24
Sheria kuhusu ndoa na talaka
Mtu akimwoa mke na akamchukia kwa sababu ya kuona jambo baya kwake, inawezekana akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani mwake. Baada ya mwanamke huyo kuondoka kwake, inawezekana akaolewa na mtu mwingine. Mume wake wa pili akichukizwa naye, akamwandikia hati ya talaka, akampa na kumfukuza kutoka nyumbani mwake, au huyo mume wa pili akifa, basi yule mume wake wa kwanza, ambaye alimpa talaka, haruhusiwi kumwoa tena baada ya mwanamke huyo kuwa najisi. Hayo yatakuwa machukizo machoni pa Mwenyezi Mungu. Usilete dhambi juu ya nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakupa kama urithi.
Kama mtu ameoa karibuni, kamwe asipelekwe vitani au kupewa wajibu mwingine wowote. Kwa mwaka mmoja atakuwa huru kubaki nyumbani ili amfurahishe mke aliyemwoa.
Sheria nyingine
Usitoe jozi ya mawe ya kusagia, hata ikiwa lile la juu, kuweka rehani kwa ajili ya deni, kwa sababu itakuwa ni kuweka uhai wa mtu kama dhamana.
Kama mtu akikamatwa akiiba yeyote miongoni mwa ndugu zake wa Waisraeli na kumtenda kama mtumwa au akimuuza, mwizi huyo ni lazima auawe. Nawe utaondoa uovu kutoka miongoni mwenu.
Pakitokea magonjwa ya ngozi ya kuambukiza, mwe waangalifu sana kufanya sawasawa na maagizo ya makuhani, ambao ni Walawi. Ni lazima mfuate kwa uangalifu yale niliyowaamuru. Kumbukeni kile Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, alichomfanyia Miriamu njiani baada ya ninyi kutoka Misri.
10 Unapomkopesha jirani yako chochote, usiingie nyumbani mwake kutwaa kile anachokitoa kama rehani. 11 Ukae nje na umwache huyo mtu uliyemkopesha akuletee hiyo rehani. 12 Ikiwa mtu huyo ni maskini, usiende kulala ukiwa na hiyo rehani yake katika milki yako. 13 Rudisha vazi lake kabla ya machweo ya jua ili apate kulilalia. Kisha atakushukuru na kitaonekana kama kitendo cha haki mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako.
14 Usimwonee mtu maskini na mhitaji ambaye umemwajiri, akiwa ni nduguyo Mwisraeli au mgeni anayeishi katika mojawapo ya miji yenu. 15 Mlipe ujira wake kila siku kabla ya jua kutua, kwa sababu yeye ni maskini na anautegemea ujira huo. La sivyo, anaweza kumlilia Mwenyezi Mungu dhidi yako, nawe ukapata hatia ya dhambi.
16 Baba wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mmoja atakufa kwa ajili ya dhambi yake mwenyewe.
17 Usipotoshe hukumu ya mgeni au yatima, au kuchukua vazi la mjane kama rehani. 18 Kumbukeni kwamba mlikuwa watumwa huko Misri, naye Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, akawakomboa kutoka huko. Hii ndiyo sababu ninawaamuru kutenda hili.
19 Unapovuna shamba lako na ukasahau mganda, usirudi kuuchukua. Acha kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane, ili Mwenyezi Mungu, Mungu wako, aweze kukubariki wewe katika kazi zote za mikono yako. 20 Unapovuna zeituni kutoka miti yako, usirudie matawi mara ya pili. Acha kilichobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 21 Unapochuma zabibu katika shamba lako la mizabibu usirudie tena. Acha zinazobaki kwa ajili ya mgeni, yatima na mjane. 22 Kumbuka kwamba mlikuwa watumwa katika nchi ya Misri. Ndiyo sababu ninawaamuru kufanya hili.