8
Orodha ya viongozi wa jamaa waliorudi na Ezra
Hawa ndio viongozi wa jamaa pamoja na wale walioandikwa ambao walikuja pamoja nami kutoka Babeli wakati wa utawala wa Mfalme Artashasta:
 
wa wazao wa Finehasi,
alikuwa Gershoni;
wa wazao wa Ithamari,
alikuwa Danieli;
wa wazao wa Daudi,
alikuwa Hatushi wa wazao wa Shekania;
wa wazao wa Paroshi,
alikuwa Zekaria, na watu mia moja na hamsini walioandikishwa;
wa wazao wa Pahath-Moabu,
alikuwa Eliehoenai mwana wa Zerahia na wanaume mia mbili;
wa wazao wa Zatu,
alikuwa Shekania mwana wa Yahazieli na wanaume mia tatu;
wa wazao wa Adini,
alikuwa Ebedi mwana wa Yonathani na wanaume hamsini;
wa wazao wa Elamu,
alikuwa Yeshaya mwana wa Athalia, na wanaume sabini;
wa wazao wa Shefatia,
alikuwa Zebadia mwana wa Mikaeli na wanaume themanini;
wa wazao wa Yoabu,
alikuwa Obadia mwana wa Yehieli na wanaume mia mbili kumi na nane;
10 wa wazao wa Bani,
alikuwa Shelomithi mwana wa Yosifia na wanaume mia moja na sitini;
11 wa wazao wa Bebai,
alikuwa Zekaria mwana wa Bebai na wanaume ishirini na nane;
12 wa wazao wa Azgadi,
alikuwa Yohanani mwana wa Hakatani na wanaume mia moja na kumi;
13 wa wazao wa Adonikamu:
hawa walikuwa wa mwisho ambao majina yao ni Elifeleti, Yeueli, Shemaya na wanaume sitini;
14 wa wazao wa Bigwai,
walikuwa Uthai na Zakuri na wanaume sabini.
Kurudi Yerusalemu
15 Niliwakusanya kwenye mto unaotiririka kuelekea Ahava, nasi tukapiga kambi pale siku tatu. Nilipokagua kati ya watu na makuhani, sikuwapata Walawi. 16 Basi niliwaita Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu waliokuwa viongozi na Yoyaribu na Elnathani waliokuwa wasomi, 17 nikawatuma kwa Ido kiongozi huko Kasifia. Niliwaambia watakayomwambia Ido na ndugu zake, watumishi wa Hekalu*yaani Wanethini (pia 8:20). huko Kasifia, ili waweze kutuletea wahudumu kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu. 18 Kwa sababu mkono wa neema wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, walituletea Sherebia, mtu mwenye busara kutoka wazao wa Mahli mwana wa Lawi, mwana wa Israeli, na wana wa Sherebia pamoja na ndugu zao wanaume kumi na nane. 19 Naye Hashabia, pamoja na Yeshaya kutoka wazao wa Merari na ndugu zake na wapwa wake, walikuwa wanaume ishirini. 20 Vilevile walileta watumishi wa Hekalu mia mbili na ishirini, kikundi ambacho Daudi na maafisa walikuwa wamekianzisha ili kusaidia Walawi. Wote waliorodheshwa kwa majina.
21 Kando ya Mto Ahava, hapo nilitangaza kufunga, ili tujinyenyekeze mbele za Mungu wetu na kumwomba kwa ajili ya kutujalia safari ya amani sisi na watoto wetu, pamoja na mali yetu yote. 22 Niliona aibu kumwomba mfalme askari na wapanda farasi wa kutulinda njiani kutokana na adui zetu, kwa sababu tulikwisha kumwambia mfalme, “Mkono wa neema wa Mungu wetu uko juu ya kila mmoja anayemtafuta, lakini hasira yake kubwa ni dhidi ya wote wamwachao.” 23 Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu wetu kuhusu jambo hili, naye akajibu maombi yetu.
24 Kisha niliwatenga viongozi wa makuhani kumi na wawili, pamoja na Sherebia, Hashabia na ndugu zao kumi, 25 nami nikawapimia fedha, dhahabu na vifaa ambavyo mfalme, washauri wake, maafisa wake na Waisraeli wote waliokuwepo walikuwa wamevitoa sadaka kwa ajili ya nyumba ya Mungu wetu. 26 Niliwapimia talanta mia sita na hamsiniTalanta 650 za fedha ni sawa na tani 25. za fedha, vifaa vingine vya fedha vya uzito wa talanta mia mojaTalanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.75., talanta mia moja za dhahabu, 27 mabakuli ishirini ya dhahabu ya thamani ya darkoni elfu moja§Darkoni 1,000 ni sawa na kilo 8.5., na vyombo viwili vya shaba iliyosuguliwa, ya thamani kama dhahabu.
28 Niliwaambia, “Ninyi pamoja na vyombo hivi ni wakfu kwa Mwenyezi Mungu. Fedha na dhahabu ni sadaka ya hiari kwa Mwenyezi Mungu, Mungu wa baba zenu. 29 Vilindeni kwa uangalifu hadi mtakapovipima ndani ya vyumba vya nyumba ya Mwenyezi Mungu katika Yerusalemu mbele ya makuhani, viongozi na Walawi pamoja na wakuu wa jamaa za Israeli.” 30 Ndipo makuhani na Walawi wakapokea fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu ambavyo vilipimwa na kupelekwa katika nyumba ya Mungu wetu mjini Yerusalemu.
31 Tulianza safari kutoka Mto Ahava kwenda Yerusalemu siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza. Mkono wa Mungu wetu ulikuwa juu yetu, naye njiani alitulinda dhidi ya adui na wanyang’anyi. 32 Kwa hiyo tuliwasili Yerusalemu ambapo tulipumzika kwa siku tatu.
33 Katika siku ya nne, ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima fedha, dhahabu na vyombo vilivyowekwa wakfu, tukakabidhi mikononi mwa kuhani Meremothi mwana wa Uria. Eleazari mwana wa Finehasi alikuwa pamoja naye, na pia Walawi wawili, Yozabadi mwana wa Yeshua, na Noadia mwana wa Binui. 34 Kila kitu kilihesabiwa kwa idadi na kupimwa kwa uzito, nao uzito wote uliandikwa wakati ule.
35 Kisha mateka waliokuwa wamerudi kutoka utumwani wakatoa sadaka za kuteketezwa kwa moto kwa Mungu wa Israeli: mafahali kumi na wawili kwa ajili ya Israeli wote, kondoo dume tisini na sita, wana-kondoo sabini na saba, na beberu kumi na wawili kuwa sadaka ya dhambi. Hii yote ilikuwa sadaka ya kuteketezwa kwa moto kwa Mwenyezi Mungu. 36 Pia walikabidhi manaibu wa mfalme na watawala wa Ng’ambo ya Mto Frati maagizo ya mfalme, ambao baadaye walitoa msaada kwa watu na kwa nyumba ya Mungu.

*8:17 yaani Wanethini (pia 8:20).

8:26 Talanta 650 za fedha ni sawa na tani 25.

8:26 Talanta 100 za fedha ni sawa na tani 3.75.

§8:27 Darkoni 1,000 ni sawa na kilo 8.5.