9
Waabudu sanamu wauawa
Kisha nikamsikia akiita kwa sauti kubwa akisema, “Walete wasimamizi wa mji hapa, kila mmoja akiwa na silaha mkononi mwake.” Nami nikaona watu sita wakija toka upande wa lango la juu linalotazama kaskazini, kila mmoja akiwa na silaha za kuangamiza mkononi mwake. Kati yao palikuwa na mtu aliyevaa mavazi ya kitani safi, naye alikuwa na vifaa vya mwandishi kiunoni mwake. Wakaingia ndani ya Hekalu na kusimama pembeni mwa madhabahu ya shaba.
Basi utukufu wa Mungu wa Israeli ukaondoka hapo juu ya makerubi, ulikokuwa umekaa, ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Ndipo Mwenyezi Mungu akamwita yule mtu aliyevaa kitani safi na mwenye vifaa vya mwandishi kiunoni mwake, akamwambia, “Pita katika mji wote wa Yerusalemu ukaweke alama kwenye paji za nyuso za wale watu wanaohuzunika na kuomboleza kwa sababu ya machukizo yote yanayotendeka katika mji huu.”
Nikiwa ninasikiliza, akawaambia wale wengine, “Mfuateni anapopita katika mji wote mkiua, pasipo huruma wala masikitiko. Waueni wazee, vijana wa kiume na wa kike, wamama na watoto, lakini msimguse mtu yeyote mwenye alama. Anzieni katika mahali pangu patakatifu.” Kwa hiyo wakaanza na wale wazee waliokuwa mbele ya Hekalu.
Ndipo akawaambia, “Linajisini Hekalu na mkazijaze ua zake maiti za wale waliouawa. Nendeni!” Kwa hiyo wakaenda, wakaanza kuua watu mjini kote. Walipokuwa wakiwaua watu, nami nikaachwa peke yangu, nilisujudu, nikapaza sauti na kusema, “Ee Bwana Mungu Mwenyezi! Je, utaangamiza mabaki yote ya Israeli, katika kumwagwa huku kwa ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?”
Mwenyezi Mungu akanijibu, “Dhambi ya nyumba ya Israeli na Yuda imekuwa kubwa mno kupita kiasi, nchi imejaa umwagaji damu na mjini kumejaa udhalimu. Kwani wamesema, ‘Mwenyezi Mungu ameiacha nchi; Mwenyezi Mungu haoni.’ 10 Kwa hiyo sitawahurumia wala kuwarehemu, lakini nitaleta juu ya vichwa vyao yale waliyoyatenda.”
11 Ndipo mtu yule aliyevaa nguo ya kitani na mwenye vifaa vya mwandishi kiunoni mwake akarudi na kutoa taarifa, akisema, “Nimefanya kama ulivyoniagiza.”