19
Paulo huko Efeso
Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa, akawauliza, “Je, mlipokea Roho wa Mungu mlipoamini?”
Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho wa Mungu.” Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yahya.”
Paulo akasema, “Ubatizo wa Yahya ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani Isa.” Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Isa. Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu wa Mungu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri. Walikuwa wapatao wanaume kumi na wawili.
Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya ufalme wa Mungu. Lakini baadhi yao wakakaidi; walikataa kuamini, na wakakashifu Njia Ile*Njia Ile maana yake wafuasi wa Isa (Yohana 14:6; Matendo 24:14); walichukuliwa kuwa dhehebu la dini ya Wayahudi. hadharani. Basi Paulo aliachana nao. Akaenda na wanafunzi wale, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano. 10 Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko jimbo la Asia wakawa wamesikia neno la Bwana Isa.
Wana wa Skewa wajaribu kutoa pepo mchafu
11 Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kupitia kwa Paulo, 12 hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.
13 Baadhi ya Wayahudi waliotangatanga wakitoa pepo wachafu wakajaribu kutumia jina la Bwana Isa kwa wale wenye pepo, wakisema, “Kwa jina la Isa, yule anayehubiriwa na Paulo, nakuamuru utoke.” 14 Wana saba wa Skewa, Myahudi aliyekuwa kiongozi wa makuhani, walikuwa wanafanya hivyo. 15 Siku moja pepo mchafu akawajibu, “Isa namjua na Paulo pia namjua, lakini ninyi ni nani?” 16 Kisha yule mtu aliyekuwa na pepo mchafu akawarukia, akawashambulia vikali, akawashinda nguvu wote, wakatoka ndani ya ile nyumba wakikimbia wakiwa uchi na wenye majeraha.
17 Habari hii ikajulikana kwa Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawajaa wote, nalo jina la Bwana Isa likaheshimiwa sana. 18 Wengi wa wale waliokuwa wameamini wakati huu wakaja na kutubu waziwazi kuhusu matendo yao maovu. 19 Idadi kubwa ya wale waliofanya mambo ya uganga wakaleta vitabu vyao na kuviteketeza kwa moto hadharani. Walipofanya hesabu ya thamani ya vitabu vilivyoteketezwa ilikuwa drakma elfu hamsiniDrakma moja ilikuwa na thamani sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja. za fedha. 20 Hivyo neno la Bwana Isa likaenea sana na kuwa na nguvu.
21 Baada ya mambo haya kutukia, Paulo akakusudia rohoni kwenda Yerusalemu kupitia Makedonia na Akaya. Akasema, “Baada ya kufika huko, yanipasa pia kwenda Rumi.” 22 Hivyo akatuma wasaidizi wake wawili, Timotheo na Erasto, waende Makedonia, wakati yeye mwenyewe alibaki kwa muda kidogo huko jimbo la Asia.
Ghasia huko Efeso
23 Wakati huo huo pakatokea dhiki kubwa kwa sababu ya Njia Ile. 24 Mtu mmoja jina lake Demetrio mfua fedha aliyekuwa akitengeneza vinyago vya fedha vya Artemi na kuwapatia mafundi wake biashara kubwa, 25 aliwaita pamoja watu wengine waliofanya kazi ya ufundi kama yake na kusema, “Enyi watu, mnajua ya kuwa utajiri wetu unatokana na biashara hii! 26 Mnaona na kusikia jinsi huyu Paulo amewashawishi na kuwapoteza watu wengi hapa Efeso na karibu jimbo lote la Asia. Anasema kwamba miungu iliyofanywa kwa mikono ya wanadamu si miungu hata kidogo. 27 Kwa hiyo kuna hatari si kwa kazi yetu kudharauliwa tu, bali pia hata hekalu la mungu wa kike Artemi aliye mkuu, anayeabudiwa jimbo lote la Asia na ulimwengu wote, litakuwa limepokonywa fahari yake ya kiungu.”
28 Waliposikia maneno haya, wakaghadhibika, wakaanza kupiga kelele wakisema, “Artemi wa Waefeso ni mkuu!” 29 Mara mji wote ukajaa ghasia. Watu wakawakamata Gayo na Aristarko, wenyeji wa Makedonia waliokuwa wakisafiri na Paulo, wakakimbilia nao katika ukumbi wa maonesho. 30 Paulo akataka kuingia katikati ya umati, lakini wanafunzi hawakumruhusu. 31 Hata baadhi ya viongozi wa sehemu ile, waliokuwa rafiki zake Paulo, wakatuma watu wakitamani asiingie katika ule ukumbi wa maonesho.
32 Umati wa watu walikuwa na taharuki. Walikuwa wakipiga kelele, hawa wakisema hili na wengine lile. Idadi kubwa ya watu hawakujua hata ni kwa nini walikuwa wamekusanyika huko. 33 Wayahudi wakamsukumia Iskanda mbele na baadhi ya watu kwenye umati ule wakampa maelekezo. Akawaashiria kwa mkono ili watulie aweze kujitetea mbele ya watu. 34 Lakini walipotambua kwamba alikuwa Myahudi, wote wakapiga kelele kwa sauti moja kwa karibu muda wa saa mbili, wakisema, “Artemi wa Efeso ni mkuu!”
35 Baadaye karani wa mji akanyamazisha umati ule wa watu na kusema, “Enyi watu wa Efeso, je, ulimwengu wote haujui ya kuwa mji wa Efeso ndio unaotunza hekalu la Artemi aliye mkuu na ile sanamu yake iliyoanguka kutoka mbinguni? 36 Kwa hiyo, kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, inawapasa mnyamaze na wala msifanye lolote kwa haraka. 37 Kwa kuwa mmewaleta hawa watu hapa, ingawa hawajaiba hekaluni wala kumkufuru huyu mungu wetu wa kike. 38 Basi, ikiwa Demetrio na mafundi wenzake wana mashtaka dhidi ya mtu yeyote, mahakama ziko wazi na wasaidizi wa mwakilishi wa mtawala. Wanaweza kufungua mashtaka. 39 Lakini kama kuna jambo jingine lolote zaidi mnalotaka kulileta, itabidi lisuluhishwe katika kusanyiko halali. 40 Kama ilivyo sasa, tuko hatarini kushtakiwa kwa kufanya ghasia kwa sababu ya tukio la leo. Kwa kuwa hakuna sababu tutakayoweza kutoa kuhalalisha msukosuko huu.” 41 Baada ya kusema haya akavunja mkutano.

*19:9 Njia Ile maana yake wafuasi wa Isa (Yohana 14:6; Matendo 24:14); walichukuliwa kuwa dhehebu la dini ya Wayahudi.

19:19 Drakma moja ilikuwa na thamani sawa na mshahara wa kibarua wa siku moja.