9
Mwenyezi Mungu aweka agano na Nuhu
1 Ndipo Mungu akawabariki Nuhu na wanawe, akiwaambia, “Zaeni, mkaongezeke kwa idadi, na mkaijaze tena dunia. 2 Wanyama wote wa nchi, na ndege wote wa angani, na kila kiumbe kinachotambaa juu ya ardhi, na samaki wote wa baharini wamekabidhiwa mikononi mwenu, nao watawaogopa na kuwahofu. 3 Kila kitu chenye uhai kiendacho kitakuwa chakula chenu. Kama vile nilivyowapa mimea mbalimbali, sasa nawapa kila kitu.
4 “Lakini kamwe msile nyama ambayo bado ina damu, kwa maana damu ni uhai. 5 Hakika damu ya uhai wenu nitaidai. Nitaidai kutoka kwa kila mnyama. Kutoka kwa kila mwanadamu pia nitaidai kwa ajili ya uhai wa binadamu mwenzake.
6 “Yeyote amwagaye damu ya mwanadamu,
damu yake itamwagwa na mwanadamu;
kwa kuwa katika mfano wa Mungu,
Mungu alimuumba mwanadamu.
7 Bali ninyi, zaeni mwongezeke kwa idadi; zidini duniani na kuijaza.”
8 Ndipo Mungu akamwambia Nuhu na wanawe pamoja naye: 9 “Sasa mimi ninaweka agano langu nanyi, pamoja na uzao wenu baada yenu, 10 pia na kila kiumbe hai kilichokuwa pamoja nanyi: ndege, mifugo, na wanyama pori wote, wale wote waliotoka katika safina pamoja nanyi: kila kiumbe hai duniani. 11 Ninaweka agano nanyi: Kamwe uhai hautafutwa tena kwa gharika; kamwe hakutakuwa tena gharika ya kuangamiza dunia.”
12 Mungu akasema, “Hii ni ishara ya agano ninalofanya kati yangu na ninyi na kila kiumbe hai kilicho pamoja nanyi, agano kwa vizazi vyote vijavyo: 13 Nimeweka upinde wangu wa mvua mawinguni, nao utakuwa ishara ya agano nifanyalo kati yangu na dunia. 14 Wakati wowote ninapotanda mawingu juu ya dunia na upinde wa mvua ukatokea mawinguni, 15 nitakumbuka agano langu kati yangu na ninyi na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina. Kamwe maji hayatakuwa tena gharika ya kuangamiza uhai wote. 16 Wakati wowote upinde wa mvua unapotokea mawinguni, nitauona na kukumbuka agano la milele kati ya Mungu na viumbe vyote vilivyo hai vya kila aina duniani.”
17 Hivyo Mungu akamwambia Nuhu, “Hii ndiyo ishara ya agano ambalo nimelifanya kati yangu na viumbe vyote vilivyo hai duniani.”
Wana wa Nuhu
18 Wana wa Nuhu waliotoka ndani ya safina walikuwa: Shemu, na Hamu, na Yafethi. (Hamu ndiye alikuwa baba wa Kanaani.) 19 Hao walikuwa wana watatu wa Nuhu, na kutokana nao watu walienea katika dunia.
20 Nuhu akawa mkulima, akawa mtu wa kwanza kupanda mizabibu. 21 Alipokunywa huo mvinyo wake, akalewa na akalala uchi kwenye hema lake. 22 Hamu, baba wa Kanaani, akauona uchi wa baba yake na kuwaeleza ndugu zake wawili waliokuwa nje. 23 Lakini Shemu na Yafethi wakachukua nguo, wakaitanda mabegani mwao wote wawili, kisha wakaenda kinyumenyume, wakaufunika uchi wa baba yao. Nyuso zao zilielekea upande mwingine ili wasiuone uchi wa baba yao.
24 Nuhu alipolevuka na kujua lile mwanawe mdogo alilomtendea, 25 akasema,
“Alaaniwe Kanaani!
Atakuwa mtumwa wa chini kabisa
kwa ndugu zake.”
26 Pia akasema,
“Atukuzwe Mwenyezi Mungu, Mungu wa Shemu!
Kanaani na awe mtumwa wa Shemu.
27 Mungu na apanue mipaka ya Yafethi;
Yafethi na aishi katika mahema ya Shemu,
na Kanaani na awe mtumwa wake.”
28 Baada ya gharika, Nuhu aliishi miaka mia tatu na hamsini. 29 Nuhu aliishi jumla ya miaka mia tisa na hamsini, ndipo akafa.