5
Uhuru ndani ya Al-Masihi
Al-Masihi alitupatia uhuru, akataka tubaki huru. Hivyo simameni imara wala msikubali tena kulemewa na nira ya utumwa.
Sikilizeni! Mimi, Paulo, nawaambieni kwamba mkikubali kutahiriwa, basi Al-Masihi hatakuwa na thamani kwenu hata kidogo. Namshuhudia tena kila mtu anayekubali kutahiriwa kwamba inampasa kushika Torati yote. Ninyi mnaotafuta kuhesabiwa haki kupitia kwa Torati mmetengwa na Al-Masihi, mko mbali na neema ya Mungu. Kwa maana, kupitia Roho wa Mungu tunangojea kwa shauku tumaini la haki kwa imani. Kwa maana ndani ya Al-Masihi Isa, kutahiriwa au kutokutahiriwa hakuleti tofauti, bali lililo muhimu ni imani itendayo kazi kupitia kwa upendo.
Mlikuwa mkipiga mbio vizuri. Ni nani aliyewazuia msiitii kweli? Ushawishi kama huo haukutoka kwa yule anayewaita. “Chachu kidogo huchachua donge zima.” 10 Nina hakika katika Bwana Isa kwamba hamtakuwa na msimamo mwingine. Mtu anayewachanganya anastahili adhabu, hata awe nani. 11 Lakini ndugu zangu, kama mimi bado ninahubiri kuhusu kutahiriwa, kwa nini bado ninateswa? Katika hiyo hali basi, kwazo la msalaba limeondolewa. 12 Laiti hao wanaowavuruga wangejihasi wao wenyewe!
13 Ndugu zangu, ninyi mliitwa ili mwe huru, hivyo msitumie uhuru wenu kama fursa ya kufuata tamaa za mwili, bali tumikianeni ninyi kwa ninyi kwa upendo. 14 Kwa maana Torati yote hukamilika katika amri moja: “Mpende jirani yako kama nafsi yako.” 15 Lakini mkiumana na kutafunana, angalieni msije mkaangamizana.
Maisha ya Kiroho
16 Kwa hiyo nasema, nendeni kwa Roho wa Mungu, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. 17 Kwa maana mwili hutamani yale yaliyo kinyume na Roho, naye Roho hutamani yale yaliyo kinyume na mwili. Roho na mwili hupingana na kwa sababu hiyo hamwezi kufanya mnayotaka. 18 Lakini mkiongozwa na Roho wa Mungu, hamko chini ya Torati.
19 Basi matendo ya mwili ni dhahiri, nayo ni haya: Uasherati, uchafu, ufisadi, 20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, 21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine yanayofanana na hayo. Nawaonya, kama nilivyokwisha kuwaonya kabla, kwamba watu watendao mambo kama hayo, hawataurithi ufalme wa Mungu.
22 Lakini tunda la Roho wa Mungu ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, 23 upole na kiasi. Katika mambo kama haya hakuna sheria. 24 Wote walio wa Al-Masihi Isa wameusulubisha mwili na shauku zake pamoja na tamaa zake. 25 Kwa kuwa tunaishi kwa Roho wa Mungu, basi, tuenende kwa Roho. 26 Tusijisifu bure, tukichokozana na kuoneana wivu.