24
1 Wakati wa utawala wa Yehoyakimu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliishambulia nchi, naye Yehoyakimu akawa mtumwa wake kwa miaka mitatu. Lakini hatimaye akabadili mawazo yake na kuasi dhidi ya Nebukadneza. 2 Mwenyezi Mungu akatuma wavamiaji wa Wakaldayo, Waaramu, Wamoabu na Waamoni ili kumshambulia. Aliwatuma kuiangamiza Yuda sawasawa na neno la Mwenyezi Mungu lililosemwa na watumishi wake manabii. 3 Hakika mambo haya yalitokea Yuda kulingana na agizo la Mwenyezi Mungu, ili kuwaondoa kutoka machoni pake kwa sababu ya dhambi za Manase na yote aliyoyafanya, 4 ikiwa ni pamoja na kumwaga damu isiyo na hatia. Kwa kuwa aliijaza Yerusalemu kwa damu isiyo na hatia, naye Mwenyezi Mungu hakuwa radhi kusamehe.
5 Kuhusu matukio mengine ya utawala wa Yehoyakimu na yote aliyoyafanya, je, hayakuandikwa katika kitabu cha kumbukumbu za wafalme wa Yuda? 6 Yehoyakimu akalala na baba zake. Naye Yehoyakini mwanawe akawa mfalme baada yake.
7 Mfalme wa Misri hakutoka tena katika nchi yake, kwa sababu mfalme wa Babeli alikuwa ameitwaa himaya yake yote, kuanzia Kijito cha Misri hadi Mto Frati.
Yehoyakini mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 36:9-10)
8 Yehoyakini alikuwa na umri wa miaka kumi na nane alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miezi mitatu. Mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani kutoka Yerusalemu. 9 Akafanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama vile baba yake alivyokuwa amefanya.
10 Wakati huo, maafisa wa Nebukadneza mfalme wa Babeli walikuja kushambulia Yerusalemu, nao wakauzingira kwa jeshi. 11 Nebukadneza mwenyewe akaupandia mji wakati maafisa wake walipokuwa wameuzingira. 12 Yehoyakini mfalme wa Yuda, mama yake, wahudumu wake, wakuu na maafisa wake wote wakajisalimisha kwa Nebukadneza.
Katika mwaka wa nane wa utawala wa mfalme wa Babeli, akamchukua Yehoyakini kuwa mfungwa. 13 Kama vile Mwenyezi Mungu alivyokuwa amesema, Nebukadneza akaondoa hazina yote kutoka Hekalu la Mwenyezi Mungu na kutoka jumba la mfalme, akavichukua vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani mfalme wa Israeli alikuwa amevitengeneza kwa ajili ya Hekalu la Mwenyezi Mungu. 14 Akawachukua watu wa Yerusalemu wote kwenda uhamishoni: yaani maafisa wote na wapiganaji, watu wenye ustadi wa ufundi na wahunzi, jumla yao watu elfu kumi. Watu maskini sana tu ndio walibaki katika nchi.
15 Nebukadneza akamchukua mateka Yehoyakini hadi Babeli. Pia akawachukua utumwani kutoka Yerusalemu hadi Babeli mama yake mfalme, wake zake, maafisa wake, na viongozi wote wa nchi. 16 Mfalme wa Babeli pia akawahamishia Babeli wapiganaji elfu saba wenye nguvu na tayari kwa vita, na mafundi na wahunzi elfu moja. 17 Akamfanya Matania, ndugu wa baba yake Yehoyakini, kuwa mfalme mahali pake, na akalibadilisha jina lake kuwa Sedekia.
Sedekia mfalme wa Yuda
(2 Nyakati 36:11-12; Yeremia 52:1-3)
18 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na moja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu miaka kumi na moja. Mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, kutoka Libna. 19 Alifanya maovu machoni pa Mwenyezi Mungu, kama alivyofanya Yehoyakimu. 20 Haya yote yalitendeka Yerusalemu na Yuda kwa sababu ya hasira ya Mwenyezi Mungu, naye mwishoni akawaondoa mbele zake.
Basi, Sedekia akaasi dhidi ya mfalme wa Babeli.