19
Waisraeli kwenye Mlima Sinai
Siku ya kwanza ya mwezi wa tatu baada ya Waisraeli kuondoka Misri, walifika Jangwa la Sinai siku hiyo hiyo. Baada ya kuondoka Refidimu, waliingia katika Jangwa la Sinai na Israeli wakapiga kambi pale jangwani mbele ya mlima.
Kisha Musa akakwea kwenda kwa Mungu, naye Mwenyezi Mungu akamwita kutoka ule mlima, akasema, “Hivi ndivyo utakavyosema na nyumba ya Yakobo na utakachowaambia Waisraeli: ‘Ninyi wenyewe mmeona nililofanya huko Misri, jinsi nilivyowabeba kwenye mabawa ya tai na kuwaleta kwangu. Sasa, mkinitii kikamilifu na kutunza agano langu, basi ninyi mtakuwa hazina yangu ya pekee miongoni mwa mataifa yote. Ijapokuwa dunia yote ni mali yangu, ninyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani na taifa takatifu.’ Haya ndio maneno utakayosema kwa Waisraeli.”
Kwa hiyo Musa akarudi, akawaita wazee wa watu na kuwaambia maneno yote ambayo Mwenyezi Mungu alikuwa amemwamuru ayaseme. Watu wote wakajibu kwa pamoja, “Tutafanya kila kitu Mwenyezi Mungu alichokisema.” Naye Musa akarudisha majibu yao kwa Mwenyezi Mungu.
Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nitakujia katika wingu zito, ili watu wanisikie nikinena nawe na kila mara waweke tumaini lao kwako.” Kisha Musa akamwambia Mwenyezi Mungu yale ambayo watu walikuwa wamesema.
10 Naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Nenda kwa watu ukawaweke wakfu leo na kesho. Waambie wafue nguo zao 11 na wawe tayari siku ya tatu, kwa sababu siku hiyo, Mwenyezi Mungu atashuka juu ya Mlima Sinai machoni pa watu wote. 12 Weka mipaka kuzunguka mlima kwa ajili ya watu, uwaambie, ‘Mwe waangalifu, msije mkapanda mlimani au kuugusa. Yeyote atakayeugusa mlima atauawa. 13 Hakika atapigwa mawe au kupigwa mishale; mkono wa mtu hautamgusa. Akiwa mwanadamu au mnyama, hataruhusiwa kuishi.’ Ila tu wakati baragumu itakapopigwa kwa mfululizo, ndipo watu wote watakapopanda mlimani.”
14 Baada ya Musa kushuka kutoka mlimani akawaendea watu na kuwaweka wakfu, wakafua nguo zao. 15 Kisha akawaambia watu, “Jitayarisheni kwa ajili ya siku ya tatu. Mwanaume yeyote asimkaribie mwanamke.”
16 Asubuhi ya siku ya tatu kulikuwa na ngurumo na radi pamoja na wingu nene juu ya mlima na mlio mkubwa sana wa tarumbeta. Kila mmoja aliyekuwa kambini akatetemeka. 17 Kisha Musa akawaongoza watu kutoka kambini kukutana na Mungu, nao wakasimama chini ya mlima. 18 Mlima Sinai ulikuwa umefunikwa na moshi, kwa sababu Mwenyezi Mungu alishuka juu yake katika moto. Moshi wa moto huo ulipanda juu kama moshi kutoka tanuru kubwa, na mlima wote ukatetemeka kwa kishindo, 19 nayo sauti ya tarumbeta ikawa kubwa zaidi na zaidi. Kisha Musa akazungumza, nayo sauti ya Mungu ikamjibu.
20 Mwenyezi Mungu akashuka juu ya Mlima Sinai na akamwita Musa apande juu mlimani. Kwa hiyo Musa akapanda juu, 21 naye Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Shuka ukawaonye watu ili wasijipenyeze kutafuta kumwona Mwenyezi Mungu, na wengi wao wakaangamia. 22 Hata makuhani, watakaomkaribia Mwenyezi Mungu ni lazima wajiweke wakfu, la sivyo Mwenyezi Mungu atawaadhibu.”
23 Musa akamwambia Mwenyezi Mungu, “Watu hawawezi kupanda Mlima Sinai kwa sababu wewe mwenyewe ulituonya ukisema, ‘Wekeni mipaka kuuzunguka mlima na kuutenga kama patakatifu.’ ”
24 Mwenyezi Mungu akajibu, “Shuka ukamlete Haruni pamoja nawe. Lakini makuhani pamoja na watu wasije wakalazimisha kuja kwa Mwenyezi Mungu, nisije nikawaadhibu.”
25 Basi Musa akashuka kwa watu na kuwaambia lile aliloambiwa.