11
Daudi na Bathsheba
Katika mwanzo wa mwaka mpya, wakati wafalme hutoka kwenda vitani, Daudi akamtuma Yoabu pamoja na watu wa mfalme na jeshi lote la Israeli. Wakawaangamiza Waamoni na kuuzingira mji wa Raba. Lakini Daudi akabaki Yerusalemu.
Ikawa siku moja wakati wa jioni Daudi aliinuka kitandani mwake na kutembeatembea juu ya paa la jumba lake la kifalme. Akiwa kule kwenye paa, akamwona mwanamke akioga. Mwanamke huyo alikuwa mzuri sana wa sura, naye Daudi akatuma mtu mmoja kuuliza habari za huyo mwanamke. Huyo mtu akamwambia Daudi, “Je, huyu si Bathsheba binti Eliamu, naye ni mke wa Uria Mhiti?” Ndipo Daudi akatuma wajumbe kumleta. Huyo mwanamke akaja kwa Daudi, Daudi akakutana naye kimwili. (Huyo mwanamke ndipo tu alikuwa amejitakasa kutoka siku zake za hedhi.) Kisha akarudi nyumbani mwake. Huyo mwanamke akapata mimba akampelekea Daudi ujumbe, kusema, “Mimi ni mjamzito.”
Ndipo Daudi akapeleka ujumbe kwa Yoabu, “Unipelekee Uria Mhiti.” Naye Yoabu akamtuma Uria kwa Daudi. Uria alipofika, Daudi akamuuliza habari za Yoabu, hali za askari na vita kwamba inaendeleaje. Kisha Daudi akamwambia Uria, “Teremka nyumbani mwako ukanawe miguu yako.” Basi Uria akatoka jumba la kifalme, tena zawadi zikamfuata kutoka kwa mfalme. Lakini Uria akalala kwenye ingilio la jumba la kifalme pamoja na watumishi wote wa bwana wake, na hakuteremka kwenda nyumbani mwake.
10 Daudi alipoambiwa kwamba, “Uria hakuenda nyumbani,” Daudi akamuuliza, “Je, si ndiyo tu umefika kutoka safari ya mbali? Kwa nini hukuenda nyumbani?”
11 Uria akamwambia Daudi, “Sanduku la Mungu, na Israeli na Yuda wanakaa kwenye mahema, naye bwana wangu Yoabu na watu wa bwana wangu wamepiga kambi mahali pa wazi. Ningewezaje kwenda nyumbani mwangu ili nile, ninywe na kukutana na mke wangu? Hakika kama uishivyo sitafanya jambo kama hilo!”
12 Ndipo Daudi akamwambia, “Kaa hapa siku moja zaidi, nami kesho nitakutuma urudi.” Kwa hiyo Uria akakaa Yerusalemu siku ile na siku iliyofuata. 13 Kwa ukaribisho wa Daudi, Uria akala na kunywa pamoja naye, Daudi akamlevya. Lakini jioni Uria alitoka kwenda kulala juu ya mkeka wake miongoni mwa watumishi wa bwana wake, hakuenda nyumbani.
14 Kesho yake asubuhi, Daudi akamwandikia Yoabu barua, akamtuma Uria kuipeleka. 15 Ndani ya barua aliandika, “Mweke Uria mstari wa mbele ambapo mapigano ni makali sana. Kisha wewe uondoke ili Uria aangushwe chini na kuuawa.”
16 Hivyo Yoabu alipokuwa ameuzingira mji kwa jeshi, akamweka Uria mahali alipojua kuwa ulinzi wa adui ulikuwa imara sana. 17 Wanaume wa mji walipotoka kwenda kupigana dhidi ya Yoabu, baadhi ya watu katika jeshi la Daudi wakauawa; zaidi ya hayo, Uria Mhiti akafa.
18 Yoabu akampelekea Daudi maelezo yote ya vita. 19 Akamwagiza mjumbe hivi, “Utakapokuwa umemaliza kumpa mfalme maelezo ya vita, 20 hasira ya mfalme yaweza kuwaka, naye aweza kukuuliza, ‘Kwa nini mlisogea karibu hivyo na mji kupigana? Hamkujua kuwa wangeweza kuwapiga mishale kutoka ukutani? 21 Ni nani aliyemuua Abimeleki mwana wa Yerub-Besheth? Je, mwanamke hakutupa juu yake jiwe la juu la kusagia kutoka ukutani, kwa hiyo akafa huko Thebesi? Kwa nini mlisogea hivyo karibu ya ukuta?’ Akikuuliza hivi, ndipo umwambie, ‘Pia mtumishi wako Uria Mhiti amekufa.’ ”
22 Mjumbe akaondoka. Alipowasili akamwambia Daudi kila kitu alichokuwa ametumwa na Yoabu kusema. 23 Mjumbe akamwambia Daudi, “Watu walituzidi nguvu wakatoka nje ya mji dhidi yetu kwenye eneo la wazi, lakini tuliwarudisha nyuma hadi ingilio la mji. 24 Ndipo wapiga upinde walitupa mishale kwa watumishi wako kutoka ukutani, na baadhi ya watu wa mfalme wakafa. Zaidi ya hayo, Uria Mhiti, mtumishi wako, amekufa.”
25 Daudi akamwambia mjumbe, “Ukamwambie Yoabu hivi, ‘Jambo hili lisikutie wasiwasi, upanga hula huyu sawa na ulavyo mwingine. Zidisha mashambulizi dhidi ya mji na uangamize.’ Mwambie Yoabu hivi ili kumtia moyo.”
26 Mke wa Uria aliposikia kwamba mumewe amekufa, akamwombolezea. 27 Baada ya muda wa maombolezo kwisha, Daudi akatumana aletwe nyumbani mwake. Naye akawa mkewe, na akamzalia mwana. Lakini jambo alilofanya Daudi lilimchukiza Mwenyezi Mungu.