28
Mavazi ya kikuhani
(Kutoka 39:1-7)
1 “Mtwae Haruni ndugu yako aliyeletwa kwako kutoka miongoni mwa Waisraeli, pamoja na wanawe Nadabu, Abihu, Eleazari na Ithamari, ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. 2 Mshonee Haruni ndugu yako mavazi matakatifu ili yampe ukuu na heshima. 3 Waambie mafundi stadi wote niliowapa hekima katika shughuli hiyo wamtengenezee Haruni mavazi hayo, ili awekwe wakfu, anitumikie katika kazi ya ukuhani. 4 Haya ndio mavazi watakayoshona: kifuko cha kifuani, kizibau, kanzu, joho lililofumwa, kilemba na mshipi. Mavazi haya yatashonwa kwa ajili ya ndugu yako Haruni na wanawe ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani. 5 Waambie watumie dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu pamoja na kitani safi.
Kizibau
6 “Tengeneza kizibau cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, za rangi nyekundu na kitani safi iliyosokotwa, kazi ya fundi stadi. 7 Kitakuwa na vipande viwili vya mabegani vilivyoshikizwa kwenye pembe zake mbili ili kufungia kizibau. 8 Mshipi wa kiunoni uliofumwa kwa ustadi utafanana nacho: utakuwa kitu kimoja na hicho kizibau, nao utengenezwe kwa dhahabu na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na nyekundu na kwa kitani iliyosokotwa vizuri.
9 “Chukua vito viwili vya shohamu, na uchore juu yake majina ya wana wa Israeli 10 kufuatana na walivyozaliwa: majina sita katika kito kimoja, na mengine sita katika kito kingine. 11 Yachore majina ya wana wa Israeli juu ya vito hivyo viwili kama vile sonara anavyochonga muhuri. Kisha uvitie vito hivyo katika vijalizo vya dhahabu, 12 na uvifungie juu ya vipande vya mabega ya kizibau yawe kama vito vya ukumbusho kwa wana wa Israeli. Haruni atavaa majina hayo mabegani mwake kama kumbukumbu mbele za Mwenyezi Mungu. 13 Tengeneza vijalizo vya dhahabu 14 na mikufu miwili ya dhahabu safi iliyosokotwa kama kamba, na uifunge mikufu hiyo kwenye vijalizo.
Kifuko cha kifuani
(Kutoka 39:8-21)
15 “Tengeneza kifuko cha kifuani kwa ajili ya kufanya maamuzi, kazi ya fundi stadi. Kitengeneze kama kile kizibau: cha dhahabu, na nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu, cha kitani safi iliyosokotwa. 16 Kitakuwa cha mraba, chenye urefu wa shibiri moja*Shibiri moja ni sawa na sentimita 22. na upana wa shibiri moja, na kikunjwe mara mbili. 17 Kisha weka safu nne za vito vya thamani juu yake. Safu ya kwanza itakuwa na akiki, yakuti manjano na zabarajadi; 18 katika safu ya pili itakuwa na almasi, yakuti samawi na zumaridi; 19 safu ya tatu itakuwa na hiakintho, akiki nyekundu na amethisto; 20 na safu ya nne itakuwa na krisolitho, shohamu na yaspi. Yote yatiwe kwenye vijalizo vya dhahabu. 21 Patakuwa na vito kumi na viwili, kila kimoja kwa jina mojawapo la wana wa Israeli, kila kimoja kichorwe kama muhuri kikiwa na jina mojawapo la yale makabila kumi na mawili.
22 “Kwa ajili ya kile kifuko cha kifuani, tengeneza mikufu ya dhahabu safi, iliyosokotwa kama kamba. 23 Tengeneza pete mbili za dhahabu kwa ajili yake, uzifungie kwenye pembe mbili za hicho kifuko cha kifuani. 24 Funga ile mikufu miwili ya dhahabu kwenye hizo pete zilizo katika pembe za hicho kifuko cha kifuani, 25 nazo zile ncha nyingine za mkufu zifunge kwenye vile vijalizo viwili, na uziunganishe na vile vipande vya mabega vya kile kizibau upande wa mbele. 26 Tengeneza pete mbili za dhahabu, uziunganishe kwenye pembe mbili za chini, upande wa ndani wa kifuko cha kifuani karibu na kizibau. 27 Tengeneza pete nyingine mbili za dhahabu, na uziunganishe sehemu ya chini ya vipande vya mabega, upande wa mbele wa kile kizibau, karibu na pindo, juu kidogo ya mshipi wa kiunoni wa kizibau. 28 Pete za kifuko cha kifuani zitafungwa kwenye pete zile za kizibau kwa kamba ya buluu, ziunganishwe na ule mshipi wa kiunoni, ili kifuko cha kifuani kisisogee kutoka kwa kile kizibau.
29 “Wakati wowote Haruni anapoingia Mahali Patakatifu, atakuwa na yale majina ya wana wa Israeli moyoni mwake juu ya kile kifuko cha kifuani cha uamuzi, kama kumbukumbu ya kudumu mbele za Mwenyezi Mungu. 30 Pia weka Urimu na Thumimu†Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha. ndani ya kifuko cha kifuani, yawe juu ya moyo wa Haruni kila mara aingiapo mbele za Mwenyezi Mungu. Kwa hiyo siku zote Haruni atakuwa na uwezo kufanya maamuzi kwa ajili ya Waisraeli mbele za Mwenyezi Mungu.
Mavazi mengine ya kikuhani
(Kutoka 39:22-31)
31 “Shona joho la kizibau lote kwa kitambaa cha rangi ya buluu tupu, 32 na katikati uweke nafasi ya kuingizia kichwa. Kutakuwa na utepe uliofumwa, unaofanana na ukosi kuizunguka nafasi hiyo, ili isichanike. 33 Tengeneza makomamanga ya nyuzi za rangi ya buluu, za zambarau, na za rangi nyekundu kuzunguka pindo la hilo joho, na uweke pia vikengele vya dhahabu kati ya hayo makomamanga. 34 Hivyo vikengele vya dhahabu na makomamanga vitapishana kuzunguka upindo wa joho lile. 35 Ni lazima Haruni alivae anapofanya huduma. Sauti ya hivyo vikengele itasikika anapoingia na kutoka Mahali Patakatifu mbele za Mwenyezi Mungu, ili asije akafa.
36 “Tengeneza bamba la dhahabu safi na uchore juu yake maneno haya kama vile muhuri huchorwa:
Mtakatifu kwa Mwenyezi Mungu.
37 Lifunge hilo bamba kwa kamba ya buluu kwenye kilemba, nalo ni lazima liwe mbele ya kilemba. 38 Haruni alivae bamba hilo kwenye paji la uso wake, naye atachukua hatia kuhusu sadaka takatifu za Waisraeli wanazoweka wakfu, sadaka za aina yoyote. Litakuwa kwenye paji la uso wa Haruni daima ili zikubalike kwa Mwenyezi Mungu.
39 “Fuma koti la kitani safi na ufanye kilemba cha kitani safi. Mshipi uwe ni kazi ya mtarizi. 40 Watengenezee wana wa Haruni makoti, mishipi na kofia, ili kuwapa ukuu na heshima. 41 Baada ya kumvika Haruni ndugu yako pamoja na wanawe nguo hizi, wapake mafuta na kuwabariki. Waweke wakfu ili wanitumikie katika kazi ya ukuhani.
42 “Watengenezee nguo za ndani za kitani zitakazofunika mwili, kutoka kiunoni hadi mapajani. 43 Haruni na wanawe ni lazima wavae haya kila wanapoingia katika Hema la Kukutania au wanaposogelea madhabahu wakati wa kutoa huduma katika Mahali Patakatifu, ili wasije wakafanya kosa wakafa.
“Haya yawe maagizo ya kudumu kwa Haruni na vizazi vyake.