3
Mashahidi waitwa dhidi ya Israeli 
  1 Sikilizeni neno hili alilosema Mwenyezi Mungu dhidi yenu, enyi watu wa Israeli, dhidi ya jamaa nzima niliowapandisha toka Misri:   
 2 “Ni ninyi tu niliowachagua  
kati ya jamaa zote za dunia;  
kwa hiyo nitawaadhibu  
kwa ajili ya dhambi zenu zote.”   
 3 Je, watu wawili hutembea pamoja  
wasipokubaliana kufanya hivyo?   
 4 Je, simba hunguruma katika kichaka  
wakati hana mawindo?  
Aweza kuvuma katika pango  
wakati ambao hajakamata chochote?   
 5 Je, ndege aweza kuanguka kwenye mtego ulio ardhini  
ambapo hajategewa chambo?  
Je, mtego unaweza kufyatuka toka ardhini  
wakati hakuna chochote cha kunasa?   
 6 Je, tarumbeta inapopigwa mjini kujulisha hatari,  
watu hawatetemeki?  
Mji unapopatwa na maafa,  
je, si Mwenyezi Mungu amesababisha?   
 7 Hakika Bwana Mungu Mwenyezi hatafanya neno lolote  
bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.   
 8 Simba amenguruma:  
je, ni nani ambaye hataogopa?  
Bwana Mungu Mwenyezi ametamka:  
je, ni nani awezaye kukosa kutoa unabii?   
 9 Tangazeni katika ngome za Ashdodi  
na katika ngome za Misri:  
“Kusanyikeni juu ya milima ya Samaria;  
angalieni wingi wa wasiwasi ulio ndani yake,  
na uonevu ulio miongoni mwa watu wake.”   
 10 Mwenyezi Mungu asema: “Hawajui kutenda lililo jema,  
wale ambao hujilundikia nyara  
na vitu vilivyotekwa katika ngome zao.”   
 11 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:  
“Adui ataizingira nchi;  
ataangusha chini ngome zenu  
na kuteka nyara maboma yenu.”   
 12 Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu:  
“Kama vile mchungaji aokoavyo kinywani mwa simba  
vipande viwili tu vya mfupa wa mguu  
au kipande cha sikio,  
hivyo ndivyo Waisraeli watakavyookolewa,  
wale wanaokaa Samaria  
kwenye kingo za vitanda vyao,  
na katika Dameski  
kwenye viti vyao vya fahari.”   
 13 “Sikia hili na ushuhudie dhidi ya nyumba ya Yakobo,” asema Bwana, yeye Bwana Mwenyezi Mungu, Mungu wa majeshi ya mbinguni.   
 14 “Siku nitakapomwadhibu Israeli kwa sababu ya dhambi zake,  
nitaharibu madhabahu za Betheli;  
pembe za madhabahu zitakatiliwa mbali  
na kuanguka chini.   
 15 Nitabomoa nyumba ya wakati wa masika,  
pamoja na nyumba ya wakati wa kiangazi;  
nyumba zilizonakshiwa kwa pembe za ndovu  
na majumba makubwa ya fahari yatabomolewa,”  
asema Mwenyezi Mungu.