18
Sadaka kwa makuhani na Walawi
Makuhani ambao ni Walawi, yaani kabila lote la Lawi, hawatakuwa na mgawo wala urithi pamoja na Israeli. Wataishi kwa sadaka zitolewazo kwa ajili ya Mwenyezi Mungu za kuteketezwa kwa moto, kwa maana huo ndio urithi wao. Hawatakuwa na urithi miongoni mwa ndugu zao; Mwenyezi Mungu ndiye urithi wao, kama alivyowaahidi.
Hili ndilo fungu la makuhani kutoka kwa watu watakaotoa dhabihu ya fahali au kondoo: mguu wa mbele, mataya na matumbo. Mtawapa malimbuko ya nafaka zenu, divai mpya, mafuta na sufu ya kwanza kutoka manyoya ya kondoo wenu, kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewachagua pamoja na wazao wao kutoka makabila yenu kusimama na kuhudumu katika jina la Mwenyezi Mungu siku zote.
Ikiwa Mlawi atahama kutoka mojawapo ya miji yenu popote katika Israeli ambapo anaishi, akaja kwa moyo wote mahali Mwenyezi Mungu atakapopachagua, anaweza akahudumu katika jina la Mwenyezi Mungu, Mungu wake, kama Walawi wenzake wote wanaohudumu hapo mbele za Mwenyezi Mungu. Atashiriki sawa katika mafao yao, hata kama amepokea fedha kutoka mauzo ya mali ya jamaa yake.
Matendo ya machukizo
Mtakapoingia katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa, msijifunze kuiga njia za machukizo za mataifa ya huko. 10 Asionekane mtu yeyote miongoni mwenu ampitishaye mwanawe au binti yake katika moto, atakayefanya uaguzi, ulozi, anayetabiri nyakati, anayejishughulisha na uchawi, 11 wala arogaye kwa kupiga mafundo, wala mwaguzi au anayeabudu mizimu, wala awaombaye wafu. 12 Mtu yeyote afanyaye mambo haya ni chukizo kwa Mwenyezi Mungu, tena ni kwa sababu ya matendo haya ya kuchukiza wayafanyayo ndiyo maana Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atayafukuza mataifa hayo mbele yenu. 13 Kamwe msilaumiwe mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
Nabii
14 Mataifa mtakayowafukuza husikiliza wale wafanyao ulozi na uaguzi. Lakini ninyi, Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, hajawaruhusu kufanya hivyo. 15 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atawainulia nabii kama mimi kutoka miongoni mwa ndugu zenu wenyewe. Msikilizeni yeye. 16 Kwa kuwa hivi ndivyo mlivyomwomba Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kule Horebu siku ile ya kusanyiko, wakati mliposema, “Na tusiisikie sauti ya Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, wala kuuona moto huu mkubwa tena, ama sivyo tutakufa.”
17 Mwenyezi Mungu akaniambia: “Wanachosema ni vyema. 18 Nitawainulia nabii kama wewe kutoka miongoni mwa ndugu zao; nitaweka maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia kila kitu nitakachomwamuru. 19 Kama mtu yeyote hatasikiliza maneno yangu ambayo huyo nabii atayasema kwa Jina langu, mimi mwenyewe nitamwajibisha. 20 Lakini nabii ambaye atathubutu kusema kwa Jina langu kitu chochote ambacho sikumwamuru akiseme, au nabii ambaye husema kwa jina la miungu mingine ni lazima auawe.”
21 Mnaweza kuulizana wenyewe, “Tutawezaje kujua wakati ujumbe haukusemwa na Mwenyezi Mungu?” 22 Ikiwa kile nabii anachotangaza kwa jina la Mwenyezi Mungu hakikutendeka au kutimia, huo ni ujumbe ambao Mwenyezi Mungu hakusema. Nabii huyo amesema kwa ujuaji. Msimwogope huyo.