20
Sheba aasi dhidi ya Daudi
Basi, kulikuwa na mtu mbaya sana aliyeitwa Sheba mwana wa Bikri, Mbenyamini, aliyekuwako huko. Akapiga tarumbeta na kupaza sauti,
“Hatuna fungu katika Daudi,
wala hatuna sehemu
katika mwana wa Yese!
Kila mtu aende kwenye hema lake,
enyi Israeli!”
Kwa hiyo wanaume wote wa Israeli wakamwacha Daudi na kumfuata Sheba mwana Bikri. Lakini wanaume wa Yuda wakawa karibu na mfalme wao katika safari yote kutoka Yordani hadi Yerusalemu.
Daudi aliporudi katika jumba lake la kifalme huko Yerusalemu, aliwachukua wale masuria kumi aliokuwa amewaacha ili kutunza jumba la kifalme, na kuwaweka ndani ya nyumba chini ya ulinzi. Akawapa mahitaji yao lakini hakukutana nao kimwili. Waliwekwa kifungoni wakaishi kama wajane hadi kifo chao.
Ndipo mfalme akamwambia Amasa, “Waite wanaume wa Yuda waje kwangu katika muda wa siku tatu, nawe mwenyewe uwepo hapa.” Lakini Amasa alipoenda kuwaita Yuda, alichukua muda mrefu zaidi ya ule mfalme aliokuwa amemwekea.
Daudi akamwambia Abishai, “Sasa Sheba mwana wa Bikri atatuletea madhara kuliko Absalomu. Wachukue watumishi wa bwana wako na umfuatie, la sivyo atapata mji wenye ngome na kututoroka.” Hivyo watumishi wa Yoabu, na Wakerethi na Wapelethi, pamoja na mashujaa wenye nguvu wote wakaondoka chini ya uongozi wa Abishai. Wakatoka Yerusalemu ili kumfuata Sheba mwana wa Bikri.
Walipokuwa kwenye mwamba mkubwa huko Gibeoni, Amasa alikuja kuwalaki. Yoabu alikuwa amevaa mavazi yake ya kijeshi; juu yake alifunga mkanda kiunoni wenye upanga ndani ya ala. Alipokuwa akienda mbele, ule upanga ukaanguka kutoka ala.
Yoabu akamwambia Amasa, “U hali gani, ndugu yangu?” Kisha Yoabu akamshika Amasa ndevu kwa mkono wake wa kuume ili ambusu. 10 Amasa hakuona upanga uliokuwa mkononi mwa Yoabu, naye Yoabu akamchoma nao tumboni, nayo matumbo yake yakamwagika chini. Pasipo kuchomwa mara ya pili, Amasa akafa. Basi Yoabu na Abishai nduguye wakamfuatia Sheba mwana wa Bikri.
11 Mmoja wa watu wa Yoabu akasimama kando ya Amasa, akasema, “Yeyote ampendaye Yoabu na yeyote aliye upande wa Daudi, na amfuate Yoabu!” 12 Amasa alikuwa akigaagaa katika damu yake katikati ya barabara; mtu mmoja akaona kwamba vikosi vyote vilikuwa vinasimama pale. Huyo mtu alipotambua kwamba kila aliyefika pale Amasa alipokuwa alisimama, alimburuta Amasa kutoka barabarani hadi kwenye shamba na kutupia nguo juu yake. 13 Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri.
14 Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walikusanyika na kumfuata. 15 Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumzingira Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wakijaribu kuubomoa ukuta ili kuuangusha chini, 16 mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.” 17 Yoabu alienda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?”
Akamjibu, “Ndiye mimi.”
Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.”
18 Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri. 19 Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi wa Mwenyezi Mungu?”
20 Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu. 21 Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima ya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Mkabidhini mtu huyu mmoja kwangu, nami nitajiondoa katika mji huu.”
Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.”
22 Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani mwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu.
23 Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli;
Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi;
24 Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa;
Yehoshafati mwana wa Ahiludi aliweka kumbukumbu;
25 Sheva*au Shausha (1 Nyakati 18:16) alikuwa mwandishi;
Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani;
26 na Ira Myairi, alikuwa kuhani wa Daudi.

*20:25 au Shausha (1 Nyakati 18:16)