26
Malimbuko na zaka
1 Mtakapokuwa mmeingia nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa kama urithi na mtakapokuwa mmeimiliki na kukaa ndani yake, 2 chukueni baadhi ya mavuno ya kwanza ya yale yote mtakayozalisha kutoka udongo wa nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, anawapa na mweke kwenye kapu. Kisha uende mahali Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakapopachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake, 3 na umwambie kuhani atakayekuwepo wakati huo, “Ninatangaza leo kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwamba nimekuja katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu aliwaapia baba zetu kwamba atatupa.” 4 Kuhani atapokea lile kapu mikononi mwako na kuliweka chini mbele ya madhabahu ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako. 5 Kisha utatangaza mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako: “Baba yangu alikuwa Mwaramu aliyekuwa anatangatanga, akaenda Misri pamoja na watu wachache, akaishi huko hadi akawa taifa kubwa, lenye nguvu na watu wengi. 6 Lakini Wamisri walituonea na kututaabisha, wakitufanyisha kazi ngumu. 7 Kisha tulimlilia Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zetu, naye Mwenyezi Mungu akasikia sauti yetu na akaona huzuni yetu, taabu yetu na mateso yetu. 8 Kwa hiyo Mwenyezi Mungu akatutoa nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, pamoja na utisho mkuu, ishara za miujiza na maajabu. 9 Akatuleta mahali hapa akatupatia nchi hii, nchi inayotiririka maziwa na asali; 10 nami sasa ninaleta malimbuko ya ardhi ambayo wewe, Ee Mwenyezi Mungu, umenipa.” Weka kapu mbele za Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na usujudu mbele zake. 11 Kisha wewe pamoja na Walawi na wageni wote walio miongoni mwenu mtafurahi katika vitu vyote vizuri ambavyo Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, amewapa pamoja na wa nyumbani mwenu.
12 Utakapokuwa umeshatoa zaka zote za mazao yako katika mwaka wa tatu, ambao ni mwaka wa zaka, utampa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, ili waweze kula katika miji yenu na kushiba. 13 Kisha umwambie Mwenyezi Mungu, Mungu wako: “Nimeondoa katika nyumba yangu ile sehemu iliyowekwa wakfu na nimempa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, kulingana na yote uliyoamuru. Sijazihalifu amri zako wala kusahau hata mojawapo. 14 Sijala sehemu iliyowekwa wakfu wakati nilipokuwa nikiomboleza, wala sijaondoa mojawapo wakati nilipokuwa najisi, wala sijatoa sehemu yake yoyote kwa wafu. Nimemtii Mwenyezi Mungu, Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoniamuru. 15 Angalia chini kutoka mbinguni, maskani yako takatifu, uwabariki watu wako Israeli pamoja na nchi uliyotupatia kama ulivyoahidi kwa kiapo kwa baba zetu, nchi inayotiririka maziwa na asali.”
Fuata maagizo ya Mwenyezi Mungu
16 Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakuagiza leo kufuata amri hizi na sheria; zingatia kwa makini kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. 17 Umetangaza leo kwamba Mwenyezi Mungu ndiye Mungu wako na kwamba utafuata njia zake, kwamba utayashika maagizo yake, amri zake na sheria zake nawe utamtii. 18 Naye Mwenyezi Mungu ametangaza leo kwamba ninyi ni taifa lake, hazina yake ya pekee kama alivyoahidi, ili mpate kuyashika maagizo yake yote. 19 Ametangaza kwamba atawaweka juu kuliko mataifa mengine aliyoyafanya katika sifa, kuwa fahari na heshima, na kwamba mtakuwa taifa takatifu kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wenu, kama alivyoahidi.