22
Wimbo wa Daudi wa ushindi
(Zaburi 18)
1 Daudi alimwimbia Mwenyezi Mungu maneno ya wimbo huu Mwenyezi Mungu alipomwokoa mikononi mwa adui zake wote, na pia mkononi mwa Sauli. 2 Akasema:
“Mwenyezi Mungu ni mwamba wangu,
ngome yangu na mwokozi wangu,
3 Mungu wangu ni mwamba wangu, ninayemkimbilia,
ngao yangu na pembe*pembe inawakilisha nguvu ya wokovu wangu.
Yeye ni ngome yangu, kimbilio langu na mwokozi wangu,
huniokoa kutoka kwa watu wenye jeuri.
4 “Ninamwita Mwenyezi Mungu, anayestahili kusifiwa,
nami ninaokolewa kutoka kwa adui zangu.
5 Mawimbi ya mauti yalinizunguka,
mafuriko ya maangamizi yalinilemea.
6 Kamba za Kuzimu†Kuzimu kwa Kiebrania ni Sheol, yaani Shimo lisilo na mwisho. zilinizunguka,
mitego ya mauti ilinikabili.
7 “Katika shida yangu nalimwita Mwenyezi Mungu,
nilimlilia Mungu wangu.
Kutoka Hekaluni mwake alisikia sauti yangu,
kilio changu kikafika masikioni mwake.
8 Dunia ilitetemeka na kutikisika,
misingi ya mbingu ikatikisika,
vilitetemeka kwa sababu
alikuwa amekasirika.
9 Moshi ukapanda kutoka puani mwake,
moto uteketezao ukatoka kinywani mwake,
makaa ya moto yaliyowaka
yakatoka ndani yake.
10 Akazipasua mbingu akashuka chini,
mawingu meusi yalikuwa chini ya miguu yake.
11 Alipanda juu ya kerubi akaruka,
akapaa juu kwa mabawa ya upepo.
12 Alifanya giza hema lake la kujifunika:
mawingu meusi ya mvua ya angani.
13 Kutokana na mwanga wa uwepo wake
mwanga wa radi ukatoka.
14 Mwenyezi Mungu alinguruma kutoka mbinguni,
sauti ya Aliye Juu Sana ilisikika.
15 Aliipiga mishale na kutawanya adui,
akawafukuza kwa umeme mkubwa wa radi.
16 Mabonde ya bahari yalifunuliwa,
na misingi ya dunia ikawa wazi
kwa kukaripia kwake Mwenyezi Mungu,
kwa uvumi wa pumzi kutoka puani mwake.
17 “Alinyoosha mkono kutoka juu na kunishika;
alinitoa kutoka kilindi cha maji makuu.
18 Aliniokoa kutoka adui yangu mwenye nguvu nyingi,
kutoka adui zangu waliokuwa na nguvu nyingi kuliko mimi.
19 Walinikabili siku ya msiba wangu,
lakini Mwenyezi Mungu alikuwa msaada wangu.
20 Alinileta nje mahali penye nafasi tele,
akaniokoa kwa kuwa alipendezwa nami.
21 “Mwenyezi Mungu alinitendea sawasawa na uadilifu wangu;
sawasawa na usafi wa mikono yangu amenilipa.
22 Kwa maana nimezishika njia za Mwenyezi Mungu;
sijatenda ubaya nikamwacha Mungu wangu.
23 Sheria zake zote zi mbele yangu,
wala sijayaacha maagizo yake.
24 Nimekuwa sina hatia mbele zake,
nami nimejilinda nisitende dhambi.
25 Mwenyezi Mungu amenilipa sawasawa na uadilifu wangu,
sawasawa na usafi wangu machoni pake.
26 “Kwa yeye aliye mwaminifu unajionesha kuwa mwaminifu,
kwa asiye na hatia unajionesha kutokuwa na hatia,
27 kwa aliye mtakatifu unajionesha kuwa mtakatifu,
lakini kwa aliyepotoka unajionesha kuwa mkaidi.
28 Wewe huwaokoa wanyenyekevu,
lakini macho yako ni juu ya wenye kiburi
ili uwashushe.
29 Wewe ni taa yangu, Ee Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu hulifanya giza langu
kuwa mwanga.
30 Kwa msaada wako naweza kushinda jeshi,
nikiwa pamoja na Mungu wangu
nitaweza kuruka ukuta.
31 “Kuhusu Mungu, njia yake ni kamilifu;
neno la Mwenyezi Mungu halina dosari.
Yeye ni ngao kwa wote
wanaokimbilia kwake.
32 Kwa maana ni nani aliye Mungu
zaidi ya Mwenyezi Mungu?
Ni nani aliye Mwamba
isipokuwa Mungu wetu?
33 Mungu ndiye anivikaye nguvu,
na kufanya njia yangu kuwa kamilifu.
34 Huifanya miguu yangu kama miguu ya kulungu,
huniwezesha kusimama mahali palipo juu.
35 Huifundisha mikono yangu kupigana vita;
mikono yangu inaweza kupinda upinde wa shaba.
36 Hufanya msaada wa wokovu wako kuwa ngao yangu;
msaada wako umeniinua niwe mkuu.
37 Huyapanua mapito yangu,
ili miguu yangu isiteleze.
38 “Niliwafuatia adui zangu na nikawaseta,
sikurudi nyuma hadi walipoangamizwa.
39 Niliwaseta kabisa, nao hawakuweza kuinuka tena;
walianguka chini ya miguu yangu.
40 Ulinivika nguvu kwa ajili ya kupigana vita;
uliwafanya adui zangu wasujudu miguuni pangu.
41 Uliwafanya adui zangu wageuke na kukimbia,
nami nikawaangamiza adui zangu.
42 Walipiga yowe, lakini hapakuwa na yeyote wa kuwaokoa;
walimlilia Mwenyezi Mungu, lakini hakuwajibu.
43 Niliwaponda kama mavumbi ya nchi;
niliwaponda na kuwakanyaga kama tope barabarani.
44 “Umeniokoa kutokana na mashambulizi ya watu wangu;
umenihifadhi mimi kama kiongozi wa mataifa.
Watu ambao sikuwajua wananitumikia,
45 nao wageni huja wakininyenyekea,
mara wanisikiapo, hunitii.
46 Wote wanalegea,
wanatoka katika ngome zao wakitetemeka.
47 “Mwenyezi Mungu yu hai! Sifa ni kwa Mwamba wangu!
Atukuzwe Mungu, Mwamba, Mwokozi wangu!
48 Yeye ndiye Mungu anilipiziaye kisasi,
ayawekaye mataifa chini yangu,
49 aniwekaye huru toka kwa adui zangu.
Uliniinua juu ya adui zangu;
uliniokoa toka kwa watu wajeuri.
50 Kwa hiyo nitakusifu, Ee Mwenyezi Mungu, kati ya mataifa;
nitaliimbia sifa jina lako.
51 “Humpa mfalme wake ushindi mkuu;
huonesha fadhili zake kwa mpakwa mafuta wake,
kwa Daudi na wazao wake milele.”