25
Kifo cha Ibrahimu
Ibrahimu alioa mke mwingine aliyeitwa Ketura. Huyu alimzalia Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. Yokshani alikuwa baba wa Sheba na Dedani; wazao wa Dedani walikuwa Waashuru, Waletushi na Waleumi. Wana wa Midiani walikuwa Efa, Eferi, Hanoki, Abida na Eldaa. Hawa wote walikuwa uzao wa Ketura.
Ibrahimu akamwachia Isaka kila kitu alichokuwa nacho. Lakini Ibrahimu alipokuwa bado hai, akawapa watoto wa masuria wake zawadi, kisha akawaondoa waende kuishi pande za mashariki mbali na mwanawe Isaka.
Kwa jumla, Ibrahimu aliishi miaka mia moja na sabini na tano (175). Ndipo Ibrahimu akapumua pumzi ya mwisho na akafa akiwa mwenye umri mzuri, mzee aliyeshiba siku; naye akakusanywa pamoja na watu wake. Watoto wake Isaka na Ishmaeli wakamzika katika pango la Makpela karibu na Mamre, katika shamba lililokuwa la Efroni mwana wa Sohari Mhiti, 10 shamba ambalo Ibrahimu alilinunua kwa Wahiti. Hapo ndipo Ibrahimu alipozikwa pamoja na mkewe Sara. 11 Baada ya kifo cha Ibrahimu, Mungu akambariki mwanawe Isaka, ambaye baadaye aliishi karibu na Beer-Lahai-Roi.
Wana wa Ishmaeli
12 Hivi ndivyo vizazi vya Ishmaeli mwana wa Ibrahimu, ambaye Hajiri Mmisri, mjakazi wa Sara, alimzalia Ibrahimu.
 
13 Haya ndiyo majina ya wana wa Ishmaeli, walioorodheshwa kulingana na jinsi walivyozaliwa:
 
Mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli ni Nebayothi,
akafuatia Kedari, Adbeeli, Mibsamu,
14 Mishma, Duma, Masa,
15 Hadadi, Tema, Yeturi,
Nafishi na Kedema.
 
16 Hawa walikuwa wana wa Ishmaeli, na haya ni majina ya viongozi wa makabila yao kumi na mbili, kufuatana na makazi yao na kambi zao.
 
17 Kwa jumla Ishmaeli aliishi miaka mia moja na thelathini na saba (137). Akapumua pumzi ya mwisho, akafa, naye akakusanywa pamoja na watu wake. 18 Wazao wa Ishmaeli waliishi kuanzia nchi ya Havila hadi Shuri, karibu na mpaka wa Misri, kuelekea Ashuru. Hao waliishi kwa uhasama na ndugu zao wote.
Yakobo na Esau
19 Hivi ndivyo vizazi vya Isaka mwana wa Ibrahimu.
 
Ibrahimu akamzaa Isaka. 20 Isaka alikuwa na umri wa miaka arobaini alipomwoa Rebeka binti Bethueli Mwaramu*au Mshami kutoka Padan-Aramu, nduguye Labani Mwaramu.
21 Isaka akamwomba Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mke wake, kwa sababu alikuwa tasa. Mwenyezi Mungu akajibu maombi yake na Rebeka mkewe akapata mimba. 22 Watoto wakashindana tumboni mwake, naye akasema, “Kwa nini haya yanatokea kwangu?” Kwa hiyo akaenda kumuuliza Mwenyezi Mungu.
23 Mwenyezi Mungu akamjibu,
“Mataifa mawili yamo tumboni mwako,
na mataifa hayo mawili
kutoka ndani yako watatenganishwa.
Mmoja atakuwa na nguvu kuliko mwingine,
na yule mkubwa atamtumikia yule mdogo.”
24 Wakati wake wa kujifungua ulipotimia, walikuwepo mapacha wa kiume tumboni mwake. 25 Wa kwanza kuzaliwa alikuwa mwekundu, na mwili wake wote ulikuwa kama mtu aliyevaa vazi lenye nywele; wakamwita jina Esaumaana yake Mwenye nywele nyingi. 26 Baadaye, ndugu yake akatoka, mkono wake ukiwa umemshika Esau kisigino; akaitwa jina Yakobomaana yake Ashikaye kisigino, au Atwaaye mahali pa mwingine, au Mdanganyaji. Isaka alikuwa na umri wa miaka sitini Rebeka alipowazaa.
27 Watoto wakakua. Esau akawa mwindaji hodari, mtu wa mbugani, naye Yakobo akawa mtu mtulivu, mwenye kukaa nyumbani. 28 Isaka, aliyekuwa anapendelea zaidi nyama za porini, alimpenda Esau, bali Rebeka alimpenda Yakobo.
29 Siku moja Yakobo alipika mchuzi wa dengu. Esau akarudi kutoka porini akiwa na njaa kali. 30 Esau akamwambia Yakobo, “Haraka, nipe huo mchuzi mwekundu! Nina njaa kali sana!” (Hii ndiyo sababu pia aliitwa Edomu§maana yake Mwekundu.)
31 Yakobo akamjibu, “Niuzie kwanza haki yako ya mzaliwa wa kwanza.”
32 Esau akasema, “Tazama, mimi niko karibu kufa, itanifaa nini haki ya mzaliwa wa kwanza?”
33 Yakobo akamwambia, “Niapie kwanza.” Hivyo Esau akamwapia, akamuuzia Yakobo haki yake ya mzaliwa wa kwanza.
34 Ndipo Yakobo akampa Esau mkate na ule mchuzi wa dengu, naye akala na kunywa, kisha akainuka akaenda zake.
Kwa hiyo Esau akaidharau haki yake ya mzaliwa wa kwanza.

*25:20 au Mshami

25:25 maana yake Mwenye nywele nyingi

25:26 maana yake Ashikaye kisigino, au Atwaaye mahali pa mwingine, au Mdanganyaji

§25:30 maana yake Mwekundu