35
Unabii dhidi ya Edomu
1 Neno la Mwenyezi Mungu likanijia kusema: 2 “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Mlima Seiri, utabiri dhidi yake 3 na useme: ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Mimi ni kinyume nawe, ee Mlima Seiri, nami nitanyoosha mkono wangu dhidi yako na kukufanya ukiwa. 4 Nitaifanya miji yako kuwa magofu nawe utakuwa ukiwa. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
5 “ ‘Kwa sababu ulificha moyoni uadui wa siku nyingi nawe ukawatoa Waisraeli wauawe kwa upanga wakati wa maafa yao, wakati adhabu yake ilipofikia kilele chake, 6 kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nitakutia katika umwagaji damu nao utakufuatia. Kwa kuwa hukuchukia kumwaga damu, kumwaga damu kutakufuatia. 7 Nitaufanya Mlima Seiri ukiwa na kuukatilia mbali na wote wanaokuja na wanaoenda. 8 Nitaijaza milima yenu kwa watu wake waliouawa, wale waliouawa kwa upanga wataanguka juu ya vilima vyako na katika mabonde yako na katika makorongo yako yote. 9 Nitakufanya ukiwa milele, watu hawataishi katika miji yako. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.
10 “ ‘Kwa sababu umesema, “Mataifa haya mawili na nchi hizi zitakuwa zetu nasi tutazimiliki,” ingawa hata Mimi Mwenyezi Mungu nilikuwa huko, 11 kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema Bwana Mungu Mwenyezi, nitakutenda kwa kadiri ya hasira na wivu uliouonesha katika chuki yako juu yao nami nitafanya nijulikane miongoni mwao wakati nitakapokuhukumu. 12 Ndipo utakapojua kuwa Mimi Mwenyezi Mungu nimesikia mambo yote ya dharau uliyosema dhidi ya milima ya Israeli. Ulisema, “Wamefanyika ukiwa na kutiwa mikononi mwetu tuwararue.” 13 Ulijigamba dhidi yangu na kusema maneno dhidi yangu bila kujizuia, nami nikayasikia. 14 Hili ndilo asemalo Bwana Mungu Mwenyezi: Dunia yote inaposhangilia, nitakufanya ukiwa. 15 Kwa sababu ulishangilia wakati urithi wa nyumba ya Israeli ulipofanyika ukiwa, hivyo ndivyo nitakavyokutendea. Utakuwa ukiwa, ee Mlima Seiri, wewe na Edomu yote. Kisha ndipo watajua kuwa Mimi ndimi Mwenyezi Mungu.’ ”