16
Hajiri na Ishmaeli
1 Basi Sarai, mkewe Abramu, alikuwa hajamzalia watoto. Lakini alikuwa na mjakazi Mmisri jina lake Hajiri. 2 Hivyo Sarai akamwambia Abramu, “Mwenyezi Mungu amenizuilia kupata watoto. Basi nenda ukutane kimwili na mjakazi wangu; huenda nitaweza kupata watoto kupitia kwake.”
Abramu akakubaliana na lile Sarai alilosema. 3 Hivyo baada ya Abramu kuishi katika nchi ya Kanaani miaka kumi, Sarai akamchukua mjakazi wake Mmisri aliyeitwa Hajiri, na kumpa mumewe awe mke wake. 4 Abramu akakutana kimwili na Hajiri, naye akapata mimba.
Hajiri alipojua kuwa ana mimba, akaanza kumdharau Sarai. 5 Ndipo Sarai akamwambia Abramu, “Unawajibika na mateso ninayoyapata. Nilimweka mtumishi wangu mkononi mwako. Sasa kwa vile anajua kwamba ana mimba, ananidharau mimi. Mwenyezi Mungu na aamue kati yako na mimi!”
6 Abramu akamwambia, “Haya, mtumishi wako yuko mkononi mwako. Mtendee lolote utakalo!” Ndipo Sarai akamtesa Hajiri, naye akamtoroka.
7 Malaika wa Mwenyezi Mungu akamkuta Hajiri karibu na chemchemi huko jangwani; chemchemi hiyo ilikuwa kando ya barabara iendayo Shuri. 8 Malaika akamwambia, “Hajiri, mtumishi wa Sarai, umetoka wapi, na unaenda wapi?”
Akamjibu, “Ninamkimbia bibi yangu Sarai.”
9 Ndipo malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia, “Rudi kwa bibi yako ukajishushe chini yake.” 10 Malaika akaendelea akasema, “Nitazidisha wazao wako, hivi kwamba watakuwa wengi mno wasiohesabika.”
11 Pia malaika wa Mwenyezi Mungu akamwambia:
“Wewe sasa una mimba
nawe utamzaa mwana.
Utamwita jina lake Ishmaeli*maana yake Mungu husikia,
kwa sababu Mwenyezi Mungu amesikia kuhusu huzuni yako.
12 Atakuwa kama punda-mwitu kati ya wanadamu;
mkono wake utakuwa dhidi ya kila mtu,
na mkono wa kila mtu utakuwa dhidi yake,
naye ataishi kwa uhasama
na ndugu zake wote.”
13 Hajiri akampa Mwenyezi Mungu aliyezungumza naye jina hili: “Wewe ndiwe Mungu unionaye mimi,” kwa maana alisema, “Sasa nimemwona yeye anayeniona mimi.” 14 Ndiyo sababu kisima kile kikaitwa Beer-Lahai-Roi†maana yake Yeye Aliye Hai Anionaye; bado kipo hata leo kati ya Kadeshi na Beredi.
15 Hivyo Hajiri akamzalia Abramu mwana, naye Abramu akamwita huyo mwana Hajiri aliyemzalia jina la Ishmaeli. 16 Abramu alikuwa na umri wa miaka themanini na sita Hajiri alipomzalia Ishmaeli.