7
Mwisho umewadia
1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi kwa nchi ya Israeli:
“ ‘Mwisho! Mwisho umekuja
juu ya pembe nne za nchi!
3 Sasa mwisho umekuja juu yenu,
nami nitamwaga hasira yangu dhidi yenu.
Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu
na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za kuchukiza.
4 Sitawaonea huruma
wala kuwarehemu.
Hakika nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu
na desturi za machukizo miongoni mwenu.
Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’
5 “Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Maafa! Maafa ambayo hayajasikiwa!
Tazama, yanakuja!
6 Mwisho umewadia!
Mwisho umewadia!
Umejiinua wenyewe dhidi yenu.
Tazama, umewadia!
7 Maangamizi yamekuja juu yenu,
ninyi mnaoishi katika nchi.
Wakati umewadia! Siku imekaribia!
Kuna hofu kuu ya ghafula juu ya milima, wala si furaha.
8 Ninakaribia kumwaga ghadhabu yangu juu yenu
na kumaliza hasira yangu dhidi yenu.
Nitawahukumu sawasawa na matendo yenu
na kuwalipiza kwa ajili ya desturi zenu zote za machukizo.
9 Sitawaonea huruma
wala kuwarehemu.
Nitawalipiza kwa ajili ya matendo yenu
na desturi za machukizo miongoni mwenu.
“ ‘Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu ambaye huwapiga.
10 “ ‘Tazama, siku imefika!
Tazama, imewadia!
Maangamizi yamezuka ghafula,
fimbo imechanua,
nayo majivuno yamechipua!
11 Jeuri imeinuka
kuwa fimbo ya kuadhibu waovu.
Hakuna hata mmoja wa hao watu atakayeachwa,
hata mmoja wa kundi hilo:
hakuna utajiri wao utabaki,
wala chochote cha thamani.
12 Wakati umewadia,
siku imefika.
Mnunuzi na asifurahi
wala muuzaji asihuzunike,
kwa maana ghadhabu iko juu ya kundi lote.
13 Muuzaji hatajipatia tena
ardhi aliyoiuza
wakati wote wawili wangali hai.
Kwa kuwa maono kuhusu kundi lote
hayatatanguka.
Kwa sababu ya dhambi zao, hakuna hata mmoja
atakayeokoa maisha yake.
14 “ ‘Wajapopiga tarumbeta
na kuweka kila kitu tayari,
hakuna hata mmoja atakayeenda vitani,
kwa maana ghadhabu yangu iko juu ya kundi lote.
15 Nje ni upanga,
ndani ni tauni na njaa.
Walio shambani
watakufa kwa upanga,
nao waliomo mjini
njaa na tauni vitawala.
16 Wote watakaopona
na kutoroka watakuwa milimani,
wakiomboleza kama hua wa mabondeni,
kila mmoja kwa sababu ya dhambi zake.
17 Kila mkono utalegea
na kila goti litakuwa dhaifu kama maji.
18 Watavaa gunia
na kufunikwa na hofu.
Nyuso zao zitafunikwa na aibu,
na vichwa vyao vitanyolewa.
19 “ ‘Watatupa fedha yao barabarani,
nayo dhahabu yao itakuwa najisi.
Fedha yao na dhahabu yao
havitaweza kuwaokoa
katika siku hiyo ya ghadhabu ya Mwenyezi Mungu.
Hawatashibisha njaa yao
au kujaza tumbo zao kwa hiyo fedha wala dhahabu,
kwa sababu imewaponza wajikwae dhambini.
20 Walijivunia vito vyao vizuri
na kuvitumia kutengeneza sanamu za machukizo
na vinyago vya upotovu.
Kwa hiyo nitavifanya vitu hivyo kuwa najisi kwao.
21 Nitavitia vyote mikononi mwa wageni
kuwa nyara na kuwa vitu vilivyotekwa mikononi mwa watu waovu wa dunia,
nao watavinajisi.
22 Nitaugeuza uso wangu mbali nao,
nao waovu wa dunia watapanajisi mahali pangu pa thamani.
Wanyang’anyi watapaingia
na kupanajisi.
23 “ ‘Andaa minyororo,
kwa sababu nchi imejaa umwagaji wa damu
na mji umejaa udhalimu.
24 Nitaleta taifa ovu kuliko yote
kumiliki nyumba zao.
Nitakomesha kiburi cha wenye nguvu
na mahali pao patakatifu patatiwa unajisi.
25 Hofu ya ghafula itakapokuja,
watatafuta amani, lakini haitapatikana.
26 Maafa juu ya maafa yatakuja,
tetesi ya mabaya juu ya tetesi ya mabaya.
Watajitahidi kupata maono kutoka kwa nabii;
mafundisho ya sheria toka kwa kuhani yatapotea,
vivyo hivyo shauri kutoka kwa wazee.
27 Mfalme ataomboleza,
mwana wa mfalme atavikwa kukata tamaa,
nayo mikono ya watu wa nchi itatetemeka.
Nitawaadhibu kulingana na matendo yao,
na kwa kanuni zao wenyewe nitawahukumu.
“ ‘Ndipo watajua kwamba Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”