5
Matofali bila nyasi
1 Baadaye Musa na Haruni wakaenda kwa Farao, wakamwambia, “Hili ndilo asemalo Mwenyezi Mungu, Mungu wa Israeli: ‘Waruhusu watu wangu waende, ili waweze kunifanyia sikukuu huko jangwani.’ ”
2 Farao akasema, “Huyo Mwenyezi Mungu ni nani, hata nimtii na kuruhusu Waisraeli waende? Simjui huyo Mwenyezi Mungu wala sitawaruhusu Waisraeli waende.”
3 Ndipo Musa na Haruni wakasema, “Mungu wa Waebrania amekutana nasi. Sasa turuhusu tuwe na safari ya siku tatu ya jangwani ili tukamtolee Mwenyezi Mungu, Mungu wetu, dhabihu, la sivyo aweza kutupiga sisi kwa tauni au kwa upanga.”
4 Lakini mfalme wa Misri akasema, “Mbona ninyi Musa na Haruni mnawaondoa watu kutoka kwenye kazi zao? Rudini kwenye kazi zenu!” 5 Kisha Farao akasema, “Tazama, sasa watu hawa ni wengi, nanyi mnawazuia kufanya kazi.”
6 Siku hiyo hiyo, Farao akatoa amri hii kwa viongozi wa watumwa na wasimamizi wa watu, akawaambia: 7 “Tangu sasa msiwape hawa watu nyasi za kutengenezea matofali; wakusanye nyasi zao wenyewe. 8 Lakini watakeni kutengeneza matofali kiasi kile kile cha mwanzo, kiwango kisipunguzwe. Wao ni wavivu, ndiyo sababu wanalia, wakisema, ‘Turuhusiwe twende kumtolea Mungu wetu dhabihu.’ 9 Fanyeni kazi kuwa ngumu zaidi kwa watu hao ili wakazane na kazi na kuacha kusikiliza uongo.”
10 Basi viongozi wa watumwa na wasimamizi wakaenda kuwaambia watu, “Hivi ndivyo Farao asemavyo: ‘Sitawapa nyasi tena. 11 Nendeni mkatafute nyasi wenyewe popote mnapoweza kuzipata, lakini kazi yenu haitapunguzwa hata kidogo.’ ” 12 Basi watu wakatawanyika kote nchini Misri kukusanya mabua ya kutumia badala ya nyasi. 13 Viongozi wa watumwa wakasisitiza wakisema, “Timizeni kazi mnayotakiwa kwa kila siku, kama wakati ule mlipokuwa mkipewa nyasi.” 14 Wasimamizi wa Waisraeli waliochaguliwa na viongozi wa watumwa wa Farao walipigwa na kuulizwa, “Kwa nini hamkutimiza kiwango chenu cha kutengeneza matofali jana na leo, kama mwanzoni?”
15 Ndipo wasimamizi wa Waisraeli wakaenda kumlilia Farao, wakisema: “Mbona umewatendea watumishi wako hivi? 16 Watumishi wako hawapewi nyasi, hata hivyo tumeambiwa, ‘Tengenezeni matofali!’ Watumishi wako wanapigwa, lakini kosa ni la watu wako wenyewe.”
17 Farao akasema, “Ninyi ni wavivu ndiyo sababu mnasema, ‘Turuhusu twende tukamtolee Mwenyezi Mungu dhabihu.’ 18 Sasa nendeni kazini. Hamtapewa nyasi zozote, nanyi ni lazima mtengeneze matofali.”
19 Wasimamizi wa Waisraeli walitambua kuwa wako taabani walipoambiwa, “Hamtakiwi kupunguza idadi ya matofali mliotakiwa kutengeneza kila siku.” 20 Walipoondoka kwa Farao, wakawakuta Musa na Haruni wakingojea kukutana nao, 21 wakawaambia Musa na Haruni, “Mwenyezi Mungu na awaangalie awahukumu ninyi! Mmetufanya tuwe chukizo kwa Farao na maafisa wake, nanyi mmeweka upanga mikononi mwao ili kutuua sisi.”
Mwenyezi Mungu anaahidi ukombozi
22 Musa akarudi kwa Mwenyezi Mungu na kumwambia, “Ee Bwana, mbona umewaletea watu hawa taabu? Kwa nini basi ukanituma mimi? 23 Tangu nilipokwenda kuzungumza na Farao kwa jina lako, amewaletea watu hawa taabu, nawe kamwe hujawakomboa watu wako.”