18
Wageni watatu
1 Mwenyezi Mungu akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre alipokuwa ameketi kwenye ingilio la hema lake wakati wa adhuhuri. 2 Ibrahimu akainua macho, akaona watu watatu wamesimama karibu naye. Alipowaona, akaharakisha kutoka ingilio la hema lake, akawalaki na kusujudu hadi chini.
3 Ibrahimu akasema, “Bwana wangu, ikiwa nimepata kibali machoni mwako, usimpite mtumishi wako. 4 Acha yaletwe maji kidogo, nanyi mnawe miguu yenu, na mpumzike chini ya mti huu. 5 Niruhusuni niwapatie chakula kidogo mle, ili mpate nguvu mwendelee na safari yenu, kwa kuwa mmekuja kwa mtumishi wenu.”
Nao wakamjibu, “Vema sana, fanya kama unavyosema.”
6 Hivyo Ibrahimu akaharakisha akaingia kwenye hema kwa Sara, akamwambia, “Chukua vipimo vitatu vya unga laini haraka, ukande na uoke mikate.”
7 Kisha Ibrahimu akakimbia kwenye kundi, akachagua ndama mzuri laini, na akampa mtumishi, ambaye aliharakisha kumtayarisha. 8 Kisha akaleta jibini, maziwa na nyama ya yule ndama iliyoandaliwa, akaviweka mbele ya wageni. Walipokuwa wakila, alisimama karibu nao chini ya mti.
9 Wakamuuliza, “Yuko wapi Sara mkeo?”
Akasema, “Yuko ndani ya hema.”
10 Kisha Mwenyezi Mungu akasema, “Hakika nitakurudia majira kama haya mwaka ujao, na Sara mkeo atakuwa na mwana.”
Sara alikuwa akiwasikiliza kwenye ingilio la hema lililokuwa nyuma ya Ibrahimu. 11 Ibrahimu na Sara walikuwa wazee tena waliosogea miaka, naye Sara alikuwa amepita umri wa kuzaa mtoto. 12 Hivyo Sara akacheka kimoyomoyo alipokuwa akiwaza, “Baada ya mimi kuwa mkongwe hivi na bwana wangu amezeeka, je, nitaweza kufurahia jambo hili?”
13 Ndipo Mwenyezi Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kwa nini Sara amecheka na kusema, ‘Kweli nitazaa mtoto nami sasa ni mzee?’ 14 Je, kuna jambo lolote gumu lisilowezekana kwa Mwenyezi Mungu? Nitakurudia majira kama haya mwaka ujao, naye Sara atakuwa na mwana.”
15 Sara akaogopa, hivyo akadanganya na kusema, “Mimi sikucheka.”
Lakini Mwenyezi Mungu akasema, “Ndiyo, ulicheka!”
Ibrahimu aiombea Sodoma
16 Watu hao waliposimama ili waondoke, walielekeza nyuso zao Sodoma, naye Ibrahimu akatembea nao ili awasindikize. 17 Ndipo Mwenyezi Mungu akasema, “Je, nimfiche Ibrahimu jambo ninalokusudia kufanya? 18 Hakika Ibrahimu atakuwa taifa kubwa na lenye nguvu, na kupitia kwake mataifa yote ya dunia yatabarikiwa. 19 Kwa maana nimemchagua yeye, ili awaongoze watoto wake na jamaa yake kufuata njia ya Mwenyezi Mungu, kwa kuwa waadilifu na kutenda haki, ili Mwenyezi Mungu atimize ahadi yake kwa Ibrahimu.”
20 Basi Mwenyezi Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi zao zinanisikitisha sana, 21 hivyo nitashuka nione kama waliyoyatenda ni mabaya kiasi cha kilio kilichonifikia. Kama sivyo, nitajua.”
22 Basi wale watu wakageuka, wakaelekea Sodoma, lakini Ibrahimu akabaki amesimama mbele za Mwenyezi Mungu. 23 Ibrahimu akamsogelea, akasema: “Je, utawaangamiza wenye haki na waovu? 24 Je, ikiwa watakuwepo watu hamsini wenye haki katika mji huo, kweli utauangamiza na wala hutauacha kwa ajili ya hao watu hamsini wenye haki waliomo? 25 Na liwe mbali nawe, kufanya jambo kama hilo: kuwaua wenye haki pamoja na waovu, kuwatendea wenye haki sawasawa na waovu. Liwe mbali nawe! Je, Mwamuzi wa dunia yote hatafanya haki?”
26 Mwenyezi Mungu akajibu, “Nikipata watu hamsini wenye haki katika mji wa Sodoma, nitauacha huo mji wote kwa ajili yao.”
27 Kisha Ibrahimu akasema tena: “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri wa kuzungumza na Bwana, ingawa mimi si kitu bali ni mavumbi na majivu. 28 Je, kama hesabu ya wenye haki imepungua watano katika hamsini, utauangamiza huo mji wote kwa ajili ya hao watano waliopungua?”
Bwana akamjibu, “Nikiwakuta huko watu arobaini na watano, sitauangamiza.”
29 Ibrahimu akazungumza naye kwa mara nyingine, “Je, kama huko watapatikana watu arobaini tu?”
Akamjibu, “Kwa ajili ya hao arobaini, sitauangamiza.”
30 Ndipo akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze. Je, kama huko watakuwepo thelathini tu?”
Akajibu, “Sitauangamiza ikiwa nitawakuta huko watu thelathini.”
31 Ibrahimu akasema, “Sasa kwa kuwa nimekuwa na ujasiri sana kuzungumza na Bwana, je, wakipatikana huko watu ishirini tu?”
Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao ishirini, sitauangamiza.”
32 Ibrahimu akasema, “Bwana na asikasirike, lakini niruhusu nizungumze tena mara moja tu. Itakuwaje kama watapatikana huko watu kumi tu?”
Bwana akajibu, “Kwa ajili ya hao kumi, sitauangamiza.”
33 Mwenyezi Mungu alipomaliza kuzungumza na Ibrahimu, akaondoka, naye Ibrahimu akarudi nyumbani.