10
 1 Kama vile inzi waliokufa huacha harufu mbaya kwenye manukato,  
ndivyo upumbavu kidogo huzidi nguvu hekima na heshima.   
 2 Moyo wa mwenye hekima huelekea kuume,  
lakini moyo wa mpumbavu huelekea kushoto.   
 3 Hata anapotembea barabarani,  
mpumbavu hukosa ufahamu  
na kudhihirisha kwa kila mmoja  
jinsi alivyo mpumbavu.   
 4 Kama hasira ya mtawala ikiwaka dhidi yako,  
usiache mahali pako,  
utulivu huweza kuzuia makosa mengi.   
 5 Kuna ubaya niliouona chini ya jua,  
aina ya kosa litokalo kwa mtawala:   
 6 Wapumbavu kuwekwa kwenye nafasi nyingi za utawala,  
hali matajiri wanashika nafasi za chini.   
 7 Mimi nimeona watumwa wamepanda farasi,  
wakati wakuu wakitembea  
kwa miguu kama watumwa.   
 8 Yeye achimbaye shimo  
aweza kutumbukia ndani yake,  
yeyote abomoaye ukuta  
anaweza kuumwa na nyoka.   
 9 Yeyote apasuaye mawe  
inawezekana yakamuumiza,  
yeyote apasuaye magogo  
inawezekana yakamuumiza.   
 10 Kama shoka ni butu  
na halikunolewa,  
nguvu nyingi zinahitajika,  
lakini ustadi utaleta mafanikio.   
 11 Nyoka akiuma kabla ya kuchezeshwa,  
mchezeshaji hatahitajika tena.   
 12 Maneno yanayotoka kinywani mwa mtu mwenye hekima yana neema,  
bali mpumbavu huangamizwa  
na midomo yake mwenyewe.   
 13 Mwanzoni maneno yake ni upumbavu,  
mwishoni ni wazimu mbaya,   
 14 naye mpumbavu huzidisha maneno.  
Hakuna yeyote ajuaye linalokuja,  
ni nani awezaye kueleza ni jambo gani  
litakalotokea baada yake?   
 15 Kazi ya mpumbavu humchosha mwenyewe,  
hajui njia iendayo mjini.   
 16 Ole wako, ee nchi ambayo mfalme wako alikuwa mtumwa  
na ambayo wakuu wako hufanya karamu asubuhi.   
 17 Heri wewe, ee nchi ambayo mfalme wako  
ni wa uzao wenye kuheshimika,  
na ambayo wakuu wako hula chakula  
kwa wakati unaofaa:  
wao hula ili kupata nguvu  
na si kwa ajili ya ulevi.   
 18 Kama mtu ni mvivu, paa la nyumba huinama;  
kutokana na mikono milegevu, nyumba huvuja.   
 19 Karamu hufanywa kwa ajili ya kicheko,  
nao mvinyo hufurahisha maisha,  
lakini fedha ni jawabu la mambo yote.   
 20 Usimshutumu mfalme hata ikiwa ni katika mawazo yako,  
au kumlaani tajiri katika chumba chako cha kulala,  
kwa sababu ndege wa angani wanaweza kuchukua maneno yako,  
naye ndege anayeruka anaweza kutoa taarifa ya yale uliyosema.