5
Kutoka Adamu hadi Nuhu
(1 Nyakati 1:1-4)
Hii ni orodha iliyoandikwa ya vizazi vya Adamu.
 
Mungu alipomuumba mwanadamu, alimfanya kwa sura ya Mungu. Aliwaumba mwanaume na mwanamke, akawabariki. Walipokwisha kuumbwa, akawaita “Binadamu.”
 
Adamu alipokuwa ameishi miaka mia moja na thelathini, alimzaa mwana aliyekuwa na sura yake, mwenye kufanana naye. Akamwita jina Sethi. Baada ya Sethi kuzaliwa, Adamu aliishi miaka mia nane, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. Adamu aliishi jumla ya miaka mia tisa na thelathini, ndipo akafa.
Sethi alipokuwa ameishi miaka mia moja na tano, akamzaa Enoshi. Baada ya kumzaa Enoshi, Sethi aliishi miaka mia nane na saba (807), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. Sethi aliishi jumla ya miaka mia tisa na kumi na mbili (912), ndipo akafa.
Enoshi alipokuwa ameishi miaka tisini, akamzaa Kenani. 10 Baada ya kumzaa Kenani, Enoshi aliishi miaka mia nane na kumi na tano (815), naye alikuwa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 11 Enoshi aliishi jumla ya miaka mia tisa na tano (905), ndipo akafa.
12 Kenani alipokuwa ameishi miaka sabini, akamzaa Mahalaleli. 13 Baada ya kumzaa Mahalaleli, Kenani aliishi miaka mia nane na arobaini, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 14 Kenani aliishi jumla ya miaka mia tisa na kumi, ndipo akafa.
15 Mahalaleli alipokuwa ameishi miaka sitini na tano, akamzaa Yaredi. 16 Baada ya kumzaa Yaredi, Mahalaleli aliishi miaka mia nane na thelathini, akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 17 Mahalaleli aliishi jumla ya miaka mia nane tisini na tano (895), ndipo akafa.
18 Yaredi alipokuwa ameishi miaka mia moja na sitini na mbili (162), akamzaa Idrisi. 19 Baada ya kumzaa Idrisi, Yaredi aliishi miaka mia nane, naye akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 20 Yaredi aliishi jumla ya miaka mia tisa na sitini na mbili (962), ndipo akafa.
21 Idrisi alipokuwa ameishi miaka sitini na tano, akamzaa Methusela. 22 Baada ya kumzaa Methusela, Idrisi alitembea na Mungu miaka mia tatu, na akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 23 Idrisi aliishi jumla ya miaka mia tatu sitini na tano (365). 24 Idrisi akatembea na Mungu, kisha akatoweka, kwa sababu Mungu alimchukua.
25 Methusela alipokuwa ameishi miaka mia moja na themanini na saba (187), akamzaa Lameki. 26 Baada ya kumzaa Lameki, Methusela aliishi miaka mia saba na themanini na mbili (782), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 27 Methusela aliishi jumla ya miaka mia tisa sitini na tisa (969), ndipo akafa.
28 Lameki alipokuwa ameishi miaka mia moja na themanini na mbili (182), alimzaa mwana. 29 Akamwita jina Nuhu. Naye akasema, “Huyu ndiye atakayetufariji katika kazi ngumu ya mikono yetu yenye maumivu makali yaliyosababishwa na ardhi iliyolaaniwa na Mwenyezi Mungu.” 30 Baada ya Nuhu kuzaliwa, Lameki aliishi miaka mia tano na tisini na tano (595), akawa na watoto wengine wa kiume na wa kike. 31 Lameki aliishi jumla ya miaka mia saba sabini na saba (777), ndipo akafa.
32 Baada ya Nuhu kuishi miaka mia tano, aliwazaa Shemu, Hamu, na Yafethi.