10
Kornelio amwita Petro
1 Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu aliyeitwa Kornelio, aliyekuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. 2 Yeye na jamaa yake yote walikuwa wacha Mungu; alitoa kwa ukarimu kwa wale walio na mahitaji na kumwomba Mungu mara kwa mara. 3 Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”
4 Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”
Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu. 5 Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro. 6 Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”
7 Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia. 8 Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.
Maono ya Petro
9 Siku iliyofuata, walipokuwa wanaukaribia mji, yapata saa sita mchana, Petro alipanda juu ya nyumba kuomba. 10 Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walikuwa wakiandaa chakula, akalala usingizi mzito sana. 11 Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama kitambaa kikubwa kikishushwa duniani kwa ncha zake nne. 12 Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao nchini, na ndege wa angani. 13 Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”
14 Petro akajibu, “La hasha, Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu chochote kilicho najisi.”
15 Ile sauti ikasema naye mara ya pili, “Usikiite najisi kitu chochote Mungu alichokitakasa.”
16 Jambo hili lilitokea mara tatu, na ghafula kile kitambaa kikarudishwa mbinguni.
17 Petro alipokuwa akisumbuka kuhusu maana ya maono hayo, wale watu waliotumwa na Kornelio waliipata nyumba ya Simoni, wakasimama kwenye lango. 18 Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.
19 Wakati Petro akiwa anafikiria kuhusu yale maono, Roho wa Mungu akamwambia, “Simoni, kuna watu watatu wanaokutafuta. 20 Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”
21 Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”
22 Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na Kornelio yule jemadari. Yeye ni mtu mwema anayemcha Mungu, na anaheshimiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika mtakatifu akukaribishe nyumbani mwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” 23 Basi Petro akawakaribisha ndani wawe wageni wake. Kesho yake akaondoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu kutoka Yafa wakafuatana naye.
Petro nyumbani mwa Kornelio
24 Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa na rafiki zake wa karibu. 25 Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni mwake kwa heshima. 26 Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”
27 Petro alipokuwa akizungumza naye, akaingia ndani na kuwakuta watu wengi wamekusanyika. 28 Akawaambia, “Mnajua kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu wa Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionesha kwamba nisimwite mtu yeyote kuwa najisi au asiye safi. 29 Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lolote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”
30 Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu aliyevaa nguo zilizong’aa akasimama mbele yangu, 31 akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na misaada yako kwa maskini imekumbukwa mbele za Mungu. 32 Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’ 33 Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”
Hotuba ya Petro
34 Ndipo Petro akafungua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35 lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye. 36 Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza Injili ya amani kupitia kwa Isa Al-Masihi. Yeye ni Bwana wa wote. 37 Mnajua yale yaliyotukia katika Yudea yote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yahya: 38 Jinsi Mungu alivyompaka mafuta Isa Al-Nasiri katika Roho wa Mungu, na jinsi alivyoenda kila mahali akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za ibilisi, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.
39 “Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Yudea na Yerusalemu. Wakamuua kwa kumtundika msalabani. 40 Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41 Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42 Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba ndiye alipakwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. 43 Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”
Watu wa mataifa wapokea Roho wa Mungu
44 Petro alipokuwa akisema maneno haya, Roho Mtakatifu wa Mungu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45 Wale waumini waliokuwa wametahiriwa waliokuja na Petro walishangaa kwa kuona kuwa kipawa cha Roho wa Mungu kimemwagwa juu ya watu wa Mataifa. 46 Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.
Ndipo Petro akasema, 47 “Je, kuna mtu yeyote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu wa Mungu kama sisi tulivyompokea.” 48 Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Isa Al-Masihi. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.