20
Israeli waasi
1 Katika mwaka wa saba, mwezi wa tano siku ya kumi, baadhi ya wazee wa Israeli wakaja ili kutaka ushauri kwa Mwenyezi Mungu, wakaketi mbele yangu.
2 Ndipo neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 3 “Mwanadamu, sema na wazee wa Israeli uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Kwa nini mmekuja? Je, ni kutaka ushauri kwangu? Hakika kama niishivyo, sitawaruhusu mtake ushauri toka kwangu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’
4 “Je, utawahukumu? Je, mwanadamu, utawahukumu? Basi uwakabili kwa ajili ya machukizo ya baba zao 5 na uwaambie: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Siku ile nilipochagua Israeli, niliwaapia wazao wa nyumba ya Yakobo kwa mkono ulioinuliwa nami nikajidhihirisha kwao huko Misri. Kwa mkono ulioinuliwa niliwaambia, “Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.” 6 Siku ile niliwaapia kwamba nitawatoa katika nchi ya Misri na kuwaleta katika nchi niliyowachagulia, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi nzuri kupita zote. 7 Nami nikawaambia, “Kila mmoja wenu aondolee mbali sanamu za chukizo ambazo mmekazia macho, nanyi msijitie unajisi kwa sanamu za Misri. Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”
8 “ ‘Lakini waliniasi na hawakunisikiliza, hawakuondolea mbali sanamu za machukizo ambazo walikuwa wamezikazia macho, wala kuondolea mbali sanamu za Misri. Ndipo nikasema, nitawamwagia ghadhabu yangu na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko Misri. 9 Lakini kwa ajili ya Jina langu niliwatoa katika nchi ya Misri. Nilifanya hivyo ili kulinda Jina langu lisinajisiwe machoni mwa mataifa walioishi miongoni mwao, na ambao machoni pao nilikuwa nimejifunua kwa Waisraeli. 10 Kwa hiyo nikawaongoza watoke Misri na kuwaleta jangwani. 11 Nikawapa amri zangu na kuwajulisha sheria zangu, kwa kuwa mtu anayezitii ataishi kwa hizo. 12 Pia niliwapa Sabato zangu kama ishara kati yangu nao, ili wapate kujua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu niliwafanya watakatifu.
13 “ ‘Lakini watu wa Israeli waliniasi Mimi jangwani. Hawakufuata amri zangu, bali walikataa sheria zangu, ingawa mtu yule anayezitii ataishi kwa hizo sheria, nao walizinajisi Sabato zangu kabisa. Hivyo nilisema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kuwaangamiza huko jangwani. 14 Lakini kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile ambacho kitalifanya Jina langu lisitiwe unajisi machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli. 15 Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba nisingewaingiza katika nchi niliyowapa, nchi inayotiririka maziwa na asali, nchi nzuri kuliko zote, 16 kwa sababu walikataa sheria zangu na hawakufuata amri zangu, na wakazinajisi Sabato zangu. Kwa kuwa mioyo yao iliandama sanamu zao. 17 Lakini niliwahurumia, wala sikuwaangamiza wala kuwafuta kabisa jangwani. 18 Niliwaambia watoto wao kule jangwani, “Msifuate amri za baba zenu wala kushika sheria zao au kujinajisi kwa sanamu zao. 19 Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu; fuateni amri zangu, tena kuweni waangalifu kushika sheria zangu. 20 Zitakaseni Sabato zangu ili ziwe ishara kati yangu nanyi. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, Mungu wenu.”
21 “ ‘Lakini watoto hao wakaniasi: Hawakufuata amri zangu, wala hawakuwa waangalifu kushika sheria zangu, ingawa mtu anayezitii anaishi kwa hizo sheria, nao wakazinajisi Sabato zangu. Hivyo nikasema ningemwaga ghadhabu yangu juu yao na kutimiza hasira yangu dhidi yao huko jangwani. 22 Lakini nikauzuia mkono wangu, na kwa ajili ya Jina langu nikafanya kile kingezuia Jina langu kunajisiwa machoni mwa mataifa ambao mbele yao nilikuwa nimewatoa Waisraeli. 23 Tena kwa mkono ulioinuliwa nikawaapia huko jangwani kwamba ningewatawanya miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbalimbali, 24 kwa sababu hawakutii sheria zangu lakini walikuwa wamekataa amri zangu na kuzinajisi Sabato zangu, nayo macho yao yakatamani sanamu za baba zao. 25 Pia niliwaacha wafuate amri ambazo hazikuwa nzuri na sheria ambazo mtu hawezi kuishi kwa hizo sheria. 26 Nikawaacha wanajisiwe kwa matoleo yao ya kuwatoa kafara wazaliwa wao wa kwanza kwa sanamu, ili nipate kuwajaza na hofu hadi wajue kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’
27 “Kwa hiyo, mwanadamu, sema na watu wa Israeli na uwaambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Katika jambo hili pia, baba zenu walinikufuru kwa kuniacha mimi: 28 Nilipowaleta katika nchi niliyokuwa nimeapa kuwapa na kuona kilima chochote kirefu au mti wowote wenye majani mengi, huko walitoa dhabihu zao, wakatoa sadaka ambazo zilichochea hasira yangu, wakafukiza uvumba wenye harufu nzuri na kumimina sadaka zao za kinywaji. 29 Ndipo nikawaambia: Ni nini maana yake hapa mahali pa juu pa kuabudia mnapopaendea?’ ” (Basi mahali pale panaitwa Bama*maana yake Mahali pa juu pa kuabudia hata leo.)
Hukumu na kurudishwa
30 “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Je, mtajinajisi kama vile baba zenu walivyofanya na kutamani vinyago vyao vya machukizo? 31 Mnapotoa matoleo yenu, yaani kutoa kafara watoto wenu motoni, mnaendelea kujinajisi na sanamu zenu zote hadi leo. Je, niulizwe ushauri na ninyi, ee nyumba ya Israeli? Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, mimi sitaulizwa ushauri na ninyi.
32 “ ‘Lile lililoko mioyoni mwenu kamwe halitatokea, mnaposema, “Tunataka tuwe kama mataifa mengine, kama watu wengine wa dunia, wanaotumikia miti na mawe.” 33 Hakika kama niishivyo asema Bwana Mungu Mwenyezi, nitawatawala kwa mkono wa nguvu, na kwa mkono ulionyooshwa, na kwa ghadhabu iliyomwagika. 34 Nitawatoa toka katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlikotawanywa, kwa mkono wa nguvu na kwa mkono ulionyooshwa na kwa ghadhabu iliyomwagwa. 35 Nitawaleta katika jangwa la mataifa na huko nitatekeleza hukumu juu yenu uso kwa uso. 36 Kama nilivyowahukumu baba zenu katika jangwa la nchi ya Misri, ndivyo nitakavyowahukumu ninyi, asema Bwana Mungu Mwenyezi. 37 Nitawafanya mpite chini ya fimbo yangu, nami nitawaleta katika mkataba wa agano. 38 Nitawaondoa miongoni mwenu wale wanaohalifu na wale wanaoasi dhidi yangu. Ingawa nitawatoa katika nchi wanazoishi, hawataingia katika nchi ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
39 “ ‘Kwenu ninyi, ee nyumba ya Israeli, hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nendeni mkatumikie sanamu zenu, kila mmoja wenu! Lakini baadaye hakika mtanisikiliza mimi nanyi hamtalinajisi tena Jina langu takatifu, kwa matoleo yenu na sanamu zenu. 40 Kwa kuwa katika mlima wangu mtakatifu, mlima mrefu wa Israeli, asema Bwana Mungu Mwenyezi, hapo katika nchi nyumba yote ya Israeli itanitumikia mimi, nami huko nitawakubali. Huko nitataka sadaka zenu na matoleo ya malimbuko yenu, pamoja na dhabihu zenu takatifu zote. 41 Nitawakubali ninyi kama uvumba wenye harufu nzuri wakati nitakapowatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mlipokuwa mmetawanyika, nami nitajionesha kuwa mtakatifu miongoni mwenu na machoni mwa mataifa. 42 Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapowaleta katika nchi ya Israeli, nchi niliyokuwa nimeapa kwa mkono ulioinuliwa kuwapa baba zenu. 43 Hapo ndipo nitakapokumbuka mwenendo wenu na matendo yenu yote ambayo kwayo mlijitia unajisi, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya maovu yote mliyokuwa mmetenda. 44 Nanyi mtajua kuwa mimi ndimi Mwenyezi Mungu, nitakapowatendea kwa ajili ya Jina langu, wala si sawasawa na njia zenu mbaya na matendo yenu maovu, ee nyumba ya Israeli, asema Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
Unabii dhidi ya kusini
45 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 46 “Mwanadamu, uelekeze uso wako upande wa kusini, hubiri dhidi ya upande wa kusini, na utoe unabii dhidi ya msitu wa Negebu. 47 Waambie watu wa Negebu: ‘Sikieni neno la Mwenyezi Mungu. Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Ninakaribia kukuwasha moto, nao utateketeza miti yako yote, mibichi na iliyokauka. Miali ya moto haitaweza kuzimwa na kila uso kutoka kusini mpaka kaskazini utakaushwa kwa moto huo. 48 Kila mmoja ataona kuwa Mimi Mwenyezi Mungu ndiye niliyeuwasha huo moto; nao hautazimwa.’ ”
49 Ndipo niliposema, “Aa, Bwana Mungu Mwenyezi! Wao hunisema, ‘Huyu si huzungumza mafumbo tu?’ ”