15
Hila ya Absalomu
1 Baada ya muda, Absalomu akajipatia magari ya vita na farasi pamoja na watu hamsini wa kupiga mbio mbele yake. 2 Akawa anaamka asubuhi na mapema na kusimama kando ya barabara inayoelekea kwenye lango la mji. Wakati wowote alipokuja mtu yeyote mwenye mashtaka yanayohitaji kuletwa mbele ya mfalme kwa maamuzi, Absalomu naye angemwita na kumuuliza, “Wewe unatoka mji upi?” Naye angejibu, “Mtumishi wako anatoka katika mojawapo ya makabila ya Israeli.” 3 Kisha Absalomu angemwambia, “Tazama, malalamiko yako ni ya haki na sawasawa, lakini hakuna mwakilishi wa mfalme wa kukusikiliza.” 4 Absalomu aliongeza, “Laiti tu ningeteuliwa kuwa mwamuzi katika nchi. Ndipo kila mmoja mwenye mashtaka au shauri angekuja kwangu nami ningeona kwamba anapata haki.”
5 Pia, wakati mtu yeyote alipomkaribia ili kusujudu mbele yake, Absalomu alinyoosha mkono wake, na kumkumbatia na kumbusu. 6 Absalomu akaendelea na tabia hii mbele ya Waisraeli wote waliomjia mfalme kumwomba awape haki; kwa hiyo Absalomu akavutia mioyo ya watu wa Israeli.
7 Hapo mwisho wa mwaka wa nne, Absalomu akamwambia mfalme, “Naomba unipe ruhusa niende Hebroni nikatimize nadhiri niliyomwekea Mwenyezi Mungu. 8 Mtumishi wako alipokuwa huko Geshuri katika nchi ya Aramu, niliweka nadhiri hii: ‘Ikiwa Mwenyezi Mungu atanirudisha Yerusalemu, nitamwabudu Mwenyezi Mungu huko Hebroni.’ ”
9 Mfalme akamwambia, “Nenda kwa amani.” Hivyo akaenda Hebroni.
10 Kisha Absalomu akatuma wajumbe kwa siri katika makabila yote ya Israeli, kusema, “Mara mtakaposikia sauti ya tarumbeta basi semeni, ‘Absalomu ni mfalme huko Hebroni.’ ” 11 Watu mia mbili kutoka Yerusalemu walikuwa wamefuatana na Absalomu. Walikuwa wamealikwa kama wageni nao walienda kwa nia njema, pasipo kujua lolote. 12 Absalomu alipokuwa anatoa dhabihu, pia akatuma aitwe Ahithofeli Mgiloni, mshauri wa Daudi, aje kutoka Gilo, ambao ndio mji wake wa nyumbani. Kwa hiyo mpango wa hila ukapata nguvu, na idadi ya waliofuatana na Absalomu ikaongezeka.
Daudi akimbia
13 Mjumbe akaja na kumwambia Daudi, “Mioyo ya watu wa Israeli inaambatana na Absalomu.”
14 Ndipo Daudi akawaambia maafisa wake wote waliokuwa pamoja naye huko Yerusalemu, “Njooni! Ni lazima tukimbie, la sivyo hakuna hata mmoja wetu atakayeokoka kutoka mkononi mwa Absalomu. Ni lazima tuondoke kwa haraka, la sivyo atakuja mbio na kutupata, atatuangamiza na kuupiga mji kwa upanga.”
15 Maafisa wa mfalme wakamjibu, “Watumishi wako tu tayari kufanya lolote mfalme bwana wetu analochagua.”
16 Mfalme akatoka, pamoja na watu wa nyumbani mwake wakimfuata; lakini akawaacha masuria kumi ili la kile jumba la kifalme. 17 Hivyo mfalme akaondoka, pamoja na watu wote wakimfuata, wakatua mahali mbali kiasi. 18 Watu wake wote wakatembea, wakampita wakiwa wamefuatana na Wakerethi na Wapelethi wote; pia Wagiti wote mia sita waliokuwa wamefuatana naye kutoka Gathi wakapita mbele ya mfalme.
19 Mfalme akamwambia Itai, Mgiti, “Kwa nini ufuatane na sisi? Rudi ukakae pamoja na Mfalme Absalomu. Wewe ni mgeni, mkimbizi kutoka nchini mwako. 20 Ulikuja jana tu. Nami leo nikufanye utangetange pamoja nasi, wakati sijui niendako? Rudi, nawe ukawachukue watu wa kwenu. Wema na uaminifu na viwe pamoja nawe.”
21 Lakini Itai akamjibu mfalme, “Hakika kama Mwenyezi Mungu aishivyo na kama mfalme bwana wangu aishivyo, popote mfalme bwana wangu atakapokuwa, ikiwa ni kuishi au kufa, hapo ndipo mtumishi wako atakapokuwa.”
22 Daudi akamwambia Itai, “Songa mbele, endelea.” Kwa hiyo Itai, Mgiti, akaendelea pamoja na watu wake wote, pia jamaa zote waliokuwa pamoja naye.
23 Watu wote wa nje ya mji wakalia kwa sauti wakati watu wote walipokuwa wakipita. Mfalme naye akavuka Bonde la Kidroni, nao watu wote wakaelekea jangwani.
24 Sadoki pia alikuwako, kadhalika Walawi wote waliokuwa pamoja naye walikuwa wamechukua Sanduku la Agano la Mungu. Wakaweka chini Sanduku la Mungu, naye Abiathari akatoa dhabihu hadi watu wote walipokuwa wameondoka mjini.
25 Kisha mfalme akamwambia Sadoki, “Rudisha Sanduku la Mungu mjini. Ikiwa nitapata kibali mbele za Mwenyezi Mungu, atanirudisha, nami nitaliona Sanduku hili tena pamoja na Maskani yake. 26 Lakini kama yeye atasema, ‘Mimi sipendezwi nawe,’ basi mimi niko tayari; yeye na anifanye chochote aonacho chema kwake.”
27 Pia mfalme alimwambia kuhani Sadoki, “Je, wewe si mwonaji? Rudi mjini kwa amani pamoja na mwanao Ahimaasi na Yonathani mwana wa Abiathari. Wewe na Abiathari wachukueni wana wenu wawili. 28 Nitasubiri kwenye vivuko katika jangwa hadi neno litakapotoka kwenu kuniarifu.” 29 Kwa hiyo Sadoki na Abiathari wakarudisha Sanduku la Mungu hadi Yerusalemu na kukaa huko.
30 Bali Daudi akaendelea, akapanda Mlima wa Mizeituni, akaenda huku analia, akiwa amefunika kichwa chake, bila viatu miguuni. Watu wote waliokuwa pamoja naye nao wakafunika vichwa vyao, wakawa wanapanda mlima huku wanalia. 31 Basi Daudi alikuwa ameambiwa, “Ahithofeli alikuwa miongoni mwa washiriki wa njama ya Absalomu.” Ndipo Daudi akaomba, akisema, “Ee Mwenyezi Mungu, geuza ushauri wa Ahithofeli kuwa ujinga.”
32 Daudi alipofika kwenye kilele cha mlima, mahali watu walikuwa wamezoea kumwabudu Mungu, Hushai Mwarki alikuwako kumlaki, akiwa amerarua joho lake, na akiwa na mavumbi kichwani. 33 Daudi akamwambia, “Ukienda pamoja nami, utakuwa mzigo kwangu. 34 Lakini ukirudi mjini na kumwambia Absalomu, ‘Nitakuwa mtumishi wako, ee mfalme; nilikuwa mtumishi wa baba yako wakati uliopita, lakini sasa nitakuwa mtumishi wako,’ basi utaweza kunisaidia kwa kupinga ushauri wa Ahithofeli. 35 Je, makuhani Sadoki na Abiathari hawatakuwa pamoja nawe? Waambie lolote utakalosikia katika jumba la mfalme. 36 Wana wao wawili, Ahimaasi mwana wa Sadoki na Yonathani mwana wa Abiathari, wako pamoja nao huko. Watume kwangu na lolote utakalosikia.”
37 Kwa hiyo Hushai, rafiki wa Daudi, akafika Yerusalemu wakati Absalomu alipokuwa anaingia mjini.