29
Unabii dhidi ya Misri
Hukumu juu ya Farao
Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili, neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao mfalme wa Misri na utabiri dhidi yake na dhidi ya Misri yote. Nena, nawe useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi:
“ ‘Mimi ni kinyume nawe, Farao, mfalme wa Misri,
ewe mnyama mkubwa ulalaye katikati ya vijito vyako.
Unasema, “Mto Naili ni wangu mwenyewe;
niliufanya kwa ajili yangu mwenyewe.”
Lakini nitatia ndoana katika mataya yako
nami nitawafanya samaki wa vijito vyako
washikamane na magamba yako.
Nitakutoa katikati ya vijito vyako,
pamoja na samaki wote
walioshikamana na magamba yako.
Nitakutupa jangwani,
wewe pamoja na samaki wote wa vijito vyako.
Utaanguka uwanjani,
nawe hutakusanywa au kuchukuliwa.
Nitakutoa uwe chakula
kwa wanyama wa nchi
na ndege wa angani.
Ndipo wale wote wanaoishi Misri watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
 
“ ‘Umekuwa fimbo ya tete kwa nyumba ya Israeli. Walipokushika kwa mikono yao, ulivunjika na kuchana mabega yao; walipokuegemea, ulivunjika na migongo yao ikateguka.
“ ‘Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaleta upanga juu yako na kuua watu wako na wanyama wao. Misri itakuwa ukiwa na isiyolimwa wala kukaliwa na watu. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
“ ‘Kwa sababu ulisema, “Mto Naili ni wangu; mimi niliuumba,” 10 kwa hiyo mimi ni kinyume nawe na kinyume na vijito vyako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa magofu na ukiwa kuanzia Migdoli hadi Aswani, hata kufikia mpaka wa Kushi. 11 Hakuna unyayo wa mtu au mnyama utakaopita ndani yake, wala hakuna yeyote atakayeishi humo kwa muda wa miaka arobaini. 12 Nitaifanya nchi ya Misri ukiwa, miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yake itabaki ukiwa miaka arobaini miongoni mwa miji iliyo magofu. Nami nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwatapanya katika nchi nyingine.
13 “ ‘Lakini hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mwishoni mwa hiyo miaka arobaini, nitawakusanya Wamisri kutoka mataifa walikotawanywa. 14 Nitawarejesha hao Wamisri kutoka kutekwa kwao na kuwaweka Pathrosi*yaani Misri ya Juu, nchi ya baba zao. Huko watakuwa na ufalme usiokuwa na nguvu. 15 Utakuwa ufalme dhaifu kuliko zote na kamwe Misri haitajikweza tena juu ya mataifa mengine. Nitaufanya ufalme wake dhaifu sana kiasi kwamba kamwe hautatawala tena juu ya mataifa mengine. 16 Misri haitakuwa tena tumaini la watu wa Israeli bali itakuwa kumbukumbu ya dhambi yao kwa kuigeukia kuomba msaada. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Bwana Mungu Mwenyezi.’ ”
Zawadi ya Nebukadneza
17 Katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza, neno la Mwenyezi Mungu likanijia, kusema: 18 “Mwanadamu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliongoza jeshi lake kufanya kazi ngumu dhidi ya Tiro; kila kichwa kilipata upara na kila bega likachunika. Lakini yeye na jeshi lake hawakupata malipo yoyote kutokana na muda wote aliongoza hiyo vita dhidi ya Tiro. 19 Kwa hiyo hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Nitaitia Misri mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atachukua utajiri wa Misri. Atateka mateka na kuchukua nyara mali ya Misri kama ujira kwa ajili ya jeshi lake. 20 Nimempa mfalme wa Babeli nchi ya Misri kuwa ujira kwa juhudi zake kwa sababu yeye na jeshi lake walifanya kwa ajili yangu, asema Bwana Mungu Mwenyezi.
21 “Katika siku hiyo nitaifanya nyumba ya Israeli iwe na nguvu nami nitakifungua kinywa chako miongoni mwao. Ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.”

*29:14 yaani Misri ya Juu