20
Ugonjwa wa Hezekia
(2 Nyakati 32:24-26; Isaya 38:1-8, 21-22)
Katika siku hizo, Hezekia akaugua, naye akawa karibu kufa. Nabii Isaya mwana wa Amozi akaenda kwake na kumwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu: Tengeneza mambo ya nyumba yako, kwa sababu utakufa, hutapona.”
Hezekia akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Mwenyezi Mungu: “Ee Mwenyezi Mungu, kumbuka jinsi nilivyoenenda mbele zako kwa uaminifu na kujitoa kwa moyo wangu wote, na kufanya yaliyo mema machoni pako.” Naye Hezekia akalia kwa uchungu.
Kabla Isaya hajaondoka katika ua wa kati, neno la Mwenyezi Mungu likamjia, akaambiwa: “Rudi ukamwambie Hezekia, kiongozi wa watu wangu, ‘Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba yako Daudi: Nimeyasikia maombi yako na nimeona machozi yako; nitakuponya. Siku ya tatu kuanzia sasa utapanda kwenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Nitakuongezea miaka kumi na tano katika maisha yako. Nami nitakuokoa wewe pamoja na mji huu kutoka mkononi mwa mfalme wa Ashuru. Nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya mtumishi wangu Daudi!’ ”
Kisha Isaya akasema, “Tengenezeni dawa ya kubandika ya tini.” Wakafanya hivyo na kuiweka kwenye jipu, naye akapona.
Hezekia alimuuliza Isaya, “Kutakuwa na ishara gani kwamba Mwenyezi Mungu ataniponya mimi, na kwamba nitapanda kwenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu siku ya tatu tangu leo?”
Isaya akajibu, “Hii ndiyo ishara ya Mwenyezi Mungu kwako kwamba Mwenyezi Mungu atafanya kile alichoahidi: Je, kivuli kiende hatua kumi mbele, au kivuli kirudi nyuma hatua kumi?”
10 Hezekia akasema, “Ni jambo rahisi kwa kivuli kutangulia mbele hatua kumi, kuliko kukifanya kirudi nyuma hatua kumi.”
11 Ndipo nabii Isaya akamwita Mwenyezi Mungu, naye Mwenyezi Mungu akakifanya kivuli kurudi nyuma hatua kumi ambazo kilikuwa kimeshuka kwenye ngazi ya Ahazi.
Wajumbe kutoka Babeli
(Isaya 39:1-8)
12 Wakati huo Merodaki-Baladani, mwana wa Baladani mfalme wa Babeli, akamtumia Hezekia barua na zawadi, kwa sababu alikuwa amesikia habari za kuugua kwa Hezekia. 13 Hezekia akawapokea wale wajumbe na kuwaonesha vitu vyote vilivyokuwa katika ghala zake: yaani fedha, dhahabu, vikolezo na mafuta safi, ghala la silaha na kila kitu kilichokuwa katika hazina yake. Hapakuwa na kitu katika jumba lake la kifalme au katika ufalme wake wote ambacho Hezekia hakuwaonesha.
14 Ndipo nabii Isaya akaenda kwa Mfalme Hezekia na kumuuliza, “Watu hao walisema nini, na wametoka wapi?”
Hezekia akamjibu, “Wametoka nchi ya mbali. Walikuja kutoka Babeli.”
15 Nabii akauliza, “Waliona nini katika jumba lako la kifalme?”
Hezekia akajibu, “Waliona kila kitu katika jumba langu. Hakuna kitu katika hazina yangu ambacho sikuwaonesha.”
16 Ndipo Isaya akamwambia Hezekia, “Sikia neno la Mwenyezi Mungu: 17 Hakika wakati unakuja ambapo vitu vyote katika jumba lako, na vyote ambavyo baba zako waliweka akiba hadi siku hii, vitachukuliwa kwenda Babeli. Hakuna chochote kitakachosalia, asema Mwenyezi Mungu. 18 Nao baadhi ya wazao wako, mwili wako na damu yako mwenyewe watakaozaliwa kwako, watachukuliwa mateka, nao watakuwa matowashi katika jumba la mfalme wa Babeli.”
19 Hezekia akamjibu Isaya, “Neno la Mwenyezi Mungu ulilosema ni jema.” Kwa kuwa alifikiri, “Si patakuwa na amani na usalama wakati wa uhai wangu?”
20 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Hezekia, mafanikio yake yote, na jinsi alivyotengeneza bwawa na mfereji ulioleta maji katika mji, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 21 Hezekia akalala na baba zake. Naye Manase mwanawe akawa mfalme baada yake.