22
Yosia mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 34; 35:20-27)
1 Yosia alikuwa na umri wa miaka nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka thelathini na moja. Mama yake aliitwa Yedida binti Adaya, kutoka Boskathi. 2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Mwenyezi Mungu na kuenenda katika njia zote za Daudi baba yake. Hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.
3 Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, Mfalme Yosia akamtuma mwandishi Shafani mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, kwenda katika Hekalu la Mwenyezi Mungu. Akasema: 4 “Panda uende kwa Hilkia, kuhani mkuu, umwambie ahesabu zile fedha ambazo zimeletwa katika Hekalu la Mwenyezi Mungu, ambazo mabawabu wamekusanya kutoka kwa watu. 5 Waambie waikabidhi kwa watu walioteuliwa kusimamia kazi ya Hekalu. Waamuru watu hawa wawalipe wafanyakazi ambao wanakarabati Hekalu la Mwenyezi Mungu: 6 wale maseremala, wajenzi na waashi. Waambie pia wanunue mbao na mawe yaliyochongwa ili kukarabati Hekalu. 7 Lakini hawahitajiki kutoa maelezo ya fedha walizokabidhiwa, kwa sababu wanafanya kazi kwa uaminifu.”
8 Hilkia kuhani mkuu akamwambia Shafani mwandishi, “Nimekipata Kitabu cha Torati ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu.” Akampa Shafani, ambaye alikisoma. 9 Kisha Shafani mwandishi akamwendea mfalme na kumpa taarifa akisema: “Maafisa wako wametoa ile fedha ambayo ilikuwa ndani ya Hekalu la Mwenyezi Mungu na imekabidhiwa mikononi mwa wasimamizi wa marekebisho ya Hekalu.” 10 Ndipo Shafani mwandishi akampasha mfalme habari, akisema: “Hilkia kuhani amenipa kitabu hiki.” Naye Shafani akakisoma kile kitabu mbele ya mfalme.
11 Mfalme aliposikia maneno ya kile Kitabu cha Torati, akararua mavazi yake. 12 Akatoa maagizo haya kwa Hilkia kuhani, Ahikamu mwana wa Shafani, Akbori mwana wa Mikaya, Shafani mwandishi, na Asaya mtumishi wa mfalme: 13 “Nendeni mkamuulize Mwenyezi Mungu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu na Yuda wote kuhusu yale yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki ambacho kimepatikana. Hasira ya Mwenyezi Mungu ni kubwa inayowaka dhidi yetu kwa sababu baba zetu hawakuyatii maneno ya kitabu hiki. Hawajatenda kulingana na yale yote yaliyoandikwa humo kutuhusu.”
14 Hilkia kuhani, Ahikamu, Akbori, Shafani na Asaya wakaenda kuongea na nabii mke Hulda, aliyekuwa mke wa Shalumu mwana wa Tikwa, mwana wa Harhasi mtunzaji wa chumba cha mavazi. Hulda aliishi Yerusalemu katika Mtaa wa Pili.
15 Akawaambia, “Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: Mwambieni yule mtu aliyewatuma ninyi kwangu, 16 ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu: Nitaleta maafa juu ya mahali hapa na watu wake, kulingana na kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hicho mfalme wa Yuda alichosoma. 17 Kwa sababu wameniacha mimi na kufukiza uvumba kwa miungu mingine, na kunighadhibisha kwa sanamu zote zilizotengenezwa kwa mikono yao, hasira yangu itawaka dhidi ya mahali hapa, wala haitatulizwa.’ 18 Mwambieni mfalme wa Yuda, ambaye amewatuma kumuuliza Mwenyezi Mungu, ‘Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli, kuhusu maneno uliyoyasikia: 19 Kwa kuwa moyo wako ulikuwa msikivu na ulijinyenyekeza mbele za Mwenyezi Mungu uliposikia kile nilichosema dhidi ya mahali hapa na watu wake, kwamba wangelaaniwa na kuachwa ukiwa, basi kwa sababu uliyararua mavazi yako na kulia mbele zangu, nimekusikia, asema Mwenyezi Mungu. 20 Kwa hiyo nitakukusanya kwa baba zako, nawe utazikwa kwa amani. Macho yako hayataona maafa yote nitakayoleta juu ya mahali hapa.’ ”
Basi wakapeleka jibu lake kwa mfalme.