14
Vyakula vilivyo najisi na vilivyo safi
(Walawi 11:1-47)
Ninyi ni watoto wa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Msijichanje ama kujinyoa upara kwenye paji la uso kwa ajili ya aliyekufa, kwa kuwa ninyi ni taifa takatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. Mwenyezi Mungu amewachagua ninyi kuwa taifa lake la pekee kutoka mataifa yote duniani.
Msile kitu chochote ambacho ni machukizo. Hawa ndio wanyama mtakaokula: ng’ombe, kondoo, mbuzi, kulungu, paa, kongoni, paa mweupe, mbuzi-mwitu, pofu na kondoo wa mlimani. Mnaweza kumla mnyama yeyote mwenye kwato zilizogawanyika mara mbili, pia yule anayecheua. Hata hivyo, miongoni mwa wale wanaocheua au wale walio na kwato zilizogawanyika kamwe msile ngamia, sungura na pelele. Iwapo wanacheua, lakini hawana kwato zilizogawanyika; ni najisi kwenu. Nguruwe pia ni najisi; ingawa ana kwato zilizogawanyika, hacheui. Msile nyama yake wala kugusa mzoga wake.
Katika viumbe hai vyote viishivyo kwenye maji, mnaweza kula yeyote aliye na mapezi na magamba. 10 Lakini chochote kisicho na mapezi na magamba msile; kwenu ni najisi.
11 Mnaweza kula ndege yeyote aliye safi. 12 Lakini wafuatao msiwale: tai, furukombe, kipungu, 13 kengewa mwekundu, kengewa mweusi, mwewe wa aina yoyote, 14 kunguru wa aina yoyote, 15 mbuni, kiruka-njia, dudumizi, kipanga wa aina yoyote, 16 bundi, mumbi, bundi mkubwa, 17 mwari, nderi, mnandi, 18 korongo, koikoi wa aina yoyote, hudihudi na popo.
19 Wadudu wote warukao kwa makundi ni najisi kwenu, msiwale. 20 Lakini viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi mwaweza kula.
21 Msile kitu chochote mtakachokuta kimekufa. Mnaweza kumpa mgeni yeyote anayeishi katika mojawapo ya miji yenu, naye anaweza kula au mnaweza kumuuzia mtu wa nchi nyingine. Lakini ninyi ni watu watakatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
Msitokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.
Zaka
22 Hakikisheni mmetenga sehemu ya kumi ya mazao yote ya mashamba yenu kila mwaka. 23 Mtakula zaka za nafaka yenu, divai mpya, mafuta na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng’ombe na ya kondoo na mbuzi mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, pale mahali atakapopachagua kama maskani kwa ajili ya Jina lake, ili mpate kujifunza kumheshimu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, daima. 24 Lakini ikiwa mahali pale ni mbali sana nanyi mmebarikiwa na Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na hamwezi kubeba zaka yenu (kwa sababu mahali pale Mwenyezi Mungu atakapopachagua kuliweka Jina lake ni mbali sana), 25 basi badilisheni zaka yenu kuwa fedha, mkaichukue hiyo fedha mwende nayo mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapopachagua. 26 Tumieni hiyo fedha kununua chochote ukitakacho: ng’ombe, kondoo, divai au kinywaji chochote chenye chachu au chochote mnachotaka. Kisha ninyi na watu wa nyumbani mwenu mtaila mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, na kufurahi. 27 Msiache kuwajali Walawi wanaoishi katika miji yenu, kwa kuwa hao hawana shamba wala urithi wao wenyewe.
28 Mwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu, 29 ili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.