3
Siku ya Mwenyezi Mungu
1 Wapendwa, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa mawazo makamilifu. 2 Nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi wetu mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.
3 Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka, wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbovu. 4 Watasema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipofariki, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.” 5 Lakini wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwa tangu zamani, nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa maji. 6 Ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa kwa hayo maji na kuangamizwa. 7 Kwa neno lilo hilo, mbingu za sasa na dunia zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.
8 Lakini wapendwa, msisahau neno hili: kwamba kwa Mwenyezi Mungu, siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Mwenyezi Mungu hakawii kuitimiza ahadi yake, kama watu wengine wanavyokudhani kukawia. Badala yake, yeye anawavumilia ninyi, maana hataki mtu yeyote aangamie, bali kila mtu afikilie toba.
10 Lakini siku ya Mwenyezi Mungu itakuja kama mwizi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu; navyo vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilicho ndani yake kitaunguzwa.
11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, je, ninyi imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu, 12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu. Siku hiyo italeta mbingu kuchomwa moto na kutoweka, na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto. 13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.
14 Kwa sababu hii, wapendwa, kwa kuwa mnatazamia mambo haya, fanyeni bidii ili awakute bila mawaa wala dosari, na mkiwa na amani kwake. 15 Hesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpendwa Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu. 16 Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote, akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha, kama wanavyopotosha Maandiko mengine na kujiletea maangamizi yao wenyewe.
17 Basi, ninyi wapendwa, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwa uthabiti wenu. 18 Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Isa Al-Masihi.
Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.