga makofi na kupaza sauti, wakisema, “Mfalme aishi maisha marefu!”
13 Athalia aliposikia kelele za walinzi pamoja na watu, akawaendea watu katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. 14 Akaangalia, na tazama, mfalme alikuwa amesimama karibu na nguzo, kama ilivyokuwa desturi. Maafisa na wapiga tarumbeta walikuwa kando ya mfalme, nao watu wote wa nchi walikuwa wanashangilia na kupiga tarumbeta. Ndipo Athalia akararua mavazi yake na kulia, “Uhaini! Uhaini!”
15 Kuhani Yehoyada akawaamuru majemadari wa vikosi vya mamia, waliokuwa viongozi wa jeshi, “Mtoeni nje kati ya safu, na mkamuue kwa upanga yeyote anayemfuata.” Kwa kuwa kuhani alikuwa amesema, “Hatauawa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.” 16 Basi wakamkamata Athalia alipofika mahali farasi huingilia katika viwanja vya jumba la mfalme, wakamuua hapo.
17 Kisha Yehoyada akafanya agano kati ya Mwenyezi Mungu na mfalme na watu kwamba watakuwa watu wa Mwenyezi Mungu. Akafanya pia agano kati ya mfalme na watu. 18 Watu wote wa nchi wakaenda kwenye hekalu la Baali na kulibomoa. Wakavunjavunja madhabahu na sanamu, na kumuua Matani kuhani wa Baali mbele ya hayo madhabahu.
Kisha Yehoyada kuhani akawaweka walinzi kwenye Hekalu la Mwenyezi Mungu. 19 Pamoja naye akawachukua majemadari wa mamia, Wakari, walinzi na watu wote wa nchi, nao kwa pamoja wakamteremsha mfalme kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu na kwenda kwenye jumba la mfalme, wakiingilia njia ya lango la walinzi. Ndipo mfalme akachukua nafasi yake kwenye kiti cha ufalme; 20 nao watu wote wa nchi wakafurahi. Mji ukatulia, kwa sababu Athalia alikuwa ameuawa kwa upanga nyumbani mwa mfalme.
21 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.