17
1 Ahithofeli akamwambia Absalomu, “Nipe ruhusa niwachague watu elfu kumi na mbili, nao waanze safari usiku huu huu kumfuatia Daudi. 2 Nitamshambulia wakati akiwa amechoka na ni dhaifu. Nitampiga na hofu, na kisha watu wote walio pamoja naye watakimbia. Nitampiga mfalme peke yake 3 na kuwarudisha watu wote kwako. Kifo cha mtu yule unayemtafuta kitamaanisha kurudi kwa wote, hakuna hata mtu mmoja atakayeumizwa.” 4 Mpango huu ulionekana mzuri kwa Absalomu na kwa wazee wote wa Israeli.
5 Lakini Absalomu akasema, “Pia mwiteni Hushai, Mwarki, ili tuweze kusikia anachokisema.” 6 Hushai alipokuja, Absalomu akasema, “Ahithofeli ametoa ushauri huu. Je, tufanye anavyosema? Kama sivyo, tupe maoni yako.”
7 Hushai akamjibu Absalomu, “Ushauri alioutoa Ahithofeli haufai kwa wakati huu. 8 Unamfahamu baba yako na watu wake, ni wapiganaji hodari, nao ni wakali kama dubu aliyepokonywa watoto wake. Zaidi ya hayo, baba yako ni mpiganaji jasiri, usiku hatalala pamoja na vikosi. 9 Hata sasa, amefichwa ndani ya pango au mahali pengine. Kama atatangulia kushambulia vikosi vyako, yeyote asikiaye habari hii atasema, ‘Kuna machinjo makubwa miongoni mwa vikosi vinavyomfuata Absalomu.’ 10 Basi hata yule askari hodari kuliko wengine wote, ambaye moyo wake ni kama wa simba, atayeyuka kwa hofu, kwa maana Israeli yote wanajua kwamba baba yako ni mpiganaji na kwamba wale walio pamoja naye ni watu hodari.
11 “Kwa hiyo nakushauri: Israeli wote na wakusanyike kwako, kuanzia Dani hadi Beer-Sheba, wakiwa wengi kama mchanga wa ufuo wa bahari; wakusanyike kwako, nawe ukiwaongoza vitani. 12 Ndipo tutakapomshambulia popote atakapoonekana, nasi tutamwangukia kama umande unavyoshuka juu ya ardhi. Yeye mwenyewe na watu wake hakuna atakayeachwa hai. 13 Kama atakimbilia katika mji wowote, basi Israeli wote watazungushia mji ule kamba, nasi tutauburuta mji huo hadi bondeni, wala isionekane hata changarawe ya huo mji.”
14 Absalomu na wanaume wote wa Israeli wakasema, “Ushauri wa Hushai, Mwarki, ni mwema kuliko ule wa Ahithofeli.” Kwa maana Mwenyezi Mungu alikuwa amekusudia kupinga ushauri mwema wa Ahithofeli, ili kuleta maafa kwa Absalomu.
15 Hushai akawaambia makuhani Sadoki na Abiathari, “Ahithofeli amemshauri Absalomu na wazee wa Israeli kufanya hivi na hivi, lakini mimi nimewashauri wao kufanya lile na lile. 16 Sasa tumeni ujumbe haraka na kumwambia Daudi, ‘Usiku huu usilale kwenye vivuko katika jangwa; vuka bila kukosa, la sivyo, mfalme pamoja na watu wote waliofuatana naye watamezwa.’ ”
17 Yonathani na Ahimaasi walikuwa wakingoja huko En-Rogeli. Naye mjakazi mmoja alipaswa kuwapasha habari nao wakawa waende kumwambia Mfalme Daudi, kwa maana wasingetaka kujihatarisha kuonekana wakiingia mjini. 18 Lakini kijana mmoja mwanaume akawaona, naye akamwambia Absalomu. Basi wote wawili wakaondoka haraka, wakaenda hadi kwenye nyumba ya mtu mmoja huko Bahurimu. Mtu huyo alikuwa na kisima uani mwake, nao Yonathani na Ahimaasi wakateremka ndani ya kisima hicho. 19 Mkewe akachukua kifuniko, akakiweka juu ya mdomo wa kile kisima na kuanika nafaka juu yake. Hakuna mtu yeyote aliyefahamu chochote kuhusu jambo hilo.
20 Watu wa Absalomu walipofika kwa huyo mwanamke, wakamuuliza, “Wako wapi Ahimaasi na Yonathani?”
Huyo mwanamke akawajibu, “Walivuka kijito.” Watu wa Absalomu wakapekua lakini hawakuwaona hata mmoja, hivyo wakarudi Yerusalemu.
21 Baada ya watu hao kuondoka, wale watu wawili yaani Yonathani na Ahimaasi wakapanda kutoka mle kisimani na kwenda kumpasha Mfalme Daudi habari. Wakamwambia, “Ondoka, uvuke mto haraka. Ahithofeli ameshauri hivi na hivi dhidi yako.” 22 Kwa hiyo Daudi na watu wote aliokuwa nao waliondoka na kuvuka Yordani. Kufika wakati wa mapambazuko, hapakuwa na mtu hata mmoja aliyekuwa hajavuka Mto Yordani.
23 Ahithofeli alipoona kwamba ushauri wake haukufuatwa, akatandika punda wake, akaondoka kwenda nyumbani mwake kwenye mji wake. Akaiweka nyumba yake katika utaratibu, kisha akajinyonga mwenyewe. Hivyo akafa na akazikwa katika kaburi la baba yake.
Kifo cha Absalomu
24 Daudi akaenda Mahanaimu, naye Absalomu akavuka Yordani pamoja na wanaume wote wa Israeli. 25 Absalomu alikuwa amemweka Amasa awe mkuu wa jeshi badala ya Yoabu. Amasa alikuwa mwana wa mtu mmoja aliyeitwa Yetheri, Mwishmaeli aliyekuwa amemwoa Abigaili binti Nahashi, dada yake Seruya mamaye Yoabu. 26 Waisraeli na Absalomu wakapiga kambi huko nchi ya Gileadi.
27 Daudi alipofika Mahanaimu, Shobi mwana wa Nahashi kutoka Raba ya Waamoni, Makiri mwana wa Amieli kutoka Lo-Debari, na Barzilai Mgileadi kutoka Rogelimu 28 wakaleta matandiko ya kitanda, mabakuli na vyombo vya mfinyanzi. Walileta pia ngano na shayiri, unga na bisi, maharagwe na kunde, 29 asali na maziwa yaliyoganda, kondoo na jibini kutoka maziwa ya ng’ombe kwa ajili ya Daudi na watu wake ili wale. Kwa maana walisema, “Watu wameona njaa, tena wamechoka na wamepata kiu huko jangwani.”