2
Kufanywa hai ndani ya Al-Masihi
1 Ninyi mlikuwa wafu katika makosa na dhambi zenu, 2 ambazo mlizitenda mlipofuata njia za ulimwengu huu na za yule mtawala wa ufalme wa anga, yule roho atendaye kazi sasa ndani ya wale wasiotii. 3 Sisi sote pia tuliishi katikati yao hapo zamani, tukitimiza tamaa za asili yetu ya dhambi na kufuata tamaa zake na mawazo yake. Nasi kwa asili tulistahili ghadhabu, kama watu wengine wote. 4 Lakini Mungu kwa upendo wake mwingi kwetu sisi, ambaye ni mwingi wa rehema, 5 hata tulipokuwa wafu kwa ajili ya makosa yetu, alitufanya tuwe hai pamoja na Al-Masihi Isa, yaani mmeokolewa kwa neema. 6 Mungu alitufufua pamoja na Al-Masihi na kutuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho katika Al-Masihi Isa, 7 ili katika ulimwengu ujao apate kuonesha wingi wa neema yake isiyolinganishwa, iliyodhihirishwa kwetu kwa wema wake ndani ya Al-Masihi Isa. 8 Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kupitia kwa imani, nayo haikutokana na ninyi wenyewe. Hii ni zawadi kutoka kwa Mungu, 9 si kwa matendo, ili mtu yeyote asije akajisifu. 10 Kwa maana sisi ni kazi ya mikono ya Mungu, tulioumbwa katika Al-Masihi Isa, ili tupate kutenda matendo mema, ambayo Mungu alitangulia kuyaandaa tupate kuishi katika hayo.
Wamoja katika Al-Masihi
11 Kwa hiyo kumbukeni kwamba hapo awali ninyi ambao ni watu wa Mataifa kwa kuzaliwa na kuitwa “wasiotahiriwa” na wale wanaojiita “waliotahiriwa” (yaani tohara ifanyikayo katika mwili kwa mikono ya wanadamu), 12 kumbukeni kwamba wakati ule mlikuwa mbali na Al-Masihi, mkiwa mmetengwa kutoka jumuiya ya Israeli, na mkiwa wageni katika yale maagano ya ahadi, nanyi hamkuwa na tumaini wala Mungu duniani. 13 Lakini sasa katika Al-Masihi Isa, ninyi ambao hapo kwanza mlikuwa mbali na Mungu, sasa mmeletwa karibu kupitia kwa damu ya Al-Masihi.
14 Kwa maana yeye mwenyewe ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi tuliokuwa vikundi viwili tuwe kikundi kimoja kwa kuvunja kizuizi na kubomoa ule ukuta wa uadui uliokuwa kati yetu, 15 kwa kuibatilisha ile sheria pamoja na amri zake na maagizo yake alipoutoa mwili wake, ili apate kufanya ndani yake mtu mmoja mpya badala ya hao wawili, hivyo akifanya amani, 16 naye katika mwili huu mmoja awapatanishe wote wawili na Mungu kupitia msalaba, ili kwa huo msalaba akaangamiza uadui wao. 17 Alikuja na kuhubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na pia akahubiri amani kwao waliokuwa karibu. 18 Kwa maana kupitia kwake sisi sote tunaweza kumkaribia Baba katika Roho mmoja.
19 Hivyo basi, ninyi sasa si wageni tena na wapitaji, bali mmekuwa wenyeji pamoja na watakatifu na pia jamaa wa nyumbani mwake Mungu. 20 Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Al-Masihi Isa ndiye jiwe kuu la pembeni. 21 Ndani yake jengo lote limeshikamanishwa pamoja na kuinuliwa ili kuwa Hekalu takatifu katika Mwenyezi Mungu. 22 Katika yeye ninyi nanyi mnajengwa pamoja ili mpate kuwa makao ambayo Mungu anaishi ndani yake kupitia kwa Roho wake Mtakatifu.