2
Yule mtu wa kuasi
Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Isa Al-Masihi na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi, msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho, wala neno la unabii, au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, kusema kwamba siku ya Mwenyezi Mungu imekwisha kuwepo. Mtu yeyote asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja hadi uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa. Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.
Je, hamkumbuki kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya? Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia. Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo hadi atakapoondolewa. Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Isa atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake. Kuja kwa yule mwasi kutalingana na vile Shetani hufanya kazi. Atatumia nguvu za aina mbalimbali katika miujiza, na ishara na ajabu za uongo, 10 na katika njia zote ambazo uovu hudanganya wanaoangamia. Wanaangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli ili wapate kuokolewa. 11 Kwa sababu hii, Mungu anawatumia nguvu ya udanganyifu, ili waamini uongo, 12 na hivyo wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.
Simameni imara
13 Lakini inatupasa kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana Isa, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho wa Mungu kwa kuiamini kweli. 14 Kwa kusudi hili Mungu aliwaita ninyi kupitia Injili tuliyowahubiria, ili mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana wetu Isa Al-Masihi.
15 Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.
16 Bwana wetu Isa Al-Masihi mwenyewe na Mungu, Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema, 17 awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.