5
Upanga dhidi ya Yerusalemu
1 “Mwanadamu, chukua upanga mkali na uutumie kama wembe wa kinyozi ili kunyoa kichwa chako na ndevu zako. Kisha uchukue mizani, uzipime na kuzigawanya nywele hizo. 2 Siku zako za kuzingirwa zitakapokwisha, choma theluthi moja ya nywele ndani ya mji. Chukua theluthi nyingine ya hizo nywele uzikatekate kwa upanga ukiuzunguka mji wote, na theluthi ya mwisho uitawanye kwa upepo, kwa kuwa nitawafuatia kwa upanga uliovutwa. 3 Lakini chukua nywele chache uzifungie ndani ya pindo la vazi lako. 4 Tena chukua nywele nyingine chache uzitupe motoni uziteketeze. Moto utaenea kutoka hapo na kufika katika nyumba yote ya Israeli.
5 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Huu ndio mji wa Yerusalemu, ambao nimeuweka katikati ya mataifa, ukiwa umezungukwa na nchi pande zote. 6 Lakini katika uovu wake umeasi sheria na amri zangu kuliko mataifa na nchi zinazouzunguka. Umeasi sheria zangu wala haukufuata amri zangu.
7 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninyi mmekuwa wakaidi kuliko mataifa yanayowazunguka na hamkufuata maagizo yangu wala kuzishika sheria zangu. Wala hamkuweza hata kuzifuata desturi za mataifa yanayowazunguka.
8 “Kwa hiyo, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi mwenyewe niko kinyume nawe, Yerusalemu, na nitakupiga kwa adhabu yangu mbele ya mataifa. 9 Kwa sababu ya sanamu zako zote za machukizo, nitakufanyia kile ambacho kamwe sijafanya kabla wala kamwe sitafanya tena. 10 Kwa hiyo, kati yako baba watakula watoto wao, na watoto watakula baba zao. Nitawapiga kwa adhabu, nami nitawatawanya watu wenu walionusurika pande zote za dunia. 11 Kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, kwa kuwa mmenajisi mahali pangu patakatifu kwa sanamu zenu mbovu na desturi zenu za machukizo, mimi mwenyewe nitaondoa fadhili zangu kwenu. 12 Theluthi ya watu wako watakufa kwa tauni au kwa njaa humu ndani yako; theluthi nyingine itaanguka kwa upanga nje ya kuta zako; nayo theluthi nyingine nitaitawanya kwenye pande nne na kuwafuatia kwa upanga.
13 “Ndipo hasira yangu itakapokoma na ghadhabu yangu dhidi yao kupungua, nami nitakuwa nimejilipizia kisasi. Baada ya kuimaliza ghadhabu yangu juu yao, watajua kuwa Mimi, Mwenyezi Mungu, nimenena katika bidii yangu.
14 “Nitakuangamiza na kukufanya kitu cha kudharauliwa miongoni mwa mataifa yanayokuzunguka, machoni pa wote wapitao karibu nawe. 15 Utakuwa kitu cha kudharauliwa na cha dhihaka, kitu cha onyo na cha kutisha kwa mataifa yanayokuzunguka, nitakapokupiga kwa adhabu katika hasira na ghadhabu yangu kwa kukukemea kwa ukali. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena. 16 Nitakapokurushia mishale yangu ya kufisha na yenye kuharibu ya njaa, nitairusha ili kukuangamiza. Nitaleta njaa zaidi na zaidi juu yako na kukomesha upatikanaji wa chakula kwako. 17 Nitatuma njaa na wanyama pori dhidi yako, navyo vitakuacha bila watoto. Tauni na umwagaji wa damu vitapita katikati yako, nami nitaleta upanga juu yako. Mimi Mwenyezi Mungu nimenena.”