Baraza la Yerusalemu na matokeo yake
15
(Matendo 15:1-35)
Baraza la Yerusalemu
Baadhi ya watu wakashuka Antiokia kutoka Yudea, nao wakawa wanawafundisha waumini: “Msipotahiriwa kulingana na desturi aliyofundisha Musa, hamwezi kuokoka.” Baada ya Paulo na Barnaba kutokubaliana nao kukawa na mabishano makali, Paulo na Barnaba na baadhi ya wengine miongoni mwao wakachaguliwa kwenda Yerusalemu ili kujadiliana jambo hili na mitume na wazee. Hivyo wakatumwa na waumini. Wakapitia Foinike na Samaria, wakielezea jinsi watu wa Mataifa walivyoongoka. Habari hizi zikaleta furaha kubwa kwa ndugu wote. Walipofika Yerusalemu, walipokelewa na kundi la waumini na mitume pamoja na wazee. Ndipo Paulo na Barnaba wakawaarifu kila kitu Mungu alichokuwa amefanya kupitia kwao.
Ndipo baadhi ya waumini waliokuwa wa dhehebu la Mafarisayo*Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli. wakasimama na kusema, “Hao watu wa Mataifa lazima watahiriwe na waagizwe kutii Torati ya Musa.”
Mitume na wazee wakakutana pamoja ili kufikiri jambo hili. Baada ya majadiliano mengi, Petro akasimama na kusema, “Ndugu zangu, mnajua kwamba siku za kwanza Mungu alinichagua ili kwa midomo yangu watu wa Mataifa wapate kusikia ujumbe wa Injili na kuamini. Mungu, ajuaye mioyo ya watu, alionesha kwamba anawakubali kwa kuwapa Roho Mtakatifu wa Mungu kama vile alivyotupatia sisi. Mungu hakutofautisha kati yetu na wao, bali alitakasa mioyo yao kwa imani. 10 Sasa basi, mbona mnataka kumjaribu Mungu kwa kuweka nira shingoni mwa wanafunzi ambayo baba zetu wala sisi hatukuweza kuibeba? 11 Lakini sisi tunaamini ya kuwa tunaokolewa kwa neema ya Bwana wetu Isa Al-Masihi, kama wao wanavyookolewa.”
12 Kusanyiko lote wakakaa kimya, wakawasikiliza Paulo na Barnaba wakieleza jinsi Mungu alivyowatumia kutenda ishara na maajabu kwa watu wa Mataifa. 13 Walipomaliza kunena, Yakobo akasema, “Ndugu zangu, nisikilizeni. 14 Simoni amekwisha kutueleza jinsi Mungu, kwa mara ya kwanza alivyoonesha kuhusika kwa kujichagulia watu kutoka watu wa Mataifa kwa ajili ya Jina lake. 15 Maneno ya manabii yanakubaliana na jambo hili, kama ilivyoandikwa:
16 “ ‘Baada ya mambo haya nitarudi,
nami nitajenga upya
nyumba ya Daudi iliyoanguka.
Nitajenga tena magofu yake
na kuisimamisha,
17 ili wanadamu wengine wote
wapate kumtafuta Mwenyezi Mungu,
hata wale watu wa Mataifa wote
ambao wanaitwa kwa Jina langu,
asema Mwenyezi Mungu, anayefanya mambo haya,’
18 ambayo yamejulikana tangu zamani.
19 “Kwa hivyo uamuzi wangu ni kwamba, tusiwataabishe watu wa Mataifa wanaomgeukia Mungu. 20 Badala yake, tuwaandikie kwamba wajiepushe na vyakula vilivyonajisiwa kwa kutolewa sanamu, wajiepushe na uasherati, au kula mnyama aliyenyongwa, na damu. 21 Kwa maana katika kila mji kwa vizazi vilivyopita, Musa amekuwa na wale wanaotangaza sheria yake kwa kuwa imekuwa ikisomwa kwa sauti kubwa katika masinagogiNyumba za ibada na mafunzo. kila Sabato.”
Barua kwa waumini wa Mataifa
22 Mitume na wazee, pamoja na kundi la waumini wote, wakaamua kuwachagua baadhi ya watu wao na kuwatuma Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba. Wakamchagua Yuda aitwaye Barsaba, pamoja na Sila, watu wawili waliokuwa viongozi miongoni mwa ndugu. 23 Wakatumwa na barua ifuatayo:
Sisi mitume na wazee, ndugu zenu.
Kwa waumini wa Mataifa mlio Antiokia, Siria na Kilikia.
Salamu.
24 Tumesikia kwamba kuna baadhi ya watu waliokuja huko kutoka kwetu bila ruhusa yetu na kuwasumbua, wakiyataabisha mawazo yenu. 25 Hivyo tumekubaliana wote kuwachagua baadhi ya watu na kuwatuma kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo, 26 watu ambao wamehatarisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Isa Al-Masihi. 27 Kwa hiyo tunawatuma Yuda na Sila, kuthibitisha kwa maneno ya mdomo mambo haya tunayowaandikia. 28 Kwa maana imempendeza Roho wa Mungu na sisi tusiwatwike mzigo wowote mkubwa zaidi ya mambo haya yafuatayo ambayo ni ya lazima: 29 Kwamba mjiepushe na vyakula vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, au kula nyama ya mnyama aliyenyongwa, na mjiepushe na uasherati. Mkiyaepuka mambo haya, mtakuwa mmefanya vyema.
Kwaherini.
30 Hivyo wakaagwa, wakashuka kwenda Antiokia. Baada ya kulikusanya kundi la waumini pamoja, wakawapa ile barua. 31 Baada ya hao watu kuisoma, wakafurahishwa sana kwa ujumbe wake wa kutia moyo. 32 Yuda na Sila, ambao wenyewe walikuwa manabii, wakanena maneno mengi ya kuwatia moyo na kuwajenga waumini katika imani. 33 Baada ya kukaa huko Antiokia kwa muda, wakaagwa kwa amani na wale ndugu ili waende kwa wale waliowatuma. [ 34 Lakini Sila bado akaendelea kukaa huko.]Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya. 35 Lakini Paulo na Barnaba walibaki Antiokia ambako wao pamoja na wengine wengi walifundisha na kuhubiri neno la Bwana Isa.
Safari ya pili ya Paulo kueneza Injili
(Matendo 15:36–18:22)
Paulo na Barnaba wagawanyika
36 Baada ya muda, Paulo akamwambia Barnaba, “Turudi tukawatembelee ndugu katika miji yote tuliyohubiri neno la Bwana Isa tuone jinsi wanavyoendelea.” 37 Barnaba alitaka wamchukue Yohana aitwaye Marko waende naye. 38 Lakini Paulo aliona si vyema kwa sababu aliwahi kuwaacha walipokuwa huko Pamfilia, hakutaka kuendelea kufanya kazi naye. 39 Pakatokea ubishi mkali kati ya Paulo na Barnaba kuhusu jambo hili, hivyo wakagawanyika. Barnaba akamchukua Yohana Marko wakasafiri baharini kwenda Kipro. 40 Lakini Paulo akamchagua Sila na akaondoka baada ya ndugu kuwatakia neema ya Bwana Isa. 41 Akapitia Siria na Kilikia, akiimarisha makundi ya waumini ya huko.

*15:5 Kundi la kidini la Wayahudi; walifuata Torati kwa dhati, hasa maagizo kuhusu utakaso. Pia waliamini katika malaika, ufufuo wa wafu, na kuja kwa Masihi ambaye atarejesha ufalme wa Daudi na ukuu wa taifa la Israeli.

15:21 Nyumba za ibada na mafunzo.

15:34 Maandiko mengine ya kale hayana maneno haya.