2
Kushuka kwa Roho wa Mungu
Siku ya Pentekoste ilipowadia, waumini wote walikuwa mahali pamoja. Ghafula, sauti kama mvumo mkubwa wa upepo mkali ikatoka mbinguni, ikaijaza nyumba yote walimokuwa wameketi. Zikatokea ndimi kama za moto zilizogawanyika na kutua juu ya kila mmoja wao. Wote wakajazwa na Roho Mtakatifu wa Mungu, wakaanza kunena kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia.
Basi walikuwako Yerusalemu Wayahudi wanaomcha Mungu kutoka kila taifa chini ya mbingu. Waliposikia sauti hii, umati wa watu walikusanyika pamoja wakistaajabu, kwa sababu kila mmoja wao aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakiwa wameshangaa na kustaajabu, wakauliza, “Je, hawa wote wanaozungumza si Wagalilaya? Imekuwaje basi kila mmoja wetu anawasikia wakinena kwa lugha yake ya kuzaliwa? Wapathi, Wamedi, Waelami, wakazi wa Mesopotamia, Yudea, Kapadokia, Ponto na jimbo la Asia, 10 Frigia, Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni kutoka Rumi 11 (Wayahudi na wale walioongokea dini ya Kiyahudi), Wakrete na Waarabu: sote tunawasikia watu hawa wakisema mambo makuu ya ajabu ya Mungu katika lugha zetu wenyewe.” 12 Wakiwa wameshangaa na kufadhaika wakaulizana, “Ni nini maana ya mambo haya?”
13 Lakini wengine wakawadhihaki wakasema, “Hawa wamelewa kwa divai!”
Petro ahutubia umati
14 Ndipo Petro akasimama pamoja na wale mitume kumi na mmoja, akapaza sauti yake na kuhutubia umati ule wa watu, akasema: “Wayahudi wenzangu na nyote mnaoishi Yerusalemu, nisikilizeni kwa makini, ili jambo hili lijulikane kwenu. 15 Hakika watu hawa hawajalewa kama mnavyodhania, kwa kuwa sasa ni saa tatu asubuhi! 16 La, hili ni jambo lililotabiriwa na nabii Yoeli, akisema:
17 “ ‘Katika siku za mwisho, asema Mungu,
nitamimina Roho wangu
juu ya wote wenye mwili.
Wana wenu wa kiume na wa kike watatabiri,
vijana wenu wataona maono,
na wazee wenu wataota ndoto.
18 Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake,
katika siku zile nitamimina Roho wangu,
nao watatabiri.
19 Nami nitaonesha maajabu juu mbinguni,
na ishara chini duniani:
damu, moto, na mawimbi ya moshi.
20 Jua litakuwa giza
na mwezi utakuwa mwekundu kama damu,
kabla ya kuja siku ile kuu ya Mwenyezi Mungu
iliyo tukufu.
21 Na kila mtu atakayeliitia
jina la Mwenyezi Mungu, ataokolewa.’
22 “Enyi Waisraeli, sikilizeni maneno haya nisemayo: Isa Al-Nasiri alikuwa mtu aliyethibitishwa kwenu na Mungu kwa miujiza, maajabu na ishara, ambayo Mungu alitenda miongoni mwenu kupitia kwake, kama ninyi wenyewe mjuavyo. 23 Baada ya huyu mtu kutolewa kwenu kwa mpango wa Mungu uliokusudiwa kwa kujua kwake Mungu tangu zamani, ninyi mlimuua kwa kumsulubisha msalabani, kwa mikono ya watu waovu. 24 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu akamwondolea uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana yeye kushikiliwa na nguvu za mauti. 25 Kwa maana Daudi asema hivi kumhusu:
“ ‘Nilimwona Bwana mbele yangu daima.
Kwa sababu yuko mkono wangu wa kuume,
sitatikisika.
26 Kwa hiyo moyo wangu unafurahia,
na ulimi wangu unashangilia;
mwili wangu nao utapumzika kwa tumaini.
27 Kwa maana hutaniacha kaburini,
wala hutamwacha Aliye Mtakatifu wako kuona uharibifu.
28 Umenionesha njia za uzima,
utanijaza na furaha mbele zako.’
29 “Ndugu zangu Waisraeli, nataka niwaambie kwa uhakika kwamba baba yetu wa zamani Daudi alikufa na kuzikwa, nalo kaburi lake lipo hapa hadi leo. 30 Lakini alikuwa nabii na alijua ya kuwa Mungu alikuwa amemwahidi kwa kiapo, kwamba angemweka mmoja wa wazao wake penye kiti chake cha utawala. 31 Daudi, akiona mambo yaliyo mbele, akanena kuhusu kufufuka kwa Al-Masihi*Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta., kwamba hakuachwa kaburini, wala mwili wake haukuona uharibifu. 32 Mungu alimfufua huyu Isa, na sisi sote ni mashahidi wa jambo hilo. 33 Basi yeye ametukuzwa hadi mkono wa kuume wa Mungu, na amepokea kutoka kwa BabaJina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi. ahadi ya Roho Mtakatifu wa Mungu, naye amemimina kile mnachoona sasa na kusikia. 34 Kwa kuwa Daudi hakupaa kwenda mbinguni, lakini anasema,
“ ‘Bwana alimwambia Bwana wangu:
“Keti mkono wangu wa kuume,
35 hadi nitakapowaweka adui zako
chini ya miguu yako.” ’
36 “Kwa hiyo Israeli wote na wajue jambo hili kwa uhakika kwamba: Mungu amemfanya huyu Isa, ambaye ninyi mlimsulubisha, kuwa Bwana na Al-Masihi.”
Waumini waongezeka
37 Watu waliposikia maneno haya yakawachoma mioyo yao, wakawauliza Petro na wale mitume wengine, “Ndugu zetu tufanye nini?”
38 Petro akawajibu, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Isa Al-Masihi, ili mpate kusamehewa dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho wa Mungu. 39 Kwa kuwa ahadi hii ni kwa ajili yenu na watoto wenu, na kwa wote walio mbali, na kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu atamwita amjie.”
40 Petro akawaonya kwa maneno mengine mengi na kuwasihi akisema, “Jiepusheni na kizazi hiki kilichopotoka.” 41 Wale wote waliopokea ujumbe wa Petro kwa furaha wakabatizwa, na siku ile waliongezeka watu wapatao elfu tatu.
Ushirika wa waumini
42 Nao wakadumu katika mafundisho ya mitume, katika ushirika, katika kumega mkate na katika kusali. 43 Kila mtu akaingiwa na hofu ya Mungu, nayo miujiza mingi na ishara zikafanywa na mitume. 44 Waumini wote walikuwa mahali pamoja, nao wakashirikiana katika mambo yote. 45 Waliuza mali yao na vitu walivyokuwa navyo, kila mtu akagawiwa kadiri ya mahitaji yake. 46 Siku zote kwa moyo mmoja walikutana ndani ya ukumbi wa HekaluNyumba kuu ya ibada kwa Waisraeli iliyokuwa Yerusalemu., wakimega mkate nyumba kwa nyumba, wakila chakula chao kwa furaha na moyo mweupe, 47 wakimsifu Mungu na kuwapendeza watu wote. Kila siku Bwana akaliongeza kundi la waumini wa Isa wale waliokuwa wakiokolewa.

*2:31 Al-Masihi maana yake Aliyetiwa mafuta.

2:33 Jina Baba linaonesha uhusiano maalum wa Isa na Mwenyezi Mungu. Kwa mwanadamu, Mwenyezi Mungu ni Baba kupitia uhusiano unaopatikana katika kumtumaini Isa Al-Masihi.

2:46 Nyumba kuu ya ibada kwa Waisraeli iliyokuwa Yerusalemu.