28
Baraka za utiifu
(Walawi 26:3-13; Kumbukumbu 7:12-24)
Ukimtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa ukamilifu na kufuata amri zake zote ninazokupa leo kwa makini, Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakuweka juu ya mataifa yote katika dunia. Baraka hizi zote zitakuja juu yako na kukupata, kama ukimtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako:
Utabarikiwa mjini na utabarikiwa mashambani.
Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na mazao ya nchi yako na mifugo wako wachanga, yaani ndama wa makundi yako ya ng’ombe, na wana-kondoo wa makundi yako.
Kapu lako na vyombo vyako vya kukandia vitabarikiwa.
Utabarikiwa uingiapo na utabarikiwa utokapo.
Mwenyezi Mungu atasababisha adui wainukao dhidi yako kushindwa mbele yako. Watakujia kwa njia moja lakini watakimbia mbele yako kwa njia saba.
Mwenyezi Mungu ataagiza baraka juu ya ghala zako na juu ya kila kitu utakachogusa kwa mkono wako. Mwenyezi Mungu, Mungu wako, atakubariki katika nchi anayokupa.
Mwenyezi Mungu atakufanya kuwa taifa lake takatifu, kama alivyokuahidi kwa kiapo, ukishika maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kwenda katika njia zake. 10 Kisha mataifa yote ya dunia wataona kuwa unaitwa kwa jina la Mwenyezi Mungu, nao watakuogopa. 11 Mwenyezi Mungu atakupa kustawi kwa wingi, katika tunda la uzao wa tumbo lako, katika wanyama wachanga wa mifugo yako na katika mazao ya ardhi yako, katika nchi aliyowaapia baba zako kukupa wewe.
12 Mwenyezi Mungu atafungua mbingu, ghala zake za baraka, kukupa mvua kwa majira yake na kubariki kazi zako zote za mikono yako. Utakopesha mataifa mengi lakini hutakopa kwa yeyote. 13 Mwenyezi Mungu atakufanya kichwa, wala si mkia. Kama utazingatia maagizo ya Mwenyezi Mungu, Mungu wako, ninayokupa siku hii ya leo na kuyafuata kwa makini, daima utakuwa juu, kamwe hutakuwa chini. 14 Usihalifu amri zangu zozote ninazokupa leo, kwa kwenda kuume au kushoto, kwa kufuata miungu mingine na kuitumikia.
Laana kwa kutokutii
(Walawi 26:14-46)
15 Lakini kama hutamtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika kwa makini amri zake zote na maagizo ninayokupa leo, laana hizi zote zitakuja juu yako na kukupata:
16 Utalaaniwa mjini na utalaaniwa mashambani.
17 Kapu lako na chombo chako cha kukandia kitalaaniwa.
18 Uzao wa tumbo lako utalaaniwa, mazao ya ardhi yako, ndama wa makundi yako ya ng’ombe na wana-kondoo wa makundi yako.
19 Utalaaniwa uingiapo na utokapo.
20 Mwenyezi Mungu ataleta laana juu yako, fadhaa na kukaripiwa katika kila kitu unachokigusa kwa mkono wako, hadi uwe umeharibiwa na kuangamizwa ghafula kwa ajili ya maovu uliyoyafanya kwa kumwacha yeye. 21 Mwenyezi Mungu atakupiga kwa magonjwa hadi akuangamize kutoka nchi unayoingia kuimiliki. 22 Mwenyezi Mungu atakupiga kwa magonjwa ya kudhoofisha, kwa homa na kuwashwa, hari na kwa ukame, kutu na kuwa na uchungu ambavyo vitakupiga hadi uangamie.
23 Anga juu yako itakuwa shaba, na ardhi chini yako itakuwa chuma. 24 Mwenyezi Mungu atafanya mvua ya nchi yako kuwa mavumbi na mchanga; vitakujia kutoka angani hadi uangamie.
25 Mwenyezi Mungu atakufanya ushindwe mbele ya adui zako. Utawajia kwa njia moja lakini utawakimbia mbele yao kwa njia saba, nawe utakuwa kitu cha kuchukiza kwa falme zote za dunia. 26 Mizoga yenu itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwa na mtu yeyote wa kuwafukuza. 27 Mwenyezi Mungu atakupiga kwa majipu ya Misri na kwa vidonda vinavyotoa usaha na kuwashwa, ambavyo huwezi kuponywa. 28 Mwenyezi Mungu atakupiga kwa wazimu, upofu na kuchanganyikiwa kwa akili. 29 Adhuhuri utapapasapapasa kama kipofu gizani. Hutafanikiwa katika lolote ufanyalo; siku baada ya siku utadhulumiwa na kunyang’anywa, wala hakuna yeyote atakayekuokoa.
30 Utaposa mke, lakini mtu mwingine atakutana naye kimwili. Utajenga nyumba, lakini hutaishi ndani yake. Utapanda shamba la mizabibu, lakini hutakula matunda yake. 31 Ng’ombe wako atachinjwa mbele ya macho yako lakini hutakula nyama yake. Punda wako atachukuliwa kwa nguvu kutoka kwako wala hatarudishwa. Kondoo wako watapewa adui zako, wala hakuna mtu yeyote wa kuwaokoa. 32 Wanao wa kiume na wa kike watatolewa kwa mataifa mengine, nawe utayachosha macho yako ukiwatazamia siku baada ya siku, hutakuwa na nguvu kuinua mkono. 33 Taifa usilolijua watakula mazao ya nchi yako na taabu ya kazi yako, hutakuwa na chochote, bali kuonewa kikatili siku zako zote. 34 Vitu utakavyoviona kwa macho yako vitakufanya wazimu. 35 Mwenyezi Mungu atayapiga magoti yako na miguu yako kwa majipu yenye maumivu makali yasiyoponyeka, yakienea kutoka nyayo za miguu yako hadi utosini.
36 Mwenyezi Mungu atakupeleka wewe na mfalme uliyemweka juu yako uende kwenye taifa ambalo hukulijua wewe wala baba zako. Huko utaabudu miungu mingine, miungu ya miti na mawe. 37 Utakuwa kitu cha kuchukiza, tena kitu cha kudharauliwa na kudhihakiwa kwa mataifa yote huko Mwenyezi Mungu atakakokupeleka.
38 Utapanda mbegu nyingi katika shamba lakini utavuna haba, kwa sababu nzige watazila. 39 Utapanda mashamba ya mizabibu na kuyapalilia, lakini hutakunywa divai yake wala hutakusanya zabibu, kwa sababu wadudu watazila. 40 Utakuwa na mizeituni katika nchi yako yote, lakini hutatumia hayo mafuta yake, kwa sababu zeituni zitapukutika. 41 Utakuwa na wana wa kiume na wa kike, lakini hawatakuwa nawe, kwa sababu watachukuliwa mateka. 42 Makundi ya nzige yatavamia miti yako yote na mazao ya nchi yako.
43 Mgeni anayeishi miongoni mwako atazidi kuinuka juu yako, lakini wewe utaendelea kushuka chini zaidi. 44 Yeye atakukopesha, lakini wewe hutamkopesha. Yeye atakuwa kichwa, lakini wewe utakuwa mkia.
45 Laana hizi zote zitakuja juu yako. Zitakufuatia na kukupata hadi uangamizwe, kwa sababu hukumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake aliyokupa. 46 Zitakuwa ishara na ajabu kwako na kwa wazao wako milele. 47 Kwa sababu hukumtumikia Mwenyezi Mungu, Mungu wako, kwa furaha na kwa moyo wakati wa kufanikiwa kwako, 48 kwa hiyo katika njaa na kiu, katika uchi na umaskini wa kutisha, utawatumikia adui ambao Mwenyezi Mungu atawatuma dhidi yako. Yeye ataweka nira ya chuma shingoni mwako hadi amekwisha kukuangamiza.
49 Mwenyezi Mungu ataleta taifa dhidi yako kutoka mbali, kutoka miisho ya dunia, kama tai ashukavyo chini, taifa ambalo hutaijua lugha yake, 50 taifa lenye uso mkali lisilojali wazee wala kuwahurumia vijana. 51 Watakula wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako hadi umeangamia. Hawatakuachia nafaka, divai mpya au mafuta, wala ndama wowote wa kundi lako au wana-kondoo wa kundi lako hadi umekuwa magofu. 52 Nao wataizingira miji yote katika nchi yako, hata kuta ndefu za ngome ambazo unazitegemea zimeanguka. Watazingira miji yote katika nchi ambayo Mwenyezi Mungu, Mungu wako, anakupa.
53 Utakula uzao wa tumbo lako, nyama ya wana wako wa kiume na wa kike, ambao Mwenyezi Mungu, Mungu wako, amekupa, kwa sababu ya mateso yale adui zako watakayokuletea wakati wa kukuzingira. 54 Hata yule mtu muungwana sana na makini miongoni mwako hatakuwa na huruma kwa ndugu yake mwenyewe au kwa mke ampendaye au watoto wake waliosalia, 55 naye hatampa hata mmoja wao nyama ya watoto wake ambao anawala. Kwa kuwa hakuna kitu kingine kilichosalia kwake katika mazingirwa makali ambayo adui yako watakuletea kwa miji yako yote. 56 Mwanamke ambaye ni muungwana sana na makini miongoni mwako, yaani ambaye ni makini sana na muungwana kiasi kwamba asingethubutu kugusa ardhi kwa wayo wa mguu wake, yeye atakuwa mchoyo kwa mume ampendaye na mwanawe mwenyewe au binti yake, 57 kondoo wa nyuma kutoka tumbo lake na watoto anaowazaa. Kwa kuwa anakusudia kuwala kwa siri wakati wa kuzingirwa na katika taabu zile adui yako atazileta juu yako na miji yako.
58 Kama hutazingatia maneno yote ya sheria hii, ambayo yameandikwa katika kitabu hiki na kama hutalicha hili jina la fahari na la kutisha, yaani la Mwenyezi Mungu, Mungu wako, 59 Mwenyezi Mungu ataleta mapigo ya kutisha juu yako na kwa wazao wako, maafa makali na ya kudumu, magonjwa mazito na ya kudumu. 60 Atakuletea juu yako magonjwa yote ya Misri yale uliyoyaogopa, nayo yataambatana nawe. 61 Pia Mwenyezi Mungu atakuletea kila aina ya ugonjwa na maafa ambayo hayakuandikwa humu katika kitabu hiki cha sheria, hadi utakapokuwa umeangamizwa. 62 Ninyi ambao mlikuwa wengi kama nyota za angani mtaachwa wachache tu, kwa sababu hamkumtii Mwenyezi Mungu, Mungu wenu. 63 Kama ilivyompendeza Mwenyezi Mungu kuwafanya ninyi mstawi na kuongezeka kwa idadi, ndivyo itakavyompendeza kuwaharibu na kuwaangamiza ninyi. Mtang’olewa kutoka nchi mnayoiingia kuimiliki.
64 Kisha Mwenyezi Mungu atawatawanya miongoni mwa mataifa yote, kutoka mwisho mmoja wa dunia hadi mwingine. Huko mtaabudu miungu mingine, miungu ya miti na ya mawe, ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua. 65 Miongoni mwa mataifa hayo hamtapata amani, wala mahali pa kupumzisha wayo wa mguu wenu. Huko Mwenyezi Mungu atawapa mahangaiko ya mawazo, macho yaliyochoka kwa kungojea na moyo uliokata tamaa. 66 Utaishi katika mahangaiko siku zote, ukiwa umejaa hofu usiku na mchana, wala hutakuwa kamwe na uhakika wa maisha yako. 67 Asubuhi utasema hivi, “Laiti ingekuwa jioni!” Jioni utasema, “Laiti ingekuwa asubuhi,” kwa sababu ya hofu ile itakayojaza moyo wako na vitu vile macho yako yatakavyoviona. 68 Mwenyezi Mungu atawarudisha tena Misri kwa meli, safari niliyosema kamwe hamngeenda tena. Huko mtajiuza ninyi wenyewe kwa adui zenu kama watumwa wa kiume na wa kike, lakini hakuna yeyote atakayewanunua.