20
Kwenda vitani
Mtakapoenda vitani kupigana na adui zenu na mkaona farasi na magari ya vita na jeshi kubwa kuliko lenu, msiwaogope, kwa sababu Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, aliyewatoa kutoka Misri, atakuwa pamoja nanyi. Mtakapokaribia kwenda vitani, kuhani atakuja mbele na kuhutubia jeshi. Atasema: “Sikia, ee Israeli, leo unaenda vitani kupigana na adui zako. Usife moyo wala usiogope, usitishwe wala usitiwe hofu mbele yao. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, ndiye huenda pamoja nanyi kuwapigania dhidi ya adui zenu na kuwapatia ushindi.”
Maafisa wataliambia jeshi: “Je, kuna yeyote aliyejenga nyumba mpya ambayo haijawekwa wakfu? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akaiweka wakfu. Je, kuna yeyote aliyepanda shamba la mizabibu na hajaanza kulifurahia? Yeye na arudi nyumbani, au sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akalifurahia. Je, kuna yeyote aliyeposa mwanamke na hajamwoa? Yeye na arudi nyumbani, ama sivyo anaweza kufa vitani na mtu mwingine akamwoa.” Kisha maafisa wataongeza haya, “Je, kuna mtu anayeogopa ama kufa moyo? Yeye na arudi nyumbani ili ndugu zake nao wasije wakafa moyo pia.” Maafisa watakapomaliza kuzungumza na jeshi, watawateua wakuu wa vikosi.
10 Mtakapoenda kushambulia mji, wapeni watu wake masharti ya amani. 11 Wakikubali na kuwafungulia malango yao, watu wake wote watakuwa watumwa wa kufanya kazi ngumu, na watawatumikia ninyi. 12 Ikiwa watakataa kufanya mapatano ya amani na wakiwaingiza katika vita, basi mtauzingira mji huo. 13 Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, atakapouweka mji huo mkononi mwenu, waueni kwa upanga wanaume wote waliomo. 14 Kwa upande wa wanawake, watoto, mifugo na kila kitu kingine chochote ndani ya huo mji, mnaweza kuvichukua kama nyara kwa ajili yenu. Nanyi mnaweza kuzitumia hizo nyara ambazo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa kutoka kwa adui zenu. 15 Hivi ndivyo mtakavyofanya kwa miji yote iliyo mbali nanyi, ambayo haimilikiwi na mataifa ya karibu.
16 Hata hivyo, katika miji ya mataifa ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi, msiache kitu chochote hai kinachopumua. 17 Waangamizeni kabisa Wahiti, Waamori, Wakanaani, Waperizi, Wahivi na Wayebusi, kama Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alivyowaamuru. 18 La sivyo, watawafundisha kufuata mambo yote ya machukizo wanayofanya wakiabudu miungu yao, nanyi mtatenda dhambi dhidi ya Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.
19 Mtakapouzunguka mji kwa vita kwa muda mrefu, mkipigana dhidi yake ili kuuteka, msiharibu miti yake kwa kuikata kwa shoka, kwa sababu mtaweza kula matunda yake. Hivyo msiikate. Je, miti hiyo ya mashambani ni watu, hata muizingire? 20 Hata hivyo, mnaweza kuikata miti isiyo ya matunda na kuitumia kuuzingira, hadi mji unaofanya vita na ninyi utakapoanguka.