24
Agano lathibitishwa
Kisha Mungu akamwambia Musa, “Njooni huku juu kwa Mwenyezi Mungu, wewe na Haruni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli. Mniabudu kwa mbali, lakini Musa peke yake ndiye atakayemkaribia Mwenyezi Mungu; wengine wasije karibu. Nao watu wasije wakapanda pamoja naye.”
Musa alipoenda na kuwaambia watu maneno yote na sheria zote za Mwenyezi Mungu, wakaitikia kwa sauti moja, “Kila kitu alichosema Mwenyezi Mungu tutakifanya.” Ndipo Musa akaandika kila kitu Mwenyezi Mungu alichokuwa amesema.
Akaamka kesho yake asubuhi na mapema na kujenga madhabahu chini ya mlima na kusimamisha nguzo kumi na mbili za mawe kuwakilisha makabila kumi na mawili ya Israeli. Kisha akawatuma vijana wanaume Waisraeli, nao wakatoa sadaka za kuteketezwa na dhabihu za mafahali wachanga kuwa sadaka za amani kwa Mwenyezi Mungu. Musa akachukua nusu ya damu ya wale wanyama na kuiweka kwenye mabakuli, na nusu nyingine akainyunyiza juu ya madhabahu. Kisha akachukua kile Kitabu cha Agano na kuwasomea watu. Nao wakajibu, “Tutafanya kila kitu alichosema Mwenyezi Mungu, nasi tutatii.”
Ndipo Musa akachukua ile damu, akawanyunyizia wale watu, akasema, “Hii ni damu ya agano ambalo Mwenyezi Mungu amelifanya nanyi kufuatana na maneno haya yote.”
Musa na Haruni, Nadabu na Abihu, pamoja na wazee sabini wa Israeli wakapanda mlimani, 10 nao wakamwona Mungu wa Israeli. Chini ya miguu yake kulikuwa na kitu kama sakafu ya mawe ya yakuti samawi, iliyo safi kama anga angavu. 11 Lakini Mungu hakuinua mkono wake dhidi ya hawa viongozi wa Waisraeli; walimwona Mungu, nao wakala na kunywa.
12 Mwenyezi Mungu akamwambia Musa, “Panda uje kwangu huku mlimani na ukae hapa, nami nitakupa vibao vya mawe, vyenye sheria na amri ambazo nimeziandika ziwe mwongozo wao.”
13 Basi Musa akaondoka na Yoshua mtumishi wake, naye Musa akapanda juu kwenye mlima wa Mungu. 14 Musa akawaambia wazee wa Israeli, “Tungojeni hapa hadi tutakapowarudia. Haruni na Huri wako pamoja nanyi, na kila aliye na shauri aweza kuwaendea wao.”
15 Musa alipopanda juu mlimani, wingu liliufunika huo mlima, 16 nao utukufu wa Mwenyezi Mungu ukatua juu ya Mlima Sinai. Kwa muda wa siku sita wingu lilifunika mlima, na siku ya saba Mwenyezi Mungu akamwita Musa kutoka kati ya lile wingu. 17 Kwa Waisraeli utukufu wa Mwenyezi Mungu ulionekana kama moto uteketezao juu ya mlima. 18 Kisha Musa akaingia ndani ya lile wingu alivyokuwa akipanda mlimani. Naye akakaa huko mlimani kwa muda wa siku arobaini, usiku na mchana.