27
Maombolezo kwa ajili ya Tiro 
  1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema:   2 “Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Tiro.   3 Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:  
“ ‘Ee Tiro, wewe umesema,  
“Mimi ni mkamilifu katika uzuri.”   
 4 Mipaka yako ilikuwa katika moyo wa bahari,  
wajenzi wako walikamilisha uzuri wako.   
 5 Walizifanya mbao zako zote  
kwa misunobari kutoka Seniri*yaani Mlima Hermoni;  
walichukua mwerezi kutoka Lebanoni  
kukutengenezea mlingoti.   
 6 Walichukua mialoni kutoka Bashani  
wakakutengenezea makasia yako;  
kwa miti ya msanduku  
kutoka pwani ya Kitimu  
wakatengeneza sitaha yako  
na kuipamba kwa pembe za ndovu.   
 7 Kitani safi kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa tanga lako,  
nacho kilikuwa bendera yako;  
chandarua chako kilikuwa cha rangi ya buluu na ya zambarau  
kutoka visiwa vya Al-Yasa.   
 8 Wakaaji wa Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia yako;  
watu wako wenye ustadi, ee Tiro,  
ndio walikuwa mabaharia wako.   
 9 Wazee wa Gebali†yaani Bubilo pamoja na mafundi stadi  
walikuwa mafundi wako kwenye meli.  
Meli zote za baharini na mabaharia wao  
walikuja kwako ili kubadilishana bidhaa zako.   
 10 “ ‘Wanaume wa Uajemi, Ludi na Putu  
walikuwa askari katika jeshi lako.  
Walitundika ngao zao na chapeo zao kwenye kuta zako,  
wakileta fahari yako.   
 11 Watu wa Arvadi na wa Heleki  
walikuwa juu ya kuta zako pande zote;  
watu wa Gamadi  
walikuwa kwenye minara yako.  
Walitundika ngao zao kuzizunguka kuta zako;  
wakaukamilisha uzuri wako.   
 12 “ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali yako.   
 13 “ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki walifanya biashara nawe; walibadilisha binadamu na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako.   
 14 “ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali yako.   
 15 “ ‘Watu wa Dedani‡yaani Rodo walifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo.   
 16 “ ‘Watu wa Aramu walifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, wakibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe§yaani marijani, jiwe la pwani au baharini na akiki nyekundu.   
 17 “ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe; walibadilishana ngano iliyotoka Minithi, mtama, asali, mafuta na zeri kwa bidhaa zako.   
 18 “ ‘Dameski walifanya biashara nawe kwa sababu ya wingi wa bidhaa zako na ukuu wa utajiri wa mali zako, wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari.   
 19 “ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali walikuletea mali ya biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai.   
 20 “ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi.   
 21 “ ‘Arabuni na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako; walifanya biashara nawe ya kubadilishana wana-kondoo, kondoo dume na mbuzi.   
 22 “ ‘Wafanyabiashara wa Sheba na wa Raama walifanya biashara nawe, wakabadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezo, vito vya thamani na dhahabu.   
 23 “ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe.   24 Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara.   
 25 “ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo  
zinazokusafirishia bidhaa zako.  
Umejazwa shehena kubwa  
katika moyo wa bahari.   
 26 Wapiga makasia wako wanakupeleka  
mpaka kwenye maji makuu.  
Lakini upepo wa mashariki utakuvunja vipande vipande  
moyoni mwa bahari.   
 27 Utajiri wako, bidhaa zako na mali yako,  
mabaharia wako, manahodha wako,  
mafundi wako wa meli,  
wafanyabiashara wako na askari wako wote,  
na kila mmoja aliye kwenye meli  
atazama kwenye moyo wa bahari  
siku ile meli yako itakapovunjika.   
 28 Nchi za pwani zitatetemeka  
wakati mabaharia wako watakapopiga kelele.   
 29 Wote wapigao makasia  
wataacha meli zao,  
mabaharia wote na wanamaji wote  
watasimama pwani.   
 30 Watapaza sauti zao  
na kulia sana kwa ajili yako;  
watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao  
na kujivingirisha kwenye majivu.   
 31 Watanyoa nywele zao kwa ajili yako,  
nao watavaa magunia.  
Watakulilia kwa uchungu wa moyo  
na kwa maombolezo makuu.   
 32 Watakapokuwa wanalia na kuomboleza juu yako,  
watafanya maombolezo kukuhusu wakisema:  
“Ni nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro,  
katika moyo wa bahari?”   
 33 Bidhaa zako zilipotoka baharini,  
ulitosheleza mataifa mengi;  
kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako  
ulitajirisha wafalme wa dunia.   
 34 Sasa umevunjavunjwa na bahari,  
katika vilindi vya maji,  
bidhaa zako na kundi lako lote  
vimezama pamoja nawe.   
 35 Wote wanaoishi katika nchi za pwani  
wanakustaajabia;  
wafalme wao wanatetemeka kwa hofu kuu,  
nazo nyuso zao zimekunjamana kwa woga.   
 36 Wafanyabiashara miongoni mwa mataifa wanakucheka;  
umefikia mwisho wa kutisha  
nawe hutakuwepo tena.’ ”